Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimefurahi sana kupiga kura yangu leo- mwananchi DRC

Raia nchini DRC wakisubiri kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2023 nchini humo.
UN News
Raia nchini DRC wakisubiri kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2023 nchini humo.

Nimefurahi sana kupiga kura yangu leo- mwananchi DRC

Haki za binadamu

Wapiga kura waliojitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa rais, magavana, wabunge na madiwani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hii leo wamelezea waliyopitia ikiwemo jinsi gani video yenye maelekezo ya upigaji kura kutoka Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo, CENI imewarahisisha upigaji huo. 

Assumpta Massoi anaelezea kwenye taarifa hii itokanayo na video kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO.

Beni, Jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Wapiga kura wakiwa kituo cha kupiga kura tayari kutimiza haki yao ya kikatiba.

Mtendaji katika kituo hiki akawapatia maelekezo ya kupiga kura na pia kuwahakikishia kuwa kasha la kutumbukiza kura liko tupu.

Upigaji kura ukaanza kwa wapiga kura kuhakikisha jina liko kwenye orodha ya mpiga kura, kisha anapatiwa nyaraka ya kupigia kura yake, anapiga kura na kisha kutumbukiza kwenye kasha la kura na kuwekewa alama ya wino kwenye kidogo.

Na miongoni mwa wapiga kura ni Mina Kasoki Muhole ambaye amesema, "tulipokelewa vizuri. Niliamka saa 11 alfajiri na kufika hapa mapema kama sa moja kasorobo. Upigaji kura ulichelewa kuanza kwani vifaa vilichelewa. Vilipofika waliweka haraka na upigaji kura ukaanza na nimepiga kura bila tatizo.”

Joel Asimwe naye mpiga kura hapa Beni anasema, “kama ujuavyo, hapa Beni uchaguzi uliopita hatukupiga kura kwa sababu unazofahamu. Hivyo nilisema lazima uchaguzi huu niende nikapige kura. Nilijitahidi mimi na mke wangu tukaamka mapema saa 10 alfajiri na kujiandaa. Tulikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kupiga kura. Ninafurahi  sana kwa sababu mchakato ulikuwa rahisi kwa sababu niliitazama video kwenye WhatsApp. Lakini haikuwa rahisi kwa wazee kupata maelekezo hayo”

Kwa mujibu wa Bwana Asimwe changamoto nyingine ilikuwa ni kuanza kwa kuchelewa na hakuna mtu aliwaeleza sababu ya kuchelewa huko.

Halikadhalika amesema “kulikuwa na mkanganyiko wa wapi twende. Kwa hiyo kuna wakati wanakueleza unapaswa kwenda pale, na siku nyingine wanakueleza uende upande mwingine. Kwa hiyo inahitaji uvumilivu. Lakini kwa ujumla nimefurahi sana na ninategemea kura yangu.”

Matokeo ya uchaguzi  kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi iliyotolewa na CENI, yatatangazwa tarehe 31 mwezi huu wa Desemba na kisha rais mteule ataapishwa tarehe 24 Januari 2024.

Mshindi ni  yule ambaye atapata kura nyingi, ikimaanisha kuwa hakutakuweko na awamu ya pili ya uchaguzi.