Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika imekuwa kitovu cha ugaidi duniani: Guterres

Watoto wakicheza mbele ya kituo cha polisi huko Gao ambacho kilishambuliwa na magaidi.
UN Photo/Marco Dormino
Watoto wakicheza mbele ya kituo cha polisi huko Gao ambacho kilishambuliwa na magaidi.

Afrika imekuwa kitovu cha ugaidi duniani: Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 10 wa Umoja wa Mataifa wa kamati Kamati ya Kuratibu Mkataba wa Kimataifa wa Kupambana na Ugaidi barani Afrika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani, amesema, "taharuki hii inayoongezeka inateketeza mamilioni ya Waafrika. Hii inajumuisha wanawake na wasichana, ambao wako katika hatari kubwa ya unyanyasaji wa kijinsia na kikatili. Katika bara zima, Da'esh, Al-Qaida na washirika wao wanatumia mienendo ya migogoro ya ndani na udhaifu ili kuendeleza ajenda zao, huku wakisambaratisha mfumo wa kijamii wa nchi nzima na machafuko, kutoaminiana na hofu.”

Mathalani amesema nchini Somalia, kundi la kigaidi la Al-Shabaab liko chini ya shinikizo, lakini liko linaelekea kushindwa”.

Guterres ameendelea kusema kuwa huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, magaidi wanaendelea kuwalenga raia huku wakipanua wigo wa operesheni zao. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa “Ugaidi bado ni tishio kubwa kaskazini mwa Msumbiji. Pia katika Ukanda wa Sahel, kuongezeka kwa uhasama kati ya vikundi vya kigaidi vinavyopigania udhibiti wa maeneo na biashara haramu ni sawa na kuishi kuzimu hapa duniani kwa watu wasio na hatia waliojikuta katikati ya jinamizi hilo na tishio hilo linaenea kwa kasi katika nchi za pwani, kama inavyoonekana katika nchi za Benin na Togo.”

Guterres ameongeza kuwa mtindo huo wa kutatanisha uko bayana. Kuanzia kwenye jumuiya hadi kwa jamii, vikundi vya kigaidi vinapanua wigo wake iwe ni kukuza mitandao yao ya bara na wapiganaji zaidi, ufadhili, na silaha. Kuanzisha uhusiano na vikundi vya uhalifu wa kimataifa na kueneza hofu, taabu, na itikadi za chuki kupitia mtandao. Katika kila hali, raia wanalipa gharama kubwa zaidi. Lakini mwishowe, ubinadamu wote hulipa. Kila tishio la kigaidi, kila shambulio kali na la itikadi kali hudhoofisha juhudi zetu za pamoja za kujenga na kudumisha amani, maendeleo na utulivu barani Afrika. Ugaidi ni shambulio la kila jinsi kwa ustaarabu wetu.”

Familia zilizopoteza makazi yao katika majimbo ya kaskazini mwa Msumbiji yenye mgogoro wanaishi katika makazi ya muda.
© UNHCR/Martim Gray Pereira
Familia zilizopoteza makazi yao katika majimbo ya kaskazini mwa Msumbiji yenye mgogoro wanaishi katika makazi ya muda.

Mbinu za mapambano dhidi ya ugaidi

Guterres amesema "Ninataka kuangazia mambo mawili muhimu ya mtazamo wetu katika vita dhidi ya ugaidi na itikadi kali Kali ambayo ni

 Mosijuhudi zetu lazima zizingatiwe katika maendeleo endelevu na shirikishi. Ugaidi hupata makazi yake katika hali tete na kutokuwa na utulivu. Kutengwa, kukosekana kwa usawa, ufikiaji mdogo wa elimu, ukosefu wa ajira, kutokuwa na imani na serikali, taasisi na sheria, ukiukwaji wa haki za binadamu, na maoni ya kutokujali, kwa pamoja, hali hizi ni chachu ya kuenea kwa ugaidi. “

Hivyo amesema “Tunahitaji kukomesha mzunguko huu mbaya. Ajenda mpya ya amani inaweka msisitizo mpya katika kuzuia. Inaunganisha nukta kati ya kuwekeza katika maendeleo, kujenga miundo thabiti ya utawala na mifumo ya haki ambayo watu wanaweza kuamini, na kuunda amani endelevu.”

Pili,  amesema “juhudi zetu lazima zizingatie katika haki za binadamu. Ugaidi unawakilisha kunyimwa haki za binadamu. Hatuwezi kupambana nao kwa kurudia ukanushaji uleule. Mara nyingi, hatua za kukabiliana na ugaidi hutumiwa vibaya au zina matokeo yasiyotarajiwa zinapotekelezwa, na kusababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Hiki ni kichocheo cha chuki, manung'uniko makubwa, vifo na uharibifu zaidi".

Kwa hivyo, Guterres amesema “Hatua zetu za pamoja dhidi ya ugaidi lazima zijikite katika kanuni zinazofafanua ubinadamu wetu wa pamoja, kuheshimu haki za binadamu, utawala wa sheria, na kutafuta amani. Na lazima ziwekwe katika mikakati inayoakisi jamii zilizotengwa na zilizo hatarini. “

Kaskazini mwa Chad ambako makundi ya kigaidi yanaendesha shughuli zao wanawake wanaweza kulazimishwa kuolewa.
UN News/Daniel Dickinson
Kaskazini mwa Chad ambako makundi ya kigaidi yanaendesha shughuli zao wanawake wanaweza kulazimishwa kuolewa.

Wanawake na wasichana ni waathirika wakubwa

Kwa mfano, Katibu Mkuu amesema makundi kama  wanawake na wasichana mara nyingi ni wa kwanza kukubwa na changamoto sa usalama na waathirika wakubwa zaidi wa ugaidi. 

Ameongeza kuwa licha ya kutofautiana kwa itikadi, makundi mengi ya kigaidi yana mkakati mmoja sawa,” utiifu wa mfumo wa kikatali kwa wanawake na wasichana, na vitendo vya unyanyasaji wa kutisha dhidi yao.”

Guterres amehitimisha kwa sema kuwa “kuanzia wasichana wa shule ya Chibok wa nchi ya Nigeria hadi wanawake na wasichana wa Yezidi nchi Iraq, miaka ya hivi karibuni imeshuhudia mifano ya kutisha ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na hata utumwa wa moja kwa moja, ikiwa ni pamoja na wanawake wanaouzwa ili kufadhili shughuli za kigaidi. Lazima tuzingatie vipaumbele na mikakati yetu ya kukabiliana na ugaidi katika suala hili muhimu, ambalo linakata ari ya ahadi yetu ya haki za binadamu za watu wote, ikiwa ni pamoja na usalama na uhuru wa wanawake na wasichana.”

Afrika ni nyumba ya matumaini.

Hatimaye, Guterres amethibitisha tarifa yake kwa kusema kwamba, “Afrika, kwangu, ni nyumba ya matumaini, bara lenye uwezo mkubwa, ambalo liko tayari kukabiliana na changamoto za karne ya 21. Lakini uwezo huu unaweza kupatikana tu kwa kushinda kivuli cha ugaidi ambacho kinasambaa kwa kasi katika bara zima. Hatuna muda wa kupoteza”.