Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya 4 ya COP28: Ahadi ya 'wakubwa dhidi ya janga la tabianchi' inapungua – Guterres

Uuunguzaji wa mafuta ya kisukuku kunasababisha mabadiliko ya hali ya tabianchi
© Unsplash/Patrick Hendry
Uuunguzaji wa mafuta ya kisukuku kunasababisha mabadiliko ya hali ya tabianchi

Siku ya 4 ya COP28: Ahadi ya 'wakubwa dhidi ya janga la tabianchi' inapungua – Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Jumapili Desemba 03 ametuma ujumbe mzito kwa sekta ya mafuta na gesi akisema ahadi zilizotolewa kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa tabianchi, COP28 anaohudhuria huko Dubai, hazifikii kile kinachohitajika ili kukabiliana na janga la tabianchi.

Ikiwa ni siku ya nne ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi, mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema,  “Hatimaye sekta ya nishati ya kisukuku inaanza kuamka, lakini ahadi zilizotolewa hazifikii kile kinachohitajika.”

Akizungumzia ahadi iliyotangazwa Jumamosi na makampuni kadhaa makubwa ya mafuta na gesi ya kupunguza uvujaji wa methane kutoka kwenye mabomba yao ifikapo mwaka wa 2030, Bwana Guterres amesema ni "hatua katika mwelekeo sahihi", lakini ahadi hiyo haikuweza kushughulikia suala la msingi, ambalo ni kuondoa uzalishaji wa hwa chafuzi kutoka katika matumizi ya mafuta ya kisukuku.

Methane (CH4) ni sehemu kuu ya gesi asilia na inawajibika kwa karibu theluthi moja ya ongezeko la joto la sayari dunia linaloonekana katika nyakati hizi. Ni ya muda mfupi lakini ina nguvu zaidi kuliko kaboni dioksidi, hewa chafuzi inayohusika zaidi na mabadiliko ya tabianchi. Bila hatua kali, uzalishaji wa methane wa anthropogenic duniani unakadiriwa kuongezeka kwa hadi asilimia 13 kati ya sasa na 2030.