Watu 117 waliuawa Ituri, DRC katika siku 4 za mwezi huu wa Juni pekee- Ripoti

28 Juni 2019

Takribani watu 117 waliuawa kwenye jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRc kati ya tarehe 10 na 13 mwezi huu wa Juni kutokana na mapigano kati ya kabila la wahema na walendu.

Takwim hizo zimepatikana baada ya uchunguzi uliofanywa na ofisi ya pamoja ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inayojumuisha kitengo cha haki za binadamu cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Uchunguzi huo ulifanyika kufuatia mfululizo wa mashambulizi kwenye vijiji vya maeneo ya Djugu na Mahagi ambapo jopo husika limethibitisha mauaji ya watu 94 yalifanyika huko Djugu na watu wengine 23 waliuawa huko Mahagi, wakiwemo wanawake na watoto.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Marta Hurtado amesema,

Sauti ya Marta Hurtado

 “Baadhi ya waathirika walikatwa vichwa. Nyumba na bohari ziliteketezwa kwa moto baada ya mali kuporwa. Kiwango cha uchomaji kilichoonekana kinadokeza kuwa washambuliaji walilenga kuzuia manusura wasiweze kurejea kwenye vijiji vyao. Idadi kubwa ya waathirika ni wahema na kabila la Alur. Washambuliaji wameripotiwa kutoka kabila la walendu.”

Ingawa awali ilionekana kuwa chanzo ni ukabila baada ya kudaiwa kuwa mashambulizi yalikuwa ni kulipiza kisasi baada ya watu wanne wa kabila la walendu kuuawa, uchunguzi umedokeza kuwepo kwa vichocheo vya kisiasa na kiuchumi.

Bi. Hurtado amesema pamoja na kutaka serikali ya DRC kuchunguza kwa kina na kwa huru ili wahusika wafikishwe mbele ya sheria,

Sauti ya Marta Hurtado

“Tunasihi pia serikali ichunguze kitendo cha jeshi kutoweza kuzuia au kukomesha mauaji na ichukue hatua za lazima kulinda wananchi kwenye eneo hili.

Mashambulizi ya mara kwa mara  huko Ituri yamesababisha watu kukimbia makazi yao na kuelekea miji mingine pamoja na kuishi kwenye kambi za muda ambazo kwa sasa zinahifadhi watu elfu 78.

 

TAGS: DRC, OHCHR, MONUSCO, ITURI, Marta Hurtado

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud