Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima kusitisha mapigano Gaza kwa maslahi ya kila mtu: Hastings

Watu katika mji wa Rafah katika Ukanda wa Gaza alikimbia shambulio la kombora.
© UNICEF/Eyad El Baba
Watu katika mji wa Rafah katika Ukanda wa Gaza alikimbia shambulio la kombora.

Lazima kusitisha mapigano Gaza kwa maslahi ya kila mtu: Hastings

Amani na Usalama

Usitishwaji wa mapigano huko Gaza ndio "njia pekee ya kusonga mbele na kwa maslahi ya kila mtu kwani vita inayoendelea huko inatishia amani na usalama kwa Wapalestina na Waisraeli kwa miaka au hata miongo ijayo”, amesema afisa mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu katika eneo la Palestina linalokaliwa.

Lynn Hastings amesisitiza kwamba kuongezeka kwa uhasama kumesukuma karibu nusu ya wakazi wa Ukanda huo, au watu wapatao milioni moja, kuingia Rafah kusini, na kuzidisha hali mbaya ya kiafya na njaa.

"Sababu kwa nini Gaza si salama sio tu kutokana na mashambulizi ya anga lakini pia kwa sababu ya hali hizi zinazosababishwa na kundi kubwa la watu kuhama  na kwenda katika maeneo madogo na ya msongamano, ambayo pia inahatarisha operesheni ya kibinadamu katika eneo hilo”, amesema.

Ombi la fursa ya kuwafikia mateka na wafungwa

Bi. Hastings pia amesisitiza kuwa usitishaji mapigano unaweza kusaidia kuachiliwa kwa mateka waliotekwa na Hamas wakati wa mashambulizi yake mabaya ya kigaidi kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, na amesisitiza wito wa kuwafikia mateka mateka hao.

Fursa kwa washirika wa kibinadamu Kamati ya Kimataifa ya chama cha Msalaba Mwekundu (ICRC) inapaswa pia kutolewa kwa wahudumu wa afya ambao wamezuiliwa na vikosi vya Israeli, kama vile mkurugenzi wa hospitali ya Al-Shifa, ambayo ilikuwa mlengwa wa uvamizi wa kijeshi mwezi uliopita. 

Maoni ya Bi Hastings kwa waandishi wa habari mjini Geneva akizunguza kutoka Jerusalem yamefuatia kura nyingi za Jumanne kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa za kuunga mkono "kusitishwa kwa mapigano mara moja kwa minajili ya kibinadamu, kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote na pia kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu".

Wananchi wengi wa Gaza wanakosa chakula

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa magonjwa ya kuambukiza Ukanda wa Gaza yanaenea, ni chini ya theluthi moja ya hospitali zote ndio angalau zinafanya kazi kwa sehemu, makazi yamefurika kupita uwezo wake kwa muda mrefu na idadi kubwa ya watu hawana chakula au maji ya kutosha.

“Takriban nusu ya wakazi wa kaskazini na theluthi moja kusini wanakabiliwa na viwango vikali vya njaa" kulingana na tathmini ya hivi maribuni ya Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP.

Bibi Hastings amesisitiza kuwa Israel kama nchi inayokalia kwa mabavu ina jukumu la kuwalinda raia wa Palestina katika eneo hilo, kutoa mahitaji yao ya kimsingi na kuhakikisha upatikanaji wa misaada bila vikwazo. 

“Hiyo ina maana sio tu kuruhusu malori ya misaada kuvuka na kuingia Gaza lakini pia kuwezesha wahudumu wa kibinadamu kutoa msaada kwa wale wote wanaohitaji”, amesema.

Masoko lazima yafunguliwe

Mratibu huyo wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa sekta ya misaada inahitaji kufanya kazi bega kwa bega na sekta za umma na sekta ya biashara kama tunavyofanya kila mahali duniani ili kusaidia wakazi wa Gaza ipasavyo.

"Tunahitaji masoko kuwa wazi", amesema, na bidhaa za biashara kuingia ili mgogoro wa utapiamlo uweze kuepukwa.

Bi Hastings amekaribisha jana kuchunguzwa kwa malori ya misaada ya Umoja wa Mataifa katika kivuko cha mpaka cha Kerem Shalom kinachodhibitiwa na Israel kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa ongezeko hilo la machafuko. 

Malori 80 yalithibitishwa na kuruhusiwa kabla ya kutumwa Rafah ili kuingia ndani ya eneo hilo, amesema.

Amerejea wito wa kufunguliwa upya na kikamilifu kwa kivuko cha Kerem Shalom kwa ajili ya shughuli za kibinadamu na za kibiashara, ambapo kabla ya tarehe 7 Oktoba ilikuwa sehemu kuu ya kufikia bidhaa katika Ukanda huo, na kusisitiza kwamba kivuko cha Rafah hakikukusudiwa kimuundo kupitisha mamia ya malori ya misaada.

Pia amesisitiza juu ya uadilifu wa operesheni hiyo ya kibinadamu, Bi Hastings amesema kuwa hakuna wasiwasi wowote ambao umeelezwa kwa Umoja wa Mataifa na mamlaka ya Israel kuhusu upotoshaji wowote wa misaada kutoka kwenye malori yake huko Gaza.

Malori yanasafirisha chakula cha msaada hadi kaskazini mwa Gaza wakati wa mapumziko ya hivi majuzi ya kibinadamu.
© WFP/Ali Jadallah
Malori yanasafirisha chakula cha msaada hadi kaskazini mwa Gaza wakati wa mapumziko ya hivi majuzi ya kibinadamu.

Mashambulizi kwenye majengo ya UN

Akizungumzia suala la usalama wa vituo vya Umoja wa Mataifa katika Ukanda huo, Bi. Hastings ametaja uharibifu wa vilipuzi uliofanywa na vikosi vya Israel dhidi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Palestina (UNRWA) katika shule ya Beit Hanoun kaskazini mwa Gaza, na kusisitiza kuwa Umoja wa Mataifa hakujua uhalali wowote wa shambulio hilo.

Pia amesema licha ya hatua za kusitisha mgogoro zinazochukuliwa, ambapo Umoja wa Mataifa hufahamisha mara kwa mara wahusika kwenye mzozo ambapo vituo vyake viko, matukio 130 yameathiri mitambo ya Umoja wa Mataifa ambayo imeharibika tangu Oktoba 7 na 62 kati yake imesababisha hasara. 

UNRWA inakadiria kuwa takriban watu 283 waliokimbia makazi yao wanaotafuta usalama katika makazi yake wameuawa na karibu 1,000 kujeruhiwa.

Uharibifu wa miundombinu

Kulingana na picha za satelaiti, takriban asilimia 60 ya nyumba huko Gaza tayari zimeharibiwa au kusambaratishwa, amesema Bi Hastings.

Akielezea juu ya ripoti ya jeshi la Israel ya uwezekano wa mafuriko kwenye mahandaki ya chini ya ardhi huko Gaza na maji ya bahari Bi Hastings ameonya kwamba ikiwa itatokea itasababisha "uharibifu mkubwa kwa muundo ambao tayari umeathiriwa na maji na usafi wa mazingira katika eneo hilo na  kuhatarisha ukanda huo sana, mfumo dhaifu wa ikolojia na kusababisha hatari ya majengo na barabara kuporomoka.”

Vurugu na umaskini katika Ukingo wa Magharibi

Mratibu huyo wa masuala ya kibinadamu pia ameangazia hali inayozidi kuwa tete katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, ambapo Wapalestina 464 tayari wameuawa mwaka huu, zaidi ya nusu tangu tarehe 7 Oktoba. 

Takriban watu 3,000 wamezuiliwa na haikuwa bayana endapo watafunguliwa mashtaka na kusomewa mashtaka, amesema. 

Vurugu za walowezi pia zimeongezeka, ikiwa na wastani wa matukio matano kwa siku kutoka mawili kwa siku mwaka jana.

Kukiwa na kusitishwa kwa vibali kwa wafanyakazi kwenye Ukingo wa Magharibi nchini Israel na katika makazi ya walowezi, na kuvurugika kwa biashara na Israel, ukosefu wa mapato kwa wakazi wa eneo hilo unatia "wasiwasi mkubwa", amesema.