Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Epukeni majawabu ya kutia moyo bila ufanisi – Guterres kwa washiriki COP28

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari katika Jiji la Expo, ukumbi wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP28, Dubai, Falme za Kiarabu.
UNFCCC/Kiara Worth
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari katika Jiji la Expo, ukumbi wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP28, Dubai, Falme za Kiarabu.

Epukeni majawabu ya kutia moyo bila ufanisi – Guterres kwa washiriki COP28

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 ukifikia ukingoni huko Dubai, Falme za Kiarabu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka washiriki waepuke msemo wa “Funika kombe mwanaharamu apite,” na badala yake waje na majawabu ya kina na ya kijasiri ili lengo la kutozidi kwa nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi liweze kufikiwa. 

Katibu Mkuu Guterres akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko Dubai, Falme za Kiarabu amewakumbusha wasongeshaji wa majadiliano hayo kwenye COP28 kuwa mkutano unakunja jamvi kesho lakini bado kuna mapengo makubwa ya kuzibwa.  

Misimamo ilegezwe bila kupuuza sayansi

"Ni wakati wa kusaka kulegeza misimamo ili kupata majawabu, anasema Guterres, akiongeza kuwa misimamo hiyo ilegezwe bila kupuuza sayansi au kupuuza umuhimu wa kuwa na matamanio makubwa. Anasema katika dunia iliyomeguka na kugawanyika, COP28 inaweza kudhihirisha kuwa ushirikiano wa kimataifa ndio tumaini letu bora la kutatua changamoto za dunia." 

Ndipo hapo Katibu Mkuu akataja maeneo mawili ambayo anasihi pande husika kwenye mkutano huo kuyapatia kipaumbele: Mosi kupunguza utoaji wa hewa chafuzi na pili;kuhakikisha kuna majawabu yanayopatia haki tabianchi. 

Katibu Mkuu anasema uhakiki wa kimataifa au Global Stocktake lazima uwasilishe mpango wa wazi wa kuongeza nishati rejelezi, kuongeza maradufu nishati fanisi, na mpango mmoja wa kushughulikia vyanzo vya janga la tabianchi ambavyo ni uzalishaji na utumiaji wa nishati kisukuku. 

Serikali zisaidie mapya yatokanayo na uondoaji wa hewa ya ukaa

“Mabadiliko hayawezi kufanyika kwa siku moja,” amesema Guterres akifafanua kuwa yatachukua muda mrefu.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, hatua za kuondokana na miradi au ajira zisizotumia hewa ya ukaa zitaanzisha mamilioni ya ajira mpya zenye staha, “lakini serikali zinapaswa kuhakikisha zinapaswa kusaidia; mafunzo na hifadhi ya jamii kwa wale watakaodhurika na mabadiliko hayo.”

Na kwa wakati huo huo, mahitaji ya nchi zinazoendelea ambazo zinategemea kwa kiwango kikubwa nishati kisukuku lazima yashughulikiwe.

Katibu Mkuu amesema kipindi cha mpito ni muhimu kizingatie kanuni ya usawa lakini unaotambua wajibu na uwezo tofauti wa kila nchi, mathalani mazingira ya kila taifa – si kupunguza matamanio lakini kuoanisha matamanio na uwiano.

“Ndio maana nilipendekeza Makubaliano kwa ajili ya Mshikamano na Tabianchi ,” amesema Katibu Mkuu, ambamo kwamo wanaotoa hewa chafuzi kwa kiwango kikubwa wanachukua hatua za ziada kupunguza hewa chafuzi, na nchi tajiri zinasaidia nchi zinazoibuka kiuchumi kufanya hivyo.

Muda na malengo yanaweza kutofautiana

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa ni dhahiri shairi kuwa kutokana na utofauti wa uwezo miongoni mwa nchi, malengo na ratiba ya utekelezaji wa mpito wa matumizi ya nishati kisukuku navyo vinaweza kutofautiana.

Hata hivyo, wote lazima wazingatie lengo la kutozalisha kabisa hewa ya  ukaa ifikapo mwaka 2050 na kudhibiti kiwango cha joto kisizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi.

Miaka miwili ijayo itakuwa muhimu sana

Kwa Katibu Mkuu, huu ni wakati wa matamanio makubwa zaidi kuwa na haki kwenye tabianchi, na COP28 ilianza kwa hatua mbili za kutia moyo ambazo ni Makubaliano ya kuanza kutekeleza Mfuko wa Fidia ya Hasara na Uharibifu, na pia kujazia Mfuko wa Tabianchi au Green Climate Fund.

“Huo ni mwanzo lakini hatua zaidi zinahitajika,” amesema Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu amesema miaka miwili ijayo itakuwa muhimu sana. Mosi, kuanzisha mpango mpya wa ufadhili kwa tabianchi baada ya 2025 kwa kuzingatia kiwango kikubwa cha udharura kwa changamoto ya tabianchi. Pili; kwa serikali kuandaa na kuwasilisha mipango mipya ya kitaifa ya hatua kwa tabianchi au Michango ya Kitaifa, NDCs ambayo inalenga kudhibiti nyuzi joto isizidi 1.5. “Serikali ziondoke Dubai na uelewa dhahiri ya kile kinachotakiwa kati ya sasa na COP30 nchini Brazil.”

Ametamatisha mkutano wake kwa kusema lazima COP28 imalizike kwa kuendeleza azma ya kudhibiti kiwango cha joto kisizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kama ilivyopitishwa na Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya tabianchi mwaka 2015.