Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante MONUSCO kwa kutuimarishia usalama; Wasema wakazi wa Ituri, DRC

Mama mkimbizi wa ndani akibeba kuni. anayeishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani kwenye kambi za wakimbizi Ituri, DRC.
UN News
Mama mkimbizi wa ndani akibeba kuni. anayeishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani kwenye kambi za wakimbizi Ituri, DRC.

Asante MONUSCO kwa kutuimarishia usalama; Wasema wakazi wa Ituri, DRC

Amani na Usalama

Katika Kambi ya Lodha, iliyoko kijijini Dzina, katika kitongoji cha Walendu-Bitsi, eneo la Djugu na ile ya Jaiba, katika eneo la uchifu la Bahema-Badjere jimboni Ituri, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, doria za usiku na mchana hufanywa kila wakati na walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo MONUSCO.  

Soundcloud

Mmoja wa wanufaika ni Lobi Tsubavile Flavien ambaye ni mkimbizi wa ndani na pia  kiongozi wa shirika moja la kiraia anasema, MONUSCO imeweka taa za barabarani katika maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na Kituo cha Fataki, huko Djugu, Bule na Gina.”  

Katika jimbo la Ituri, watu waliokimbia makazi yao wanaishi katika takribani kambi 38, ambapo miongoni mwao ni Drodro, Roe, Lodha, Jaiba na Gina. Zaidi ya wakimbizi wapatao 400,000 wanafaidika na ulinzi wa moja kwa moja wa ujumbe wa walinda amani wa MONUSCO.    

Walinda amani hao wakiwemo wale wa kutoka Nepal hulinda kambi za watu waliohamishwa kwa kufanya doria za usiku na mchana. Na zaidi ya yote MONUSCO imeweka miundombinu ya kuhakikishia raia usalama wao, moja ya majukumu ya ujumbe huo ambao kwa sasa unaanza kufunga virago taratibu kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia ombi la serikali ya DRC.  

Bwana Lobi anaendelea kusema, “Naamini kuwa taa zote zilizowekwa barabarani na mengine yote ya doria ni kwa ajili ya ulinzi wa raia na kuwalinda watu usiku. Hatuwezi kusahau hilo kamwe.  Sisi binafsi tunaihitaji MONUSCO.”  

Anasema anadhani katika maeneo mengine ambayo MONUSCO haijathaminiwa na wanasiasa, ni kwa sababu tu “kuweko kwa taarifa za uongo kuwa MONUSCO haifanyi chochote.  Hayo si maoni yetu. MONUSCO ililinda idadi ya watu katika LODA, JAIBA, wakimbizi kwenye kambi ya GINA na DRODRO"  

Mbele ya MONUSCO, adui hatokei tena, tunalima kwa amani 

Mtazamo wa MONUSCO Ituri unatolewa pia na Akiki Astrid, mkulima huyu akiwa na jembe lake shambani anasema, "Mimi natokea kwenye kambi la Djaiba naenda shambani. Huko tunalindwa na walinda amani wa Monusco. Tunapomaliza shughuli zetu tunarudi pamoja nao. Zamani wakati tulikua tukienda pasipo ulinzi, waasi walitushambulia, ila tangu tunalindwa na Monusco, adui hatokei tena. Kwa hiyo tunasema asante kwa kazi MONUSCO anafanya"  

Ulinzi wa raia unasalia kuwa msingi wa majukumu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, amesisitiza Karna Soro, mkuu wa ofisi ya MONUSCO jimboni Ituri akisema,  

"Tunafanya kazi na viongozi wa Ituri kuweka utaratibu wa kuendeleza vikao vya mazungumzo ambavyo vimewekwa.  Katika mwaka uliopita, MONUSCO iliandaa mazungumzo ya mchango wa jumuiya.  MONUSCO iliunga mkono serikali ya jimbo katika majadiliano na makundi yaliyojihami, ambayo yaliruhusu kutiwa saini kwa makubaliano ya wao kuacha mauaji.”  

Amesema MONUSCO pia ilifanya kazi na serikali katika kikao cha amani huko NAIROBI, KENYA. Monusco pia imesaidia pia serikali ya jimbo kutekeleza kile tunachoita hapa kuwa mazungumzo ya ARU, ambayo yaliruhusu vikundi vyenye silaha kusaini tena mkataba huo na kuthibisha nia yao ya kusitisha mapigano.  

Wakazi wa Djugu wanaishi kwa kiasi kikubwa kwa kutegemea shughuli za kilimo na hivyo wakati makundi yaliyojihami yanapowashambulia, inakuwa vigumu sana kwa wao kufika mashambani kwa ajili ya kilimo.  

 

Ripoti hii imeandaliwa na GEORGE MUSUBAO, wa UN News mashariki mwa DRC.