Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP27: Nishati kisukuku ni kiama, asema Mshauri Mkuu wa UN kuhusu tabianchi

Wanaharakati vijana wakiandamana huko Sharm el-Sheikh kwenye COP27 wakipinga matumizi ya nishati kisukuku
UNFCCC/Kiara Worth
Wanaharakati vijana wakiandamana huko Sharm el-Sheikh kwenye COP27 wakipinga matumizi ya nishati kisukuku

COP27: Nishati kisukuku ni kiama, asema Mshauri Mkuu wa UN kuhusu tabianchi

Tabianchi na mazingira

Siku ya 6 ya mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC (COP27) imejikita katika harakati za kupunguza hewa ya ukaa duniani na kuona ni kwa vipi nchi zinazoendelea zinaweza kupatiwa ufadhili wa kifedha kutoka nchi Tajiri ambazo zinaongoza kwa kutoa hewa chafuzi.

Utoaji wa hewa chafuzi unapaswa kudhibitiwa ili kiwango cha joto kisizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi. Ili kufikia lengo hilo na mengine yaliyowekwa kupitia mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuepuka janga kubwa zaidi la madhara ya mabadiliko ya tabianchi, dunia inapaswa kuondokana na mafuta kisukuku haraka iwezekanavyo, amesema Selwin Hart, Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Tabianchi.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko Sharm el-Sheikh, Bwana Hart amesema “hakuna mjadala dhidi ya sayansi. Lakini bila shaka, nchi zinazoendelea hasa zile maskini, zitahitaij msaada kuelekea mpito wa kuanza kutumia nishati jadidifu kwa kina siku za usoni.”

Bwana Hart ambaye ni mzaliwa wa Barbados, moja ya nchi za visiwa vidogo na katika mikutano ya nyuma UN kuhusu mabadiliko ya tabianchi amekuwa mshiriki kwenye mazungumzo amesisitiza kuwa kipaumbele kielekezwe kwenye kusaidia kuondoa vikwazo ambavyo nchi zinazoendelea zinakumbana nazo katika kuelekea mpito wa kuanza kutumia nishati jadidifu.

“Mathalani, gharama ya mtaji. Uwekezaji kwenye nishati jadidifu unahitaji mitaji mikubwa. Asilimia 80 ya mtaji lazima iwepo kabla ya kuanza mradi, kwa sababu unapaswa kununua paneli za sola na betri za kuhifadhi nishati Pamoja na gharama za ufungaji mitambo ambayo ni kubwa. Hata hivyo gharama za uendeshaji ni sifuri kwa sababu hupaswi kununua mafuta au dizeli kuendesha kituo cha nishati jadidifu,” amefafanua Bwana Hart.

Nishati ya kisukuku inayochoma hutoa idadi ya vichafuzi vya hewa ambavyo ni hatari kwa mazingira na afya ya umma.
Unsplash/Andreas Felske
Nishati ya kisukuku inayochoma hutoa idadi ya vichafuzi vya hewa ambavyo ni hatari kwa mazingira na afya ya umma.

Ulinganifu wa kipekee

Mtaalamu huyo akatoa mifano ya ulinganifu kuhusu mazingira yasiyo sawia baina ya nchi zinazoendelea pindi linapokuja suala la mpito kuelekea nishati jadidifu.

“Ninaweza kulinganisha Algeria na Denmark. Denmark ina mazingira yasiyo rafiki kwa ajili ya nishati jadidifu ilhali Algeria mazingira yake ni bora kwa nishati jadidifu kwa asilimia 70 zaidi. Lakini Denmark ina paneli za sola mara saba zaidi kuliko Algeria. Sababu hapa ni gharama ya mtaji,” amefafanua akiongeza kuwa ni yale matarajio ya mapato ambayo wanatarajia wale waliotoa mtaji kwa ajili ya biashara.

Hivyo amesema jamii ya kimataifa inahitaji ijitolee kila kitu ili kutatua tatizo hili.

Kwa Bwana Hart, uhamasishaji wa matrilioni ya dola unahitajika ili angalau kuweko na nuru kuelekea mpito wa nishati jadidifu, badala ya kumimina mitaji kwenye miradi ya nishati ya mafuta kisukuku, ambayo anaona kuwa ni hatari Dhahiri inayoweza kusababisha kuwekeza kwenye rasilimali zisizolipa au kuhamishia madeni kwa vizazi vijavyo.

“Nishati kisukuku ni kiama, kama alivyosema Katibu Mkuu,.. tunahitaji kuongeze maendeleo ya nishati jadidifu kufikia asilimia 60 ya uwezo wote wauzalishaji wa nishati katika miaka 8 ijayo, hii ikimaanisha kuwekeza mara tatu uwezo wa sasa katika muongo huu,” ameongeza Bwana Hart.

Na kwa mtaalam huyo, hilo linawezekana kwa sababu dunia imeongeza mara tatu uzalishaji wa nishati jadidifu katika muongo mmoja uliopita, hivyo, tunahitaji kufanya tena muongo huu. Teknolojia ziko, na fedha vivyo hivyo. Ni suala tu la kuelekezwa inapohitajika ambako kuna uchafuzi na ambako idadi ya watu inaongezeka na mahitaji ya nishati halikdhalika.

Ulaji kidogo wa nyama na ulaji zaidi wa vyakula vya mboga za majani unaweza kupunguza hewa chafuzi kwa kuwa kinyesi cha ng'ombe kinatoa hewa ya Methani inayoharibu mazingira
Unsplash/Jo-Anne McArthur
Ulaji kidogo wa nyama na ulaji zaidi wa vyakula vya mboga za majani unaweza kupunguza hewa chafuzi kwa kuwa kinyesi cha ng'ombe kinatoa hewa ya Methani inayoharibu mazingira

Sekta za kuondokana na uzalishaji hewa ya ukaa

Uondoaji hewa ya ukaa kwa lugha ya kiingereza Decarbonization humaanisha kusaka mbinu mbadala za kuishi na kufanya kazi ambazo zinapunguza utoaji wa hewa chafuzi na kunasa hewa ya ukaa na wakati huo huo kuihifadhi kwenye udongo na mioto. Inahitaji mabadiliko au marekebisho ya miundo yetu ya sasa ya kiuchumi na kijamii ambayo inajikita katika ukuaji kwa gharama yoyote ile.

Katika siku ya leo ambayo maudhui kwenye COP27 yalikuwa Kuondoa au kupunguza hewa ya ukaa,  ripoti mpya ya UN inasisitiza umuhimu wa kupunguza kwa kiwango kikubwa hewa chafuzi kutoka nchi zinazozalisha nishati inayotoa hewa chafuzi kwa asilimia 25 ya duniani kote na asilimia 66 kwenye sekta ya viwanda.

Ripoti hiyo imetaja viwanda vya sarufi, chuma na chuma cha pua na vile vya kemikali na kuwa wachafuzi wakuu na kuelezea hatua za kuchukua kupunguza na kuzielekeza kwenye mpito wa kutotoa hewa chafuzi.

Wanapendekeza uchumi ambao utoaji hewa ya ukaa unapunguzwa na hata kama itatolewa basi inadakwa na kutumika au inaondolewa, halikadhalika ubunifu wa kutatua changamoto ya kiwango kikubwa cha joto kwenye viwanda vya kuchakata kemikali, mathalani kuchoma nishati kisukuku.

Mashirika ya kiraia yahamaisha kuondokana na nishati kisukuu

Mabanda ya nchi na mashirika ya kiraia kwenye COP27 yalishiriki kikamilifu na shughuli lukuki ikiwemo kuondokana na nishati kisukuku.

Walionesha michezo na miradi kadhaa ikiwemo ya ni kwa vipi kuelekea mpito wa nishati jadidifu ili kuonesha wageni ni kwa vipi mustakabili utakuwa wakati wa matumizi ya nishati jadidifu iwapo uamuzi utatekelezwa.

Waandamanaji walishiriki wakiwemo madaktari ambao walikuwa wanaonekana kupatia sayari dunia msaada wa kupumua, CPR, kama njia ya kuonesha madhara ya kiafya kutokana na mabadiliko ya tabianchi, huku mashirika ya kidini kutoka Afrika yakiandamana na kuimba, “Hatutaki tena nishati kisukuku, tunatak ahatua sasa.!

Mmoja wa washiriki alisikika akisema, “Ifikapo COP28, pengine Afrika itapeleka miili ya watu Dubai . Pengine hatutaweza kushiriki kwa sababu mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuwa yamefuta bara la Afrika. Hatutoi ombi, tunataka deni la tabianchi nchi kwa Afrika, lilipwe, bara ambalo limechangia kidogo au halijajachangia kabisa kwenye madhara ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema mwanaharakati kutoka Uganda akiwakilisha shirika la kiraia Green faith. 

“Ujumbe wetu ni rahisi: Mafuta kisukuku yabakie ardhini.”

Mashirika ya kidini nayo  hayakuwa nyuma huko COP27 yakitaka mafuta ya kisukuku yasalie ardhini kwani yanachangia hewa ya ukaa
UN News/Laura Quinones
Mashirika ya kidini nayo hayakuwa nyuma huko COP27 yakitaka mafuta ya kisukuku yasalie ardhini kwani yanachangia hewa ya ukaa

Majawabu ya kuondoa hewa ya ukaa- Je wajua kiwango uzalishacho cha hewa ya ukaa?

Wanachama wengine wa mashirika ya kiraia wanasongesha majawabu ya kuanzia kwenye jamii kupanda juu ili kusaidia jamii kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa.

Michelle Li, muasisi wa shirika la Clever Carbon, anasongesha ufahamu kuhusu vyanzo vya kusambaa kwa hewa ya ukaa ili kuchagiza kasi ya kupunguza hewa chafuzi, na kufikia viwango vilivyowekwa vya kuhakikisha hewa inayotolewa inaondolewa haraka, NET ZERO na kuweka teknolojia zinazopimika halikadhalika majawabu.

“Ufahamu kuhusu hewa ya ukaa, kuelewa na kufahamu kiwango cha hewa ya ukaa tunachozalisha katika maamuzi au vitendo vyetu vya kila siku, kuanzia chakula hadi kutembea. Mlo wa mtu asiyekula nyama kwa wastani huzalisha gramu 600 wa hewa chafuzi, ukila kuku gramu 1300 na ukila nyama ya ng’ombe gramu 7,700. Ufahamu wa hewa ya ukaa ni pia ni uelewa kuhusu ujazo wa hewa hiyo angani ambao kwa sasa ni 420ppm (420 Parts Per Million) au kwa lugha rahisi ni mililita 420 za ujazo wa hewa ya ukaa kwa kila lita moja ya hewa angani. Wataalamu wanaonya kuwa iwapo “tukivuka na kufikia 450ppm basi tutavuka lengo la kuhakikisha joto halizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi,” amefafanua Bi. Li akizunguzma na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Kwa Bi. Li, uelewa kuhusu hewa ya ukaa ni mbinu ambayo inaweza kupunguza na kuondoa maelfu ya tani za ukaa kutoka angani.

“Ni jambo rahisi na linaweza kuanza kutumika leo hii. Tunapoangazia viwanda kupunguza hewa ya ukaa, elimu kuhusu utoaji wa hewa ya ukaa kwa mtu binafsi inaweza kuchagiza pia,” amefafanua Bi. Li.

Bango linaloonesha mchakato wa mashauriano kwenye COP27 Sharm el-Sheikh nchini Misri
UNFCCC/Kiara Worth
Bango linaloonesha mchakato wa mashauriano kwenye COP27 Sharm el-Sheikh nchini Misri

Mwelekeo sawa kwenye mashauriano

Balozi Wael Aboulgmagd, Mwakilishi Maalum wa Urais wa Misri kwenye COP27 katika mkutano na waandishi wa Habari ametangaza kuwa kuna maendeleo mazuri kwenye maeneo ya mashauriano.

“Tunaona pande husika zina mwelekeo mzuri kwenye miradi ya kuhimili tabianchi, kupunguza madhara na kulipa fidia ya hasara na uharibifu,” amesema Balozi Aboulgmagd.