Vijana tumieni mitandao ya kijamii kujiendeleza

2 Januari 2018

Nchini Afghanistan, vijana wametakiwa kutumia fursa ya mitandao ya kijamii ili kujikwamua kimaendeleo. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta Massoi)

Vijana wa Kike na wa kiume nchini Afghanistani walikutana kwa siku tano huko Herat ambako lengo kubwa lilikuwa kuwahamasisha juu ya kujiendeleza na kuepuka vitendo vya kigaidi.

Baraza la mashauriano la vijana  linaloangazia masuala ya maendeleo, vita dhidi ya vitendo vya kigaidi na pia hamasa kwa  vijana nchini Afghanistan liliandaa jukwaa hilo la vijana kwa udau na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA.

Vijana walichangia mawazo mbalimbali ikiwemo mikakati ya kupiga vita itikadi za kigaidi na fursa za ajira kwa vijana  ambao ni waathirka wakubwa wa ajira  nchini Afghanistan.

Bwana Tawab Mobarez, ambaye ni mratibu wa kitengo cha vijana kwenye serikali ya jimbo la Herat  na pia msemaji mkuu katika kongamano hilo alisema baada ya kuzungumza na vijana wengi, ni dhahiri kwamba swala la amani, usalama , na pia vita dhidi ya  itikadi ya  kigaidi kwa vijana ni suala mtambuka ambalo litawanusuru vijana katika  fikra potofu na za kimasikini.

Pia alishukuru jitihada za UNAMA kuandaa kongamano hilo ambalo ni jitihada za kutambua umuhimu wa vijana  nchini humo, ambao ndio msingi wa mustakabali wa uchumi wa nchi hiyo.

UNAMA imeendelea na mikakati ya kuwafikia vijana, wazee, wanawake nchini Afghanistan katika  jitihada za kutafuta amani ya kudumu na pia maendeleo kwa jamii yote kwa ushirikiano na serikali na pia asasi za kiraia.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud