Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukwaji  haki za binadamu DRC waongezeka Februari - Ripoti

Makazi ya Wakimbizi wa ndani, IDP huko Sake, Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© UNICEF/Jospin Benekire
Makazi ya Wakimbizi wa ndani, IDP huko Sake, Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ukiukwaji  haki za binadamu DRC waongezeka Februari - Ripoti

Haki za binadamu

Ofisi ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kuhusu haki za binadamu, (UNJHRO) imeripoti ongezeko la asilimia 2 la vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo kwa mwezi wa Februari mwaka huu ikilinganishwa na mwezi uliotanguliwa wa Januari.

Taarifa iliyochapishwa na Radio Okapi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO inanukuu ripoti hiyo ya kila mwezi ikisema kuwa matukio 378 ya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili yaliripotiwa mwezi Februari nchini kote   yakihusisha watu 1,074 kati yao hao wanaume 722, wanawake 222, watoto 78 na wengine 52 ambao jinsia au umri wao havikutambuliwa.

Makundi yaliyojihami yashika kasi kwenye vitendo katili

Katika ripoti hiyo, UNJHRO inadokeza kuwa, kama ilivyokuwa katika vipindi vilivyotangulia, ni wafuasi wa makundi yaliyojihami ndio wanahusika na idadi kubwa ya vitendo hivyo.

Matukio 244 sawa na asilimia 65 ya matukio yote yalitekelezwa na makundi yaliyojihami, huku matukio mengine yakitekelezwa na wanajeshi wa jeshi la serikali.

Kwenye majimbo yenye mapigano na mizozo, ofisi hiyo imenakili matukio 330 katika mwezi Februari, ambapo jimbo la Kivu Kaskazini lina matukio 186 likifuatia na Ituri matukio 85 na kisha Kivu Kusini, matukio 26.

Hata majimbo yasiyo na mapigano kuna ukikwaji wa haki

Kwa upande wa majimbo  yasiyoathiriwa na mapigano, UNJHRO imerekodi matukio 45 yaliyotekelezwa na mawakala wa serikali huko Katanga Juu, Kasai, Kasai Mashariki na mji mkuu Kinshasa.

Tayari matukio yote kuhusu mwelekeo wa ukiukwaji wa haki za binadamu yamewasilishwa kwenye ofisi za serikali kuhakikisha manusura wanapatiwa haki, na watekelezaji wanakumbwa na mkono wa sheria.

Halikadhalika, ofisi hiyo inasema kuwa imesaidia juhudi za serikali za kuimarisha mienendo na tabia za vikosi vya ulinzi na usalama.

Takribani programu 21 za kuelimisha na kuhamasisha watendaji hao kuhusu haki za binadamu wakati wanatekeleza majukumu yao, ziliendeshwa mwezi mzima wa Februari nchini kote DRC.