Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku  ya 13: Wanaharakati wa tabianchi huko COP28 wapigwa na butwaa kuondolewa kwa neno nishati kisukuku

Mashirika ya kiraia yanadai fidia kwa hasara na uharibifu uliosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
UNFCCC/Kiara Worth
Mashirika ya kiraia yanadai fidia kwa hasara na uharibifu uliosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Siku  ya 13: Wanaharakati wa tabianchi huko COP28 wapigwa na butwaa kuondolewa kwa neno nishati kisukuku

Tabianchi na mazingira

Saa zikizidi kuyoyoma kwenye mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 huko Dubai, Falme za Kiarabu, wanaharakati wa mazingira wamestaajabishwa na kitendo cha rasimu ya kwanza ya majadiliano ya hitimisho la mkutano huo kuengua wito wa kuondokana na mafuta au nishati kisukuku. 

Kitendo hicho kimeripotiwa kusababisha ‘vilio’ miongoni mwa mashirika ya kiraia na nchi zinazoathiriak zaidi na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Nyaraka hiyo yenye kurasa 21 iliandaliwa na Rais wa COP28 ambaye ni Falme za Kiarabu na mwenyeji wa mkutano huo.  

Nyaraka haitaji kokote kuondokana na nishati kisukuku, jambo ambalo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema mapema Jumatatu kuwa ni moja ya misingi mikuu ya mafanikio ya mkutano huo na moja ya mambo ambayo mataifa mengi yameomba yazingatiwe.  

Badala yake, rasimu ya nyaraka hiyo inataka nchi zipunguze ‘matumizi na uzalishaji wa nishati kisukuku kwa njia ya haki, mipango na uwiano.’  

Marekani, nchi za Muungano wa Ulaya na kundi la nchi zinazoendelea za visiwa vidogo waliungana na vikundi vya mashirika ya kiraia kukataa rasimu hiyo kwa kutochukua hatua za kudhibiti ongezeko la joto duniani.  

Hata hivyo hii si rasimu ya mwisho, na mashauriano yanatarajiwa kuendelea siku nzima ya Jumanne, siku iliyokuwa imepangwa kumalizika kwa COP28.  

Yatarajiwa wajumbe kuwa na vuta nikuvute kwenye rasimu mpya inayotarajiwa kwa kuzingatia orodha kubwa ya mambo ambayo nchi zinaweza kufanya kupunguza joto duniani. 


Wanaharakati na wawakilishi wa baadhi ya nchi wanataka lugha thabiti ambayo inaakisi uhalisia wa udharura wa kukabili janga la tabianchi.  

Vifuatavyo ni baadhi ya mikakati (mingi ikiwa ya kihiari) ambayo imejumuishwa kwenye nyaraka ya sasa na kile kilichoachwa.  

Kilichomo:  

  • Kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa dunia kuzalisha nishati safi ifikapo mwaka 2030 [ Marekani na China zimeahidi kushirikiana kufikia lengo hili kufuatia makubaliano yaliyotiwa saini kabla ya COP28 kati ya nchi mbili hizo zinazoongoza kwa utoaji wa hewa chafuzi duniani]; 
  • Kuondokana nayo kwa haraka makaa yam awe na kudhibiti idadi ya leseni mpya ya uzalishaji wake. 
  • Teknolojia zisizotoa kabisa hewa chafuzi au zitoazo kiwango kidogo cha hewa chafuzi, ikiwemo kuondokana na teknolojia kama vile kufyonya hewa ya ukaa, kutumia na kuhifadhi. 
  • Ufadhili kwa tabianchi, lakini itumike lugha isiyo na uthabiti; na   
  • Malengo ya uhimili kukiwa na ahadi zisizotosheleza za kifedha, au ‘bila mpango kazi’ kupima wa kuupima.  

Kilichoenguliwa: 

  • Kuondokana na nishati kisukuku; 
  • Maneno “mafuta” au “gesi asilia” hayamo; 
  • ‘Wajibu thabiti’ kwa nchi tajiri; na 
  • Uwiano kwenye uhimili, unahitajika kwa usaidizi wa uwiano kutoka nchi tajiri. 

 ‘Utakuwa usiku mrefu’ 

Harjeet Singh, Mkuu wa Mkakati wa Kimataifa kwenye Mtandao wa Kimataifa kuhusu Hatua kwa Tabianchi ameimbia Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko Dubai, ya kwamba alikuwa anatarajia nyaraka mpya iwe na “uthabiti zaidi,” lakini lugha kuhusu kuondokana na nishati kisukuku imetolewa kabisa.. Kama mashirika ya kiraia tumeikataa nyaraka hiyo.” 

“Hakutakuweko na mashauriano kwenye nyaraka hii,” amesema Bwana Singh. “Hebu tuone nchi zinasema nini.” 

Bwana Singh amesema kwa kipindi cha wiki mbili mkutano huo huko Falme za Kiarabu umekuwa ukifanyika huku kukiwa na shinikizo dhahiri kutoka nje hususan kwenye sekta ya nishati kisukuku. Tumeona Umoja wa nchi za kuzalisha mafuta, OPEC, wakiwasilisha barua; kwa vipi [nchi zinazozalisha mafuta] zinapinga kuondolewa kwa nishati kisukuku; kwa vipi nchi tajiri zinasalia mashuhuda. 

“Utakuwa usiku mrefu,” amesema Bwana Singh.