Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutake tusitake lazima tupambane na ugaidi ni tishio la kimataifa:Voronkov

Familia ikihama kutoka nyumba yao iliyosambaratishwa muda mchache baada ya mshambuliaji wa kujilipua wa ISIS kujilipua kwenye gari kwenye moja ya mitaa huko Al Andalus, kitongoji cha Mosul nchini Iraq.
UNHCR/Ivor Prickett
Familia ikihama kutoka nyumba yao iliyosambaratishwa muda mchache baada ya mshambuliaji wa kujilipua wa ISIS kujilipua kwenye gari kwenye moja ya mitaa huko Al Andalus, kitongoji cha Mosul nchini Iraq.

Tutake tusitake lazima tupambane na ugaidi ni tishio la kimataifa:Voronkov

Amani na Usalama

Vita dhidi ya ugaidi ni lazima , na ili kufanikiwa wadau wote wakiwemo wataalamu, viongozi wa nchi na asasi za kiraia lazima washirikishwe.

Hayo yamesemwa na msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya umoja huo ya kupambana na ugaidi Bwana. Vladimir Voronkov alipohohiwa na UN News kuhusu mkutano wa kimataifa wa vita dhidi ya ugaidi.

Bwana. Voronkov amesema mkutano huo wa ngazi ya juu ambao ni wa kwanza wa aina yake utakaowaleta pamoja wakuu wa mashirika ya kupambana na ugaidi duniani, ni tukio muhimu sana kwa sababu watu hawa wanakutana kwa mara ya kwanza na itawapa fursa ya kuzungumza kwa kauli moja kama wataalamu, kitu ambacho ni kigeni kabisa kwa Umoja wa Mataifa na kwa mchakato wa kupambana na ugaidi,  lakini pia ni fursa muhimu kwa pande zote husika kwa sababu kuu tatu ,

(SAUTI YA VLADIMIR VORONKOV-1)

“Kwanza kabisa kuonyesha mshikamano wetu katika vita dhidi ya ugaidi na kuzuia ukatili wa itikadi kali, pili agenda ya mkutano huu ilifafanuliwa kwa pamoja na nchi wanachama na kutakuwa na vikao vinne tofauti vitakavyoandaliwa ili kupata taswira kamili kuhusu matokeo ya majadiliano hayo.

Na ni ajenda zipi zinatazotamalaki?

 Vladimir Voronkov, msaidizi wa Katibu Mkuu katika vita dhidi ya ugaidi, akihutubia Baraza la Usalama.
Picha/Loey Felipe
Vladimir Voronkov, msaidizi wa Katibu Mkuu katika vita dhidi ya ugaidi, akihutubia Baraza la Usalama.

(SAUTI YA VORONKOV 2)

Mada ya kwanza itakayojadiliwa itakuwa ni kubadilishana taarifa, ni muhimu sana kwa wakati huu baada ya kundi la ISIL kushindwa kijeshi nchini Iraq na Syria na ni muhimu sana kuelewa jinsi gani ya kuzuia uwezekano wa tishio kutoka kwa wapiganaji magaidi toka nje. Pili ni mada kuhusu wapiganaji magaidi kutoka nje , ni watu wengi sana takribani maelfu ya watu, hivyo hatua ya pamoja kuhusu suala hili muhimu na la hatari sana inahitajika. Tatu itakuwa ni mada ya kuzuia ghasia za itikadi kali ikiwemo matumizi mabaya ya teknolojia mpya. Nadhani pia ni muhimu kwa sababu bila uwepo wa asasi za kiraia ni vigumu kuongea kuhusu jamii zenye mnepo katika sehemu mbalimbali duniani.”

Na kuhusu matumizi ya tekinolojia kama kutumia mitandao, Je imegeuka uwanja mpya wa mapambo ya kigaidi?

(SAUTI YA VORONKOV 3)

“Kwa kiasi fulani ndio, hali hii ni mpya na uwanja mgumu wa mapambano kwa sababu, bila shaka magaidi wana ujuzi wa hali ya juu katika nyanja hii ya shughuli zao, na vita dhidi ya ugaidi vinategemea ni jinsi gani tumejizatiti katika karne hii ya intaneti na jinsi gani tunaweza kuandaa mapigo ya kuukabili ugaidi, jinsi gani tunaweza kuzuia shambulio lolote la kigaidi kwa kutumia intaneti. Hivyo ni uwanja muhimu wa mapambano.

Bwaba Voronkov pia amezungumzia umuhimu wa kuwafikia vijana ambao wako hatarini kutumbukia kwenye itikadi kali akisema kwamba vijana walio katika maeneo yenye shughuli nyingi za wanamgambo kama Mali Kaskazini , wanahitaji kufikiwa katika ngazi ya mashinani ili kupambana na propaganda za kigaidi.

(SAUTI YA VORONKOV 4)

“Nadhani ni muhimu sana kwa upande huu wa haki za binadamu, upande ambao utaonyesha kwamba binadamu hawa mazingira waliyomo sio rahisi, kwa sababu maisha yao yaliwekwa hatarini na magaidi na wanaowaingiza kutoka makundi ya wanamgambo wenye silaha.”

Mkutano huo wa kimataifa na wa ngazi ya juu katika vita dhidi ya ugaidi utafanyika kwenye makao makuu ya umoja wa Mataifa mjini New York Marekani wiki ijayo