Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yahitaji dola bilioni 2.6 billion ili kusaidia watu milioni 7.6 Somalia 2023

Baadhi ya familia 280 walikimbilia kambi ya watu waliohama makazi yao huko Daniyle kusini mashariki mwa Somalia.
© UNICEF/Zerihun Sewunet
Baadhi ya familia 280 walikimbilia kambi ya watu waliohama makazi yao huko Daniyle kusini mashariki mwa Somalia.

UN yahitaji dola bilioni 2.6 billion ili kusaidia watu milioni 7.6 Somalia 2023

Msaada wa Kibinadamu

Naibu mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Adam Abdelmoula, leo ametoa ombo maalum la dola bilioni 2.6 kwa ajili ya kuwasaidia mamilioni ya watu katika taifa hilo la Pembe ya Afrikaambako changamoto za mabadiliko ya tabianchi na mgogoro wa muda mrefu vimesababishaSomalia kuwa moja ya janga kubwa Zaidi la kibinadamu duniani.

Mratibu huyo Bwana Abdelmoula  amesema mjini Geneva Uswis alikozindua ombi hilo kwamba “Somalia imeelekea ukingoni mwa janga la njaa katika miezi ya hivi karibuni kutokana na ukame wa kihistoria unaodhihirishwa na misimu mitano duni mfululizo ya mvua. Mgogoro uko mbali sana mahitaji yanabaki kuwa ya juu na ya haraka. Baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi yanaendelea kukabiliwa na hatari ya janga la njaa.”

Mratibu huyo amesema mwezi Machi, mvua za msimu zilianza na mafuriko ya ghafla ya mito kufurika yakatokea na kuua watu 21 na kuwalazimisha wengine zaidi ya 100,000 kuyahama makazi yao

Kutokana na mvua katika nyanda za juu za Ethiopia, mito ya Shabelle na Juba inaweza kufurika na kufurika mashamba pia.

Hata hivyo, mvua nchini Somalia zinatarajiwa kunyesha chini ya kiwango na kuna uwezekano wa mkubwa hazitotosha kuboresha mtazamo wa Wasomali wengi. Mratibu huyo wa kibinadamu amesema."Hivyo ndivyo mabadiliko ya tabianchi hufanya. Yanaunda mizunguko isiyotabirika ya ukame na mafuriko. Somalia, ambayo imefanya kidogo sana kuchangia mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi, inabeba mzigo mkubwa wa athari zake.”

Karibu nusu ya watu Somalia wanahitaji msaada

Kwa mujibu wa tarifa ya mratibu huyo “karibu nusu ya wakazi wa Somalia ambao ni sawa na watu milioni 8.25 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi wa kuokoa maisha. Kati ya hao, takriban watu milioni 3.8 ni wakimbizi wa ndani.”

Imeongeza kuwa watu wengine takriban milioni 5 wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula.

Pia watoto wapatao milioni 1.8 wana utapiamlo, na watu milioni 8 wanakosa maji ya kutosha, vyoo na huduma za usafi.

Pia takwimu zinaonyesha kuwa theluthi mbili ya watu wote katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame hawana huduma muhimu za afya.

Changamoto hizo zinazidishwa na migogoro na ukosefu wa usalama.

“Karibu watu 660,000 wanaishi katika maeneo yanayodhibitiwa na makundi ya watu wenye silaha wasio wa serikali na kwa kiasi kikubwa watu hao wako nje ya ufikiaji wa msaada wa kibinadamu. Mapigano yanayoendelea Laas Caanood yamewakosesha makazi watu 185,000 katika muda wa miezi mitatu iliyopita.”

Hadi kufikia sasa msaada mkubwa wa wafadhili, kuongezeka kwa misaada ya kibinadamu na mvua za msimu ambazo ziko chini ya kiwango cha kawaida vimeepusha baa la njaa kwa sasa.

Hata hivyo bado, vifo vya ziada vya zaidi ya watu 43,000 vilitokea kwa sababu zinazohusiana na ukame mwaka 2022.