Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
UNESCO inasema kauli za chuki zinaongezeka duniani kote

Kauli za chuki ni hatari kwa kila mtu: Guterres

Unsplash/Jon Tyson
UNESCO inasema kauli za chuki zinaongezeka duniani kote

Kauli za chuki ni hatari kwa kila mtu: Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kauli za chuki ni hatari kwa watu wote na kila mtu anao wajibu wakuzuia kauli hizo katika jamii.

Katika taarifa yake iliyotolewa kwa waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kupinga kauli za chuki duniani amesema “Wote tuweke ahadi ya kutumia uwezo wetu wote kumaliza kauli za chuki kwa kuhamasisha kuenzi tofauti zetu na kujumuisha kila mtu” Mwaka jana (2021), Baraza Kuu LA Umoja wa Mataifa lilikutana ili kupitisha azimio la kutaka kuwepo na mazungumzo kuhusu tamaduni na dini mbalimbali ili kukabiliana na kauli za chuki pamoja na kutangaza Siku ya Kimataifa ambayo kwa mara ya kwanza inaadhimisha leo. Ukuaji wa mitandao ya kijamii unaelezwa kuwa moja ya visababishi vikubwa vinavyoeneza kauli za chuki, wakati wa janga la COVID-19 kulienea kauli za chuki dhidi ya watu wachache na hii kuthibitisha kuwa jamii nyingi ziko hatarini kwa unyanyapaa, unaguzi na mambo mengine yanayoendana na hayo. Guterres anasema ili kukabiliana na tishio hilo ndio maana “miaka mitatu iliyopita, nilizindua Mkakati na Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu kauli za chuki. Hii inatoa mfumo wa msaada wetu kwa Nchi Wanachama kukabiliana na janga hili huku zikiheshimu uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, kwa ushirikiano na mashirika ya kiraia, vyombo vya habari, makampuni ya teknolojia na majukwaa ya mitandao ya kijamii.” Hatari ya kauli za chuki Kauli za chuki zina chochea vurugu, hudhoofisha utofauti ndani ya jamii, na kutishia maadili na kanuni zinazo unganisha jamii kwa pamoja. Maneno haya yanapotumika yanaweza kuwa ni silaha na kusababisha madhara ya kimwili. Kuongezeka kutoka kwa matamshi ya chuki hadi ghasia kumechangia pakubwa katika uhalifu wa kutisha wa zama za kisasa, kutoka chuki dhidi ya Wayahudi inayoendesha mauaji ya Holocaust, hadi mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda. Kauli hizi zinapotumika zinakuza ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni, chuki dhidi ya wanawake, kudhalilisha watu binafsi na jamii, na ina athari kubwa kwa juhudi za kukuza amani na usalama, haki za binadamu na maendeleo endelevu SGDs.