Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Walinda amani wa UN kutoka India watoa matibabu ya bure Beni kwa wakazi 500

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka India anayehudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa MAtaifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO akimpatia matibabu mkazi mmoja wa eneo la Beni, jimboni Kivu Kaskazini.
Video ya MONUSCO
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka India anayehudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa MAtaifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO akimpatia matibabu mkazi mmoja wa eneo la Beni, jimboni Kivu Kaskazini.

DRC: Walinda amani wa UN kutoka India watoa matibabu ya bure Beni kwa wakazi 500

Afya

Mjini Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC takribani watu 500 wamenufaika na matibabu ya bure yanayotolewa na walinda aman iwa Umoja wa Mataifa kutoka India, wanaohudumu kwenye ujumbe wa umoja huo wa kulinda amani nchini humo MONUSCO. 

Miongoni mwa wanufaika hao ni Samson Muvu, Mkuu wa kitongoji cha Paida hapa mjini Beni, akizungumza kupitia video ya MONUSCO akiwa kwenye kituo cha matibabu kinachoendeshwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka India anaelezea vile ambavyo waliagizwa na mkuu wa kitongoji cha Ruwenzori kwenda kuhamasisha watu kufika hapa kupata matibabu ya bure.

Bwana Muvu anasema, "nikaona na mimi kama kiongozi nije nipate dawa kwa sababu mwili hauko vizuri. »

Mwingine ni Kamate Masika ambaye anasema, "mimi ni mkimbizi kutoka Mbao Oicha, Niko hapa Beni. Tangu ile vita ya kila siku wanachinja watu, mimi nasikia mwili unachoka, na mishipa yote inauma. Sina amani. Wakati Niko hapa mwili unaendelea kuuma ndio jirani yangu akanionesha jinsi ya usaidizi wa dawa iko MONUSCO kwani yeye amepata yake. Na ndio niliamua kuja ili nitunzwe.”

Kamate alipata pia msongo wa mawazo na kiwewe kwani alishuhudia jamaa zake pia wakichinjwa.

Anne- Marie Kave anasema ni mara ya pili amefika hapa. Awali alikwenda kwingineko na kulipa jumla ya dola 180. Anasema jambo jema ni kwamba “nilipofika hapa dawa ya bure ya askari. Naamini nitalima. Nitafanya kazi ya shamba. Sikufanya kazi ya shamba kutokana na maumivu ya kiuno.”

Dkt. Kowsalya mlinda amani huyu wa MONUSCO kutoka India ni mshauri mtabibu na anasema “watu wanakuja hapa na magonjwa ya kawaida kama vile Mafua, Malaria, homa ya matumbo, maumivu ya mgongo, kichwa, kisukari na moyo. Tunawapatia matibabu na wanaridhika pian a matibabu.”