Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa mawili Israel na Palestina, "njia pekee ya kufikia amani ya kudumu" - Guterres

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Wapalestina.
UN Photo/Eskinder Debebe
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Wapalestina.

Mataifa mawili Israel na Palestina, "njia pekee ya kufikia amani ya kudumu" - Guterres

Amani na Usalama

Wakati vita huko Gaza ikiwa sasa imedumu kwa zaidi ya miezi mitatu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Januari 23 ameendelea kusisitiza kwa Baraza la Usalama kwamba uwepo wa mataifa mawili, Israel na Palestina zikiishi bega kwa bega kwa amani na usalama, ndiyo njia pekee ili kupata amani ya kudumu”.

"Jukumu la jumuiya ya kimataifa liko wazi. Ni lazima tuje pamoja ili kuwaunga mkono Waisraeli na Wapalestina kuchukua hatua madhubuti kuelekea mchakato wa kweli wa amani,” mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameuambia mkutano wa Baraza la Uslama uliolenga hali ya Gaza.

"Katika miongo miwili iliyopita, suluhisho la serikali mbili limekosolewa, kudharauliwa, na kuachwa mara kwa mara. Hata hivyo, inasalia kuwa njia pekee ya kufikia amani ya kudumu na ya usawa – nchini Israel, Palestina na katika eneo zima,” amesisitiza akiongeza kusema, "kama tulivyoona katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, pia ni njia pekee ya kutoka kwa mizunguko isiyoisha ya hofu, chuki na vurugu."

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, "wakati huu wa kutisha kwa Waisraeli na Wapalestina lazima uwahimize pande zinazohusika katika mzozo huo, pamoja na jumuiya ya kimataifa, kuchukua hatua kwa ujasiri na azma ya kufikia amani ya haki na ya kudumu."

Mkutano ulioongozwa na Ufaransa

Mkutano huu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umeanza mchana saa nane saa za New York, Marekani ili kutathmini hali ya Gaza, ambako operesheni ya kijeshi ya Israel imeendelea bila kusitishwa kwa zaidi ya miezi mitatu kulipiza kisasi mashambulizi ya umwagaji damu ya Hamas nchini Israel.

Mkutano huo unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Stéphane Séjourné, ambaye nchi yake inashikilia zamu ya urais wa Baraza la Usalama mwezi Januari.

Mawaziri wengine wa mambo ya nje pia wanashiriki katika mkutano huu, wakiwemo wa Algeria, Ahmed Attaf, wa Slovenia, Tanja Fajon, na wa Urusi, Sergei Lavrov.

Mkutano huo unafanyika katika muktadha wa uwezekano wa mgogoro Kwenda mbali zadi ya Gaza ambapo kumekuwa na kurushiana risasi mara kwa mara kati ya vikosi vya Israel na Hezbollah nchini Lebanon na kuongeza mashambulizi ya anga yanayofanywa na Marekani na Uingereza dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen, wanaoshambulia meli katika Bahari ya Shamu, ikiwa ni ishara ya mshikamano na wanaharakati wa Kipalestina.