Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana kwenye COP28: Sauti na mahitaji yetu lazima yawe mbele kwenye mazungumzo ya tabianchi

Wajumbe Vijana wa Kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi  (IYCD) wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28,  Dubai, Falme za Kiarabu.
COP28/Anthony Fleyhan
Wajumbe Vijana wa Kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi (IYCD) wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, Dubai, Falme za Kiarabu.

Vijana kwenye COP28: Sauti na mahitaji yetu lazima yawe mbele kwenye mazungumzo ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Vijana wanaharakati wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi wanaoshiriki mkutano wa COP28 huko Dubai, Falme za kiarabu hii leo wamesema hawatakaa kimya huku mabadiliko ya tabianchi yakitishia mustakabali wao. Vijana hao wamedai kwamba watunga sera wa serikali watangulize mahitaji ya karibu watoto bilioni 2 duniani kwani sauti na mawazo yao yanaweza kusaidia kuokoa sayari.

 Vijana wameshika hatamu hii leo wakati mazungumzo ya kuzuia ongezeko la joto duniani na mustakabali wa nishati ya kisukuku yakizua gumzo zaidi wakati mkutano huo unaoelekea ukingoni ambao umepangwa kukamilika Jumanne ijayo.

Katika kuelekea mkutano huo, Umoja wa Mataifa ulitoa msururu wa ripoti za kutisha zinazothibitisha kwamba sayari yetu iko katika hatua ya mwisho. Uchunguzi wa hivi karibuni kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa, WMO, ulisema kwamba gesi chafuzi “zimesababisha kasi kubwa ya kuyeyuka kwa barafu na kupanda kwa kina cha bahari.”

Dunia ni nyumbani kwa vijana bilioni 1.8 kati ya umri wa miaka 10 hadi 24 - kizazi kikubwa zaidi cha vijana katika historia. Wanazidi kuongea na kufahamu hatari zinazoletwa na mzozo wa hali ya hewa, na walichukua hatua kuu leo ukumbi wa michezo wa Al-Waha katika Jiji la Maonyesho la Dubai.

 

Harakati za mabadiliko

Katika tukio la mazungumzo ya vijana, Ameila Turk wa mtandao wa kimataifa wa watoto na wanaharakati vijana – YOUNGO, alielezea taarifa ya vijana duniani iliyotolewa kwa wajumbe wa COP28, waraka wa sera ulioandaliwa na maoni ziadi ya 750,000 yaliyotolewa kutoka zaidi ya nchi 150.

Turk amesema “Ingawa hatuna uwezo wa kuleta kila mtu kwenye COP yenyewe, taarifa ya kimataifa ni mfano bora wa jinsi tunavyoweza kuonesha ... kile tunachojali sana, na kuonesha watazamaji pia kwa nini tuko hapa.”

Katika maelezo yake, Dk. Mashkur Isa wa YOUNGO aliwataka waliohudhuria walio na umri wa chini ya miaka 35 kuinua mikono juu na mikono mingi kwenye ukumbi uliojaa ilipanda.

Hata hivyo, alibainisha kuwa inasikitisha kwamba kiwango hicho cha juu cha uwakilishi wa vijana kilikosekana kwa kiasi kikubwa katika kazi ya kila siku ya COP28, pamoja na makongamano ya awali ya Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi.

“Licha ya wito wetu unaoendelea wa kuchukua hatua kabambe za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, watoto wetu na vijana hawapo kwenye mijadala ya tabianchi, ahadi na utungaji sera. Wahusika wa majadiliano haya lazima walinde maslahi yetu kwa kuweka mara moja sauti za watoto na vijana katikati ya ngazi zote za maamuzi ya mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Muonekano wa nje wa jengo la COP28 huko Dubai.
© UNDP in Ukraine.
Muonekano wa nje wa jengo la COP28 huko Dubai.

Uwezeshaji

Mwanachama wa YOUNGO Bhumi Sharma, msimamizi wa mdahalo kuhusu mabadiliko ya tabianchi wa vijana, alisema kuwa kuhakikisha fedha kwa ajili ya Hatua ya Uwezeshaji wa Mabadiliko ya tabianchi (ACE) ni suala muhimu.

ACE, ambayo inaangazia mojawapo ya malengo ya Kifungu cha 6 cha Makubaliano ya Paris inalenga kuwawezesha wanajamii wote kushiriki katika hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia elimu na uhamasishaji wa umma, mafunzo, ushiriki wa umma, ufikiaji wa habari kwa umma, na ushirikiano wa kimataifa.

“Kumekuwa na ukosefu wa fedha kwa muda mrefu na licha ya juhudi, nchi zilizoendelea haziko tayari kulizungumzia,” alisema.

Akiongea na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, alisisitiza kwamba uharakati wa kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unatoka ndani, “na wakati hatuwezi kumlazimisha mtu yeyote kujali juu ya kitu ambacho hajali,” matumaini yake ni kwamba watu watachukulia kwa uzito mzozo wa mabadiliko ya tabianchi.