Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili huko Ituri ni wa kutisha, waliorejea walazimika kukimbia tena- UNHCR

Madaktari kutoka kikosi cha Morocco kilichopo kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO wakipatiwa matibabu wakimbizi waliokimbia mapigano jimbo la Ituri.
UN /Christophe Boulierac
Madaktari kutoka kikosi cha Morocco kilichopo kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO wakipatiwa matibabu wakimbizi waliokimbia mapigano jimbo la Ituri.

Ukatili huko Ituri ni wa kutisha, waliorejea walazimika kukimbia tena- UNHCR

Amani na Usalama

Ni jambo la kusitikisha pale ambapo mtu amejiandaa kurejea nyumbani baada ya kuishi ugenini, lakini hatimaye analazimika kukimbia tena kutokana na kukuta makazi  yake yamechomwa moto na mali nyingine nyingi zimeharibiwa. Huko ni Ituri, DRC ambako wahema na walendu wanapambana.

Baada ya miezi kadhaa ya mzozo kati ya kabila la wahema na lile la walendu kwenye jimbo la Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeweza kufika eneo ambako wamekutana na watu 150,000 waliofurushwa ambao sasa wanarejea kwa imani ya kupata nyumba zao.

Hali ni mbaya kwenye eneo hilo, imesema UNHCR na kuongeza kuwa takriban watu 350,000 waliofurushwa makwao wamekuta nyumba zao ziliteketezwa na hivyo kulazimika kukimbia tena.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi msemaji wa UNHCR Charlie Yaxley amesema..

“Timu yetu imesikia ripoti za kusikitisha kuhusu vitendo vya kikatili, ikiwemo vikundi vilivyojihami kuvamia raia kwa kutumia bunduki, mikuki, mapanga na vijiji kuteketezwa,  na mashamba na maduka kuvamiwa na kuporwa na kuharibiwa kabisa.”

UNHCR imeongeza kwamba changamoto ni nyingi huku hospitali, shule na miundombinu muhimu vimeharibiwa kabisa.

Halikadhalika UNHCR imeelezea wasiwasi wake kuhusu idadi ya watoto wanaougua utapiamlo uliokithiri na wanaohitaji huduma ya dharura ya afya.

“Wakati huo huo, hali ni mbaya katika maeneo ya watu waliofurushwa. Katika maeneo mengi hakuna maji safi, huduma ya afya na vifaa vya kujisafi. Hali inatia wasiwasi katika eneo la wakimbizi karibu na hospitali kuu ya Bunia ambako kuna hatari kubwa ya magonjwa kusambaa.”

UNHCR imesema ukosefu wa ufadhili unakandamiza juhudi za uwasilishaji msaada huku ikitaja kupokea asilimia 17 tu ya ombi la dola milioni 201 kwa ajili ya msaada wa dharura ndani ya DRC.

Kwa mantiki hiyo UNCHR imetolea wito wafadhili kwani DRC ni miongoni mwa nchi zilizofadhiliwa kwa kiasi kidogo duniani.

TAGS: UNHCR, DRC, Hema, Lendu, msaada wa kibinadamu