Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ituri hali si shwari watu 30 wauawa, maelfu wakimbilia Uganda

Kamanda wa doria kutoka kikosi cha Bangladesh kinachohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko DRC, MONUSCO akisalimiana na Chifu wa kijiji cha ADA huko jimbo la Ituri, mashariki mwa DRC.
MONUSCO
Kamanda wa doria kutoka kikosi cha Bangladesh kinachohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko DRC, MONUSCO akisalimiana na Chifu wa kijiji cha ADA huko jimbo la Ituri, mashariki mwa DRC.

Ituri hali si shwari watu 30 wauawa, maelfu wakimbilia Uganda

Amani na Usalama

Hali si shwari huko jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako watu 30 wameuawa wakati wa mapigano ya kikabila huku maelfu wakiendelea kumiminka nchi jirani. Selina Jerobon na ripoti kamili.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linasema lina wasiwasi mkubwa juu ya mapigano hayo kati ya wahema na walendu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo msemaji wa UNHCR Babar Baloch amesema mgogoro huo umekuwa ukijirudiarudia kwa muda mrefu akitaja mwaka 1999 na 2003.

Amesema mapigano ya hivi karibuni zaidi yamesababisha raia kukimbilia Uganda.

(Sauti ya Babar Baloch)

“UNHCR inaendelea kufualia kwa karibu mgogoro huu, ambapo taarifa za awali zinasema kuna zaidi ya  wakimbizi 1000 wamepokelewa katika kambi za wakimbizi nchini Uganda mwanzoni mwa wiki hii kupitia ziwa Albert, ambapo ni umbali wa kilomita 250 kaskazini mwa mji mkuu kampala. Tuna wasiwasi mgogoro huu unaweza kuathiri maeneo mengine katika jimbo hili kutokana na kasi ya kuenea kwa silaha katika ukanda huu.”

Bwana Baloch ametoa wito kwa pande zote kinzani kufikia suluhisho la amani katika janga hilo na pia   amesihi mashirika ya kibinadamu kutoa misaada ya dharura kwa wahitajii wakubwa katika mgogoro huu ambao ni watoto, wazee na wanawake.