Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za pamoja ni muhimu kukabili janga la tabianchi- Somalia

Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78 New York, Marekani
UN /Cia Pak
Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78 New York, Marekani

Hatua za pamoja ni muhimu kukabili janga la tabianchi- Somalia

Tabianchi na mazingira

Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre amesema nchi yake majanga ya ukame na mafuriko ambayo yamekumba taifa lao katika miaka ya karibuni, yamesababisha vifo vya maelfu ya watu huku mamilioni wakisalia wakimbizi wa ndani, hivyo amesihi jamii ya kimataifa iimarishe uwezo wa kujenga mnepo ili kukabili janga la tabianchi.

Katika hotuba yake kwa Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo, Bwana Barre amesema mabadiliko ya tabianchi ni tishio la uwepo wa binadamu, janga ambalo ametanabaisha kuwa halitambui mipaka na hivyo na hatua za nchi moja moja hazitaweza kulikabili.

“Si sawa kabisa kwamba Somalia, nchi ambayo inachangia kidogo sana kwenye utoaji wa hewa chafuzi duniani, inabeba mzigo wa madhara ya tabianchi,” amesema Waziri Mkuu huyo akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78.

Amesem wakati huu ambapo nusu ng’we ya utekelezaji wa maendeleo ya malengo endelevu, SDGs umefika,  ni vema ahadi zilizotolewa kufanikisha zikageuzwa kuwa vitendo kwa kutunga sera thabiti, na ahadi zikatimizwa ili kuhakikisha amani, ustawi na maendeleo kwa wote.

Tumeweza kudhibiti Al-Shabaab

Bwana Barre amesema Somalia imepiga hatua kubwa kuelekea kwenye amani na utulivu na kwamba “serikali yangu imechukua njia ya marekebisho kufikia suluhu ya kisiasa na kusongesha utangamano wa kudumu kwenye jamii yetu.”

Amesema ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja, kampeni ya Somalia dhidi ya ugaidi imekomboa asilimia 45 ya maeneo ambayo awali yalikuwa yanashikiliwa na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab.

Kwa mantiki hiyo amesisitiza wito wa Somalia wa kutaka kuondolewa bila masharti yoyote kwa vikwazo vya silaha vilivyowekwa dhidi ya taifa hilo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 1992.

“Hatua hiyo itawezesha Somalia kukabili kwa ufanisi zaidi ugaidi na kujenga mustakabali bora na wenye ustawi na amani kwa wananchi wetu.”

Mpango wa mpito tunazingatia

Waziri Mkuu huyo wa Somalia amesisitiza azma ya nchi yake ya kutekeleza kwa kina mpango wa mpito wa amani nchini humo na hatimaye kubeba kwa ukamilifu jukumu la usalama baada ya kuondoka kwa vikosi vya ujumbe wa Muungano wa Afrika wa usaidizi kwa Somalia, AMISOM mwishoni mwa mwaka ujao wa 2024.

“Kuondoka kwa AMISOM ni hatua muhimu kuelekea kuthibitisha uhuru wetu,” amesema Bwana Barre.