Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakuu wa Afrika Mashariki wanasemaje kuhusu ujio wa DRC ndani ya EAC?

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa na Rais wa DRC Felix Tshisekedi mjini Kinshwasa Septemba 2, 2019
MONUSCO/Michael Ali
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa na Rais wa DRC Felix Tshisekedi mjini Kinshwasa Septemba 2, 2019

Wakuu wa Afrika Mashariki wanasemaje kuhusu ujio wa DRC ndani ya EAC?

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Wakati mwishoni mwa mwezi huu, tarehe 24, ulimwengu utakuwa unaadhimisha siku ya kimataifa ya ushirikiano wa kimataifa na matumizi ya diplomasia kwa ajili ya amani, nchi za ukanda wa Afrika Mashariki zitakuwa zinajivunia kuendelea kutimiza kwa vitendo lengo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitisha azimio namba A/RES/73/127 tarehe 12 mwezi Desemba mwaka 2018 la kuhifadhi na kusongesha ushirikiano baina ya mataifa ambao ndio msingi wa mkataba wa Umoja wa Mataifa na ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu na pia msingi wa nguzo kuu tatu za Umoja wa Mataifa ambazo ni amani na usalama, maendeleo na haki za binadamu. 

Wiki iliyopita, Ijumaa ya tarehe 8 Aprili mwaka huu wa 2022, Kikao cha 19 cha marais wa Jumuiya ya Afrika mashariki kiliridhia nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iwe mwanachama wa Jumuiya hiyo. 

Ni siku ambayo ilianza na hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya Nairobi nchini Kenya kwenye hema kubwa jeupe lililokuwa na nakshi za bendera za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sasa ina nchi 7 wanachama baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiunga rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita.  

Nchi wanachama ni TanzaniaKenyaUgandaBurundiRwandaSudan Kusini, na sasa DRC.  

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa jumuiya hiyo Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, “Jamhuri ya Kidemokrasi imetimiza vigezo vyote vya kuwa mwanachama wa EAC.” 

Rais Uhuru Kenyatta alisisitiza kuwa wakazi wa Afrika Mashariki wana mengi yanayowaunganisha ikiwemo lugha ya Kiswahili na kwa hivyo kwa kuiunganisha DRC na jumuiya, EAC itakuwa katika nafasi nzuri ya kukukusanya nguvu za pamoja na rasilimali ili kuiimarisha miundo mbinu inayohitajika sana hususan kwenye usafiri unaoziunganisha kanda za mashariki na magharibi. 

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Antoine Tshisekedi alipokea vizuri tukio hilo akilitaja kuwa la kihistoria.  

Kwenye hotuba yake alisisitiza kuwa upo umuhimu wa ushirikiano hasa katika masuala ya biashara, kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi na kudumisha amani, kwani, “kwa kujiunga na jumuiya, Wakongo wanataka si tu kufurahia matunda ya ushirikiano wa biashara bali pia kudumisha kwanza uhusiano uliojikita kwenye amani na usalama kwa wote.” 

Baadhi ya wakuu wan chi zinazoiunda Jumuiya ya Afrika Mashariki walihudhuria tukio hili jijini Nairobi wakishuhudia tukio hili la kijistoria.  

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni aliyekuwa mcheshi kwenye shughuli hiyo alisema, “ujio wa DRC kwenye jumuiya utaleta ufanisi kwa kuwa na soko pana zaidi la bidhaa na kuimarisha usalama wa kikanda. Ni rahisi kuijumuisha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwani tunazungumza lugha moja tofauti na Ulaya ambako hicho ni kikwazo.” 

Naye Paul Kagame, Rais wa Rwanda aliwahimiza wadau kutimiza ahadi kwa vitendo kwa manufaa ya kikanda, akisema, “tumetoa ahadi na hotuba nyingi. Kilichobaki sasa ni kuzifanyia kazi ahadi hizo. Niko nanyi kwa hali zote hadi malengo hayo yatimie.” 

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki, EAC, Dkt. Peter Mathuki anakubaliana na yote yaliyosemwa na viongozi wakuu wan chi wanachama akisema, “Jumuiya sasa imekuwa kubwa na soko limepanuka kadhalika rasilimali. Hii ni fursa nzuri kwa EAC kuimarika na kuwa kitu kimoja.” 

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Peter Mathuki (kulia) akihojiwa na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kando mwa Mjadala Mkuu wa UNGA76
UN News/Assumpta Massoi
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Peter Mathuki (kulia) akihojiwa na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kando mwa Mjadala Mkuu wa UNGA76

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imepewa muda wa miezi mitano kukamilisha hatua za uanachama kabla mkataba rasmi kuanza kufanya kazi.  

Wakati hayo yakijiri, DRC inasema kwa upande wake inapania kuundwa kwa taasisi mpya ya kuratibu madini itakayokuwa na makao makuu ndani ya mipaka yake.  

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ndiyo nchi kubwa zaidi kwenye eneo lililo kusini mwa jangwa la sahara na ya pili barani Afrika. DRC inajiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati ambapo kitisho cha uasi bado kinashuhudiwa kwenye eneo la mashariki. Ifahamike kuwa waasi wa M23 walioko mashariki ya Congo walitiliana saini Na serikali kuu ya DRC mnamo mwaka 2009 kuweka silaha chini lakini bado muafaka unalegalega.  

Jumuiya ya Afrika Mashariki iliasisiwa mwaka 1967, ikasambaratika baada ya miaka kumi na kufufuliwa upya Mwaka 2000.