Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2024 rasmi kiswahili kuanza kutumika EAC

Dkt. Peter Mathuki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
UN News
Dkt. Peter Mathuki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mwaka 2024 rasmi kiswahili kuanza kutumika EAC

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kwa watafsiri na wakalimani wa lugha ya Kiswahili, mwaka 2024 huwekakuwa wa neema kwao kwani jumuiya ya Afrika Mashariki EAC imetangaza rasmi kuanzia mwaka huu lugha hiyo itaanza kutumika rasmi katika vikao na mikutano yake yote pamoja na makabrasha yote kutolewa kwa lugha hiyo. 

Akizungumza katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Dkt. Peter Mathuki amemueleza Leah Mushi kuwa tayari bajeti ya jumuiya ya 2023 imepitishwa na inafungu la kuwezesha lugha tatu kutumika ambazo ni Kingereza, Kifaransa na Kiswahili. 

“Ukiangalia bajeti yetu ya mwaka huu tumeweka mikakati yote ya kuwa na watafsiri wa makablasha yote kwa lugha ya kiingereza, kiswahili na kifaransa. Kwa hivyo pia tuta tafuta wataalamu wa lugha ya Kiswahili tuwaajiri watusaidie kufanya hiyo kazi. “ 

Kiswahili kilitangazwa rasmi kutambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO ambapo tarehe 7 ya mwezi Julai kila mwaka dunia inaadhimisha siku hiyo na Katibu Mkuu huyo wa EAC ameeleza kuwa eneo lao Afrika la Mashariki wanaitegemea sana lugha hiyo.

“Kiswahili tunakitegemea sana sababu wananchi wengi katika jumuiya yetu wanaelewa lugha ya Kiswahili kwahiyo hii sasa itakuwa kazi yetu sisi kama watendaji wa jumuiya kuhakikisha kwamba habari zote na vikao vyote vinafanyika kwa lugha ya Kiswahili.”

Dkt. Mathuki alieleza pia kwanini imechukua muda mrefu kwa lugha hiyo kuanza kutumika rasmi ilihali wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo walishatoa maelekezo ya lugha hiyo kutumika rasmi katika vikao yake. 

“Shida ilikuwa ni Kiswahili hakikuwepo kwenye katiba ya jumuiya, lakini sasa baada ya kusema turekebishe katiba ya jumuiya na kuweka lugha hiyo si tu bungeni bali kwenye vikao vyote vya jumuiya na hiyo sasa tumeanza mikakati yake.” 

Somalia mwanachama mpya EAC

Kikao cha 23 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliridhia na kutangaza rasmi nchi ya Somalia kujiunga rasmi na jumuiya hiyo kama mwanachama na kuwa mwanachama wa nane akijiunga na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC.

Hafla ya kuikaribisha rasmi nchi hiyo zilifanyika nchini Uganda ambapo Katibu Mkuu Dkt Mathuki alieleza umuhimu wa taifa hilo kujiunga na jumuiya. 

“Kuongezeka kwa nchi ya nane katika jumuiya yetu ina maana kwanza soko linazidi kupanuka sasa tunakuwa na watu karibu milioni 350 hili ni soko kubwa sana, litatoa nafasi nyingi za ajira na kibiashara. Lakini pia ukiangalia ukanda wa pwani wa Somalia una urefu wa takriban km kama 3,300 hiyo itachangia pakubwa hasa kibiashara.“

Ameongeza kuwa “fursa hizo za biashara ni furaha kubwa kwa jumuiya kwa sababu vijana sasa wako na nafasi ya kusafiri katika nchi zote hizo za jumuiya mahali popote kutafuta ajira na nafasi za kibiashara.”

Kuhusu suala la ulinzi na usalama wa Somalia Dkt.Mathuki ameeleza kuwa sasa kwakuwa nchi hiyo ni mwanachama wanaweza kuwa nayo pamoja na kuisaidia katika changamoto za kiusalama na mambo mengine. 

Ushirikiano na Umoja wa Mataifa 

Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekuwa zikishirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo suala la ulinzi na usalama wa wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo - DRC ambayo kwa muda mrefu inabiliwa na mzozo hususan mashariki mwa nchi hiyo. 

“Katika jumuiya yetu ya EAC ni wajibu wetu kuhakikisha nchi zote zinaishi kwa amani na usalama , kwahivyo mambo ya usalama hasa mashariki mwa DRC nijambo linalochukuliwa kwa uzito sana na wakuu wa nchi wanachama ambao walisema watume majeshi kule, lakini pia suala la pili likawa ni kutumia diplomasia ambapo makundi yaliyopo DRC yalitakiwa kujiunga pamoja na kuzungumza na mwezeshaji ili kujua namna ya kusaidia kutatua shida walizonazo. “ 

Dkt. Mathuki ameeleza kuwa haya yote wanayafanya kwa ushirikiano wa karibu na Umoja wa Mataifa ambao wana Ujumbe wake wa kulinda amani nchini DRC – MONUSCO. “Tunafanya kazi na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa hasa kupitia Baraza lake la Usalama, tunashirikiana kwa kupeana taarifa na kwa pamoja tunaona ni kwa namna gani tutasaidia DRC kutoka kwenye changamoto waliyonayo lengo likiwa ni kuwasaidia wananchi wa DRC.”