Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujio wa ‘Jopo la kuhama kutoka mafuta ya kisukuku’ watangazwa kwenye COP28

Mwanamke kijana nchini Côte d'Ivoire akiwa ameinua paneli ya sola ikiwa ni sehemu ya masomo yake ya nishati mbadala.
© UNICEF/Frank Dejongh
Mwanamke kijana nchini Côte d'Ivoire akiwa ameinua paneli ya sola ikiwa ni sehemu ya masomo yake ya nishati mbadala.

Ujio wa ‘Jopo la kuhama kutoka mafuta ya kisukuku’ watangazwa kwenye COP28

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Jumamosi ametangaza mpango wake wa kuunda jopo linalolenga kuhakikisha hatua za kuondoka katika matumizi ya nishati ya mafuta ya kisukuku kuelekea nishati mbadala zinakuwa za haki, endelevu na kunufaisha nchi zote.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amelitoa tangazo hili katika hotuba yake kwenye mkutano wa viongozi wa nchi zinazoendelea unaofanyika katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi, COP28, unaoendelea Dubai, Falme za Kiarabu.

Bwana Guterres, ambaye amekuwa mtetezi mkubwa wa kuachana na nishati ya mafuta ya kisukuku, amewaambia viongozi wa Kundi la Nchi 77 zinazoendelea, linalojumuisha China, kuwa upatikanaji na upatikanaji wa madini muhimu ya mpito wa nishati ni muhimu ili kufikia malengo yaliyowekwa na Mkataba wa Paris wa 2015.

‘Endelea kusukuma sindano’ – Rais wa Baraza Kuu

Katika hotuba yake, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Dennis Francis amesifu G77 na China kwa kuongoza mamlaka ya kuhamia nishati mbadala na kuongoza wito wa kujenga uwezo wa kustahimili tabianchi.

"Wameongoza mijadala kuhusu ufadhili - ikiwa ni pamoja na kushinikiza mageuzi ya usanifu wa fedha wa kimataifa, ambayo yatawezesha nchi zinazoendelea kupata ufadhili wa maendeleo bila kuongezeka kwa viwango vya madeni visivyokuwa endelevu," ameongeza.

Rais wa Baraza Kuu amebainisha nia yake ya kuitisha ‘Wiki ya Uendelevu’ mnamo Aprili 2024, ili kushughulikia mienendo ya uendelevu kuhusiana na miundombinu, uchukuzi, utalii, na, bila shaka, nishati.

"Lazima tuendelee kusukuma sindano kwenye sekta hizi ambazo ni muhimu sana kwa uchumi wa kisasa, ambazo bado zinachangia zaidi katika uzalishaji wa hewa chafuzi," amesema Balozi Francis akiwaalika viongozi wa nchi zinazoendelea kuja New York kwa 'wiki' hiyo kuendeleza harakati kuanzia katika matokeo ya za uamuzi uliyochukuliwa katika COP28.