Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cameroon leo imezindua mpango wa chanjo ya RTS,S dhidi ya malaria: WHO

Mhudumu wa afya akijiandaa kutoa chanjo ya malaria wakati wa huduma ya afya ya jamii nchini Cameroon.
WHO
Mhudumu wa afya akijiandaa kutoa chanjo ya malaria wakati wa huduma ya afya ya jamii nchini Cameroon.

Cameroon leo imezindua mpango wa chanjo ya RTS,S dhidi ya malaria: WHO

Afya

Cameroon leo imezindua mpango mpya wa chanjo ya malaria ya RTS,S kupatikana katika huduma zake za kawaida za chanjo za kitaifa, na kuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo nje ya mpango wa majaribio wa chanjo ya malaria ambao ulifanywa nchini Ghana, Kenya na Malawi kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO.

Uzinduzi huu unakuja huku juhudi zikiongezeka kwa kasi za kuongeza chanjo dhidi ya ugonjwa huo katika maeneo hatarishi barani Afrika, bara ambalo linachukua asilimia 94 ya visa vya malaria duniani kote na asilimia 95 ya vifo vinavyohusishwa na ugonjwa huo.

Dkt. Shalom Ndoula, katibu mkuu wa mpango mpana wa chanjo nchini Cameroon amesema "Chanjo hiyo italenga hasa watoto wote wenye umri wa miezi sita kufikia Desemba 31, mwaka 2023," 

Chanjo hiyo sasa imesambazwa katika vituo vya afya vya umma na vya kibinafsi, katika wilaya 42 za afya kwenye mikoa 10 ya nchi hiyo. 

Uzinduzi huu unafuatia kuwasili kwa dozi 331,200 za chanjo nchini Cameroon mwezi Novemba 2023. Dozi zingine zinatarajiwa kuwasili katika wiki zijazo.

Shehena ya chanjo dhidi ya Malaria, ambayo imependekezwa na WHO (RTS,S) imewasili nchini Cameroon.
© UNICEF/StoryMaxima
Shehena ya chanjo dhidi ya Malaria, ambayo imependekezwa na WHO (RTS,S) imewasili nchini Cameroon.

Nyenzo ya ziada dhidi ya malaria

Kulingana na Dkt. Ndoula, chanjo hiyo ni zana ya ziada kwa ajili ya mapambano dhidi ya malaria, ambayo ilichaguliwa na nchi "kwa misingi ya sifa zake za awali, kuhakikisha hakikisho la ubora, ufanisi na usalama wa kuingizwa katika mpango wa chanjo".

Ili kujiandaa na uzinduzi huo, WHO na washirika wengine, ikiwa ni pamoja na Muungano wa chanjo duniani GAVI, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto  UNICEF, Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa na mpango wa Clinton wa upatikanaji wa huduma za afya, wameisaidia mamlaka ya afya ya kitaifa kuimarisha hatua muhimu za kuanzishwa kwa chanjo.

Ili utoaji wa chanjo uwe na ufanisi, ni muhimu kwamba nchi ziweke maandalizi ya kina ikiwa ni pamoja na kupitishwa kwa sera ya kitaifa ya chanjo na miongozo, ujumuishaji wa chanjo mpya katika ratiba ya usambazaji wa chanjo zingine na msaada wa kiafya, utayarishaji wa usambazaji wa chanjo, mipango, mafunzo kwa wafanyakazi wa huduma za afya, uwekezaji katika miundombinu, uwezo wa kiufundi, uhifadhi wa chanjo, ushirikiano wa jamii na kuundwa kwa mahitaji, pamoja na usimamizi wa msaada, ufuatiliaji na tathmini ya mchakato ili kuhakikisha ubora wa usambazaji wa chanjo.

Hatua muhimu

Mbali na Cameroon, Benin, Burkina Faso na Liberia wamepokea chanjo hiyo na wanakamilisha mipango yao ya kuisambaza.

"Kuzinduliwa kwa chanjo ya malaria kunaashiria hatua muhimu katika kuzuia na kupambana na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa na vifo," amesema mwakilishi wa WHO nchini Cameroon, Dkt. Phanuel Habimana.

Ameongeza kuwa "Tumejitolea kusaidia mamlaka za afya za kitaifa ili kuhakikisha usambazaji mzuri wa chanjo ya malaria pamoja na uimarishaji wa hatua nyingine za kukabiliana na ugonjwa wa malaria".

Cameroon ni miongoni mwa nchi 11 zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa malaria duniani. Nchi ilirekodi zaidi ya visa milioni 3 na vifo zaidi ya 3,800 mwaka wa 2021. 

Vita dhidi ya malaria ni mojawapo ya vipaumbele vya mpango wake wa maendeleo ya afya ya kitaifa. 

Juhudi za kudhibiti na kuzuia ugonjwa wa malaria zilizofanywa kwa miaka mingi kwa msaada wa washirika zimepunguza polepole mzigo wa ugonjwa huo nchini Cameroon.

Mvulana mdogo ambaye amepatikana na Malaria anapatiwa huduma za afya mashariki mwa Cameroon. (Maktaba)
© UNICEF/Frank Dejongh
Mvulana mdogo ambaye amepatikana na Malaria anapatiwa huduma za afya mashariki mwa Cameroon. (Maktaba)

Zaidi ya watoto milioni 2 walichanjwa

"Nilichagua kuwachanja mapacha wangu kwa sababu niliona jinsi malaria inavyoweza kuwa na madhara," amesema Hélène, raia wa Cameroon ambaye mapacha wake walikuwa wa kwanza kupokea chanjo hiyo ya malaria, na kuongeza kuwa "Nimejitolea kuhakikisha kwamba watoto wangu wanapata dozi zote nne za chanjo na itachukua hatua nyingine, kama vile kuhakikisha kwamba wanalala ndani ya vyandarua."

Tangu mwaka wa 2019, Ghana, Kenya na Malawi zimekuwa zikitoa chanjo ya RTS,S kwa ratiba ya dozi nne kwa watoto wanaoanza karibu na umri wa miezi 5, katika wilaya zilizochaguliwa chini ya mpango wa majaribio, unaojulikana kama Mpango wa Utekelezaji wa Chanjo ya Malaria (MVIP) .

Zaidi ya watoto milioni 2 wamepatiwa chanjo dhidi ya malaria katika nchi tatu za Afrika chini ya MVIP, na zaidi ya dozi milioni 8 zimetolewa, na hivyo kuchangia kupungua kwa asilimia 13 ya sababu zote za vifo miongoni mwa watoto walio katika umri kupokea chanjo hiyo na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa ugonjwa mbaya wa malaria na watoto kulazwa hospitalini.

Nchi tisa za Afrika zinajiandaa kuzindua chanjo ya malaria mwaka huu. Mbali na Cameroon, nchi za Benin, Burkina Faso na Liberia wamepokea chanjo hiyo na wanakamilisha mipango yao ya kuisambaza.

WHO, GAVI, UNICEF na washirika wengine wanafanya kazi kwa karibu na nchi za Afrika kuwasilisha chanjo ya malaria ili kuhakikisha utoaji na mafanikio yake.

Mzigo wa malaria ni mzito zaidi katika bara la Afrika. Mwaka 2022, visa milioni 249 vya malaria vilirekodiwa duniani kote, na kusababisha vifo 608,000, sawa na asilimia 77 ambavyo viliathiri watoto wa chini ya umri wa miaka 5, haswa barani Afrika.