Skip to main content

Haya ndiyo mambo ya kutarajia katika Wiki ya mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi barani Afrika 2023

Sio tu kwamba mikoko inasaidia kuzuia kuendelea kwa mabadiliko ya tabianchi, lakini pia ina jukumu muhimu katika kupunguza athari zake.
The Mangrove Photography Awards/Shyjith Kannur
Sio tu kwamba mikoko inasaidia kuzuia kuendelea kwa mabadiliko ya tabianchi, lakini pia ina jukumu muhimu katika kupunguza athari zake.

Haya ndiyo mambo ya kutarajia katika Wiki ya mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi barani Afrika 2023

Tabianchi na mazingira

Viongozi wa Afrika wanatarajiwa kukutana jijini Nairobi, kenya wiki ijayo kwa jaili ya wiki ya mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi, Mkutano wa kila mwaka ambao wanatarajiwa kujadili njia mbalimbali za kupunguza utoaji wa gesi chafuzi huku wakija na mbinu za mnepo wa kukabiliana na athari za hali ya hewa.

Msichana wa Kiturkana akichota maji kutoka kisima wakati wa kiangazi chini ya mto uliokauka.
Photo: IRIN/A. Morland
Msichana wa Kiturkana akichota maji kutoka kisima wakati wa kiangazi chini ya mto uliokauka.

Mkutano huo unaonaza Jumatatu ya tarehe 04 Septemba 2023 linawaleta pamoja watunga sera, viongozi wafanyabiashara na wanaharakati wa mazingira kutoka kila pembe ya bara la Afrika. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ni miongoni mwa watakao hudhuria mkutano huo na anatarajiwa kuhutubia katika siku ya kwanza ya mkutano huo. 

Wiki ya mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi barani Afrika 2023 umeandaliwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi UNFCCC, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP, shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira duniani, UNEP, na Benki ya Dunia, kwa msaada wa wadau wa kikanda.

Mkutano huu unakuja wakati Bara la Afrika linashuhudia kupanda kwa joto kwa kasi zaidi kuliko maeneo mengine duniani, kusababisha matukio ya mara kwa mara ya hali mbaya ya hewa na ukame wa muda mrefu, na kusababisha uhaba wa chakula na watu kupoteza maisha.

Benaziz, Mama mwenye umri wa miaka 30, amesimama na binti yake, Oumara mwenye umri wa miaka 3 karibu na maji yaliyotuama ambayo bado yamesalia zaidi ya miezi 6 baada ya mafuriko makubwa ya 2022.
© UNICEF/Juan Haro
Benaziz, Mama mwenye umri wa miaka 30, amesimama na binti yake, Oumara mwenye umri wa miaka 3 karibu na maji yaliyotuama ambayo bado yamesalia zaidi ya miezi 6 baada ya mafuriko makubwa ya 2022.

Afrika inateseka zaidi 

Kwa mujibu wa UNEP Afrika kwa ujumla inachangia chini ya asilimia 3 ya jumla ya hewa chafuzi duniani. 

Na katika mkutano huu viongozi wanatarajiwa kuongeza mwito wao wa usaidizi wa kifedha ili kusaidia bara hilo kukabiliana na athari ziletwazo na mabadiliko ya tabianchi.

Wiki ya mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi barani Afrika 2023 ni mojawapo ya wiki nne za mikutano ya mabadiliko ya tabianchi za kikanda zilizofanyika mwaka huu. Mkutano huu umeundwa ili kuongeza kasi kabla ya viongozi hao kushiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28 huko Dubai baadae mwaka huu.

Kwa ratiba kamili ya mkutano, kujisajili, kufahamu wanaoshiriki, kufuatilia yanayojiri, bofya hapa