Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya dozi 330,000 za chanjo dhidi ya Malaria (RTS,S) zawasili Cameroon- WHO/UNICEF/GAVI

Shehena ya chanjo dhidi ya Malaria, ambayo imependekezwa na WHO (RTS,S) imewasili nchini Cameroon.
© UNICEF/StoryMaxima
© UNICEF/StoryMaxima
Shehena ya chanjo dhidi ya Malaria, ambayo imependekezwa na WHO (RTS,S) imewasili nchini Cameroon.

Zaidi ya dozi 330,000 za chanjo dhidi ya Malaria (RTS,S) zawasili Cameroon- WHO/UNICEF/GAVI

Afya

  • Burkina Faso, Liberia, Niger, na Sierra Leone katika wiki zijazo.
  • Bara la Afrika labeba 95% ya mzigo wa Malaria duniani kote
  • Nchi kujumuisha chanjo katika programu muhimu za chanjo

Hatimaye shehena za kwanza kabisa za chanjo dhidi ya Malaria RTS,S, iliyopendekezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, zimeanza kusambazwa Afrika ambapo shehena yenye dozi 331,200 imewaili Yaoundé, mji mkuu wa Cameroon Jumanne usiku.

Taarifa ya mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Afya, WHO, la kuhudumia watoto, UNICEF na Ubia wa Chanjo duniani, (GAVI) iliyotolewa leo katika miji ya Geneva, USwisi, New York, Marekani na Copenhagen, Denmark inasema shehena hiyo ya kwanza imewasili Cameroon ambayo hapo awali haikushiriki katika mpango wa majaribio wa chanjo dhidi ya malaria na unaashiria kuwa  utoaji wa chanjo dhidi ya malaria katika maeneo hatarishi zaidi katika bara la Afrika utaanza hivi karibuni.

Dozi nyingine milioni 1.7 zinatarajiwa kuwasili katika wiki zijazo huko Burkina Faso, Liberia, Niger na Sierra Leone huku nchi nyingine za Afrika zikitaraji kupokea dozi za chanjo dhidi ya Malaria miezi ijayo,

Chanjo kujumuishwa kwenye programu za utoaji chanjo muhimu

Hii ikimaanisha kwamba nchi kadhaa za Afrika ziko kwenye hatua za mwisho za maandalizi ya kujumuisha chanjo ya Malaria kwenye program za kawaida ambapo mipango inaonesha dozi za kwanza chini ya utaratibu huo zitaanza robo ya kwanza ya mwaka 2024.

Maandalizi ya kina yanahitajika ili kuanzisha chanjo yoyote mpya katika programu muhimu za chanjo, kama vile kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya, kuwekeza katika miundombinu, uwezo wa kiufundi, kuhifadhi chanjo, ushirikishwaji wa jamii na mahitaji, na kupanga na kuunganisha utolewaji sambamba na utoaji wa chanjo nyingine na afua za afya.

Mhudumu wa afya akiwa ameshika sindano ya chanjo ya malaria nchini Ghana wakati wa kampeni ya chanjo kwa wingi. (Maktaba)
WHO
Mhudumu wa afya akiwa ameshika sindano ya chanjo ya malaria nchini Ghana wakati wa kampeni ya chanjo kwa wingi. (Maktaba)

Ghana, Kenya na Malawi walishaonesha njia

Tangu mwaka wa 2019, Ghana, Kenya, na Malawi zimekuwa zikitoa chanjo hiyo katika ratiba ya dozi 4 kutoka karibu umri wa miezi 5 katika wilaya zilizochaguliwa kama sehemu ya mpango wa majaribio, unaojulikana kama Mpango wa Utekelezaji wa Chanjo ya Malaria, MVIP.

Takribani kila dakika moja, mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki dunia kutokana na Malaria. Mzigo wa Malaria ndio mkubwa zaidi katika bara la Afrika, ambalo linachukua takriban 95% ya wagonjwa wa malaria duniani.

Kauli ya Mkuu wa WHO

Akizungumzia hatua hii ya karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesu amesema "utoaji wa chanjo ya malaria kwa nchi nyingine kote barani Afrika utatoa ulinzi wa kuokoa maisha kwa mamilioni ya watoto walio katika hatari ya malaria.”

Hata hivyo amesema, “hatupaswi kuishia hapa. Kwa pamoja, lazima tutafute nia na rasilimali za kuleta chanjo ya malaria kwa kiwango kikubwa, ili watoto wengi waweze kuishi maisha marefu na yenye afya njema.”

Soma taarifa nzima hapa kupata kwa kina habari hii.