Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO inafanya nini kufanikisha uchaguzi mkuu DRC?

Bw. Jean Tobie Okala, Msemaji wa MONUSCO, ofisi ya Beni-Lubero, DRC.
UN News/George Musubao
Bw. Jean Tobie Okala, Msemaji wa MONUSCO, ofisi ya Beni-Lubero, DRC.

MONUSCO inafanya nini kufanikisha uchaguzi mkuu DRC?

Haki za binadamu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, (MONUSCO) unashiriki katika maandalizi ya uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu ambapo tayari umeshasaidia usafirishaji wa nyaraka za uchaguzi, halikadhalika mafunzo kwa polisi wa kitaifa ili uchaguzi huo uwe huru na ufanyike kwa amani. 

Ikumbukwe kuwa wiki iliyopita, Rais wa DRC Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani alithibitisha kuwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge, magavana na madiwani utafanyika kama ilivyopangwa na Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo, CENI tayari imeshaanza kuchapisha majina ya wagombea. 

Tumesafirisha nyaraka nyeti za CENI 

Akizungumza George Musubao wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa mjini Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC, Msemaji wa MONUSCO mjini Beni-Lubero Bwana Jean Tobie Okala amesema “CENI  inatuambia inabidi zifanyike kwa hali ya usalama na amani. Jambo la kwanza ni kuungwa mkono kwa CENI. Nakujulisha kwamba tangu Januari 2023 MONUSCO imesafirisha maelfu ya tani za shehena nyeti sana za uchaguzi ambazo ni za CENI na ambazo zimewezesha shughuli za kurekodi na kuandikisha wapiga.” 

Bwana Okala amesema walisafirisha vifaa hivyo kutoka Kinshasa hadi Goma, kutoka Goma hadi Beni na maeneo mengine. 

Tunahakikisha pia usalama wa raia 

Kuhusu usalama Bwana Okala amesema “mkubaliane nami kwamba bila usalama ni vigumu kwa wapiga kura kusafiri kwenda kupiga kura. Hili linahusisha mambo kadhaa, la kwanza ni doria za kupambana na usalama ambazo tunazipanga kila siku, "twenty-four seven" kama waingereza wanavyosema, walinzi wa amani wa MONUSCO katika miji ya Beni-Lubero, huenda Eringeti na kwingineko kuwaunga mkono jeshi la serikali FARDC kuwezesha wanawake kwenda mashambani, wakati mwingine hata wanafunzi kwenda shule.” 

Mafunzo kwa polisi wa kitaifa 

Pamoja na kuimarisha usalama, msemaji huyo wa MONUSCO ofisi ya Beni-Lubero amezungumzia pia mafunzo kwa polisi wa kitaifa ili kuimarisha usalama wakati wa uchaguzi mkuu. 

"Jambo lingine katika suala la usalama ni mafunzo kwa maafisa wa polisi 1,730 wa DRC ambapo wamepatiwa mbinu za kudhibiti umati wa watu wenye hasira, kudumisha na kurejesha utulivu wa umma. Hii inafanywa na maafisa wa polisi wa wilaya ya Oicha, takriban kilomita 30 kutoka mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini.,” amesema Bwan Okala. 

Ameeleza kuwa waliopatiwa mafunzo ni maafisa wa polisi na kwamba “kama unavyojua, kuhakikisha uchaguzi ni salama ni jukumu la polisi. Hivyo hatutaki kuwe na mauaji au  machafuko, hatutaki matumizi ya nguvu kupita kiasi . Hii ndiyo sababu polisi wa Umoja wa Mataifa (UNPOL) tangu Ijumaa Septemba 8, 2023 walizindua mafunzo kwa maafisa wa polisi 1,730 wa DRC.” 

Kwa mujibu wa Bwana Okala, mafunzo hayo yatadumu kwa miezi mitatu, kuanzia Septemba hadi Novemba. “Na hawa ndio watu watakaowezesha Wakongomani katika eneo hilo kupiga kura kwa amani" 

 

Taarifa hii imeandaliwa na George Musubao wa UN News kutoka mji wa Beni, jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.