Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusake mbinu mpya za kubaini, kuzuia na kutibu Malaria- WHO

Mhudumu wa afya nchiini Malawi akitoa damu ya mgonjwa kwa ajili  ya kuchunguza Malaria.
© UNICEF/Arjen van de Merwe
Mhudumu wa afya nchiini Malawi akitoa damu ya mgonjwa kwa ajili ya kuchunguza Malaria.

Tusake mbinu mpya za kubaini, kuzuia na kutibu Malaria- WHO

Afya

 Utafiti zaidi na maendeleo katika vifaa vya kuzuia malaria na tiba ni muhimu ili kutokomeza malaria katika siku zijazo limesema shirika la afya ulimwenguni, WHO leo Ijumaa kupitia ripoti yake iliyozinduliwa Geneva Uswisi.  

WHO imesisitiza umuhimu wa hatua katika kuimarisha huduma za afya kwa wote na kuimarisha ufikishaji wa huduma na ufuatiliaji bora kwa ajili ya mbinu bora za kukabiliana na ugonjwa wa Malaria.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kutokomeza malaria kunaweza kuwa moja ya hatua kubwa katika afya ya umma na iwapo kuna mbinu mpya na mifumo mIpya ya kukabiliana na malaria hilo linawezekana.

Akifafanua zaidi mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva, Dkt. Marcel Tanner, ambaye ni mwenyekiti wa kundi maalum la WHO la ushauri kuhusu kutokomeza malaria , amesema “Ili kufikia dunia isiyo na malaria ni lazima kuimarisha ari na kutafuta mbinu mpya na vifaa ambavyo vitazingatia hali mashinani. Mfumo wa sasa uliozoleleka unapunguza kasi ya hatua lakini pia inaturudisha nyuma.”

FAIDA YA KUZUIA MALARIA NI KUBWA

WHO imesema faida kutokana na kutokomeza malaria ni nyingi na zitakuwa na manufaa kwa jamii zilizo hatarini zaidi ikiwemo watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 ambao wanajumuisha asilimia 61 ya vifo vya malaria. 

Aidha zaidi ya asilimia 90 ya vifo Laki Nne kutokana na malaria kila mwaka hutokea kwenye nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara.

Ripoti imesema juhudi mpya za kudhibiti Malaria zitazuia visa Bilioni 2 na vifo Milioni 4  vya malaria kufikia mwaka 2030 iwapo harakati hizo zitafikia asilimia 90 ya watu katika nchi 29 zinazobeba asilimia 95 wa mzigo wa malaria duniani.

Gharama ya kuimarisha juhudi za kuzuia malaria ni dola Bilioni 34 huku faida za kiuchumi kutokana na harakati hizo ni dola Bilioni 283 za kipato cha ndani hii ikiwa ni faida ya urari wa 8 kwa 1 .

Mtoto mwenye umri wa miaka miwili akiwa na mama yake baada ya kupewa dawa ya kutibu malaria katika zahanati ya kijiji katika wilaya ya Kasungu Malawi.
© UNICEF/UN066838/Hubbard
Mtoto mwenye umri wa miaka miwili akiwa na mama yake baada ya kupewa dawa ya kutibu malaria katika zahanati ya kijiji katika wilaya ya Kasungu Malawi.

CHANGAMOTO ZA KUKABILI MALARIA

Baadhi ya changamoto zinazokabili utokomezaji wa malaria ni upatikanaji wa afya kwa wote huku mwanamke mmoja mjamzito kati ya watano anayeishi katika maeneo ya maambukizi  ya juu Afrika an auwezo wa kupata dawa za kujikinga dhidi ya malaria. 

Aidha nusu ya idadi ya watu walio hatarini kuambukiza malaria wanalala chini ya vyandarua vilivyotibiwa na asilimia tatu wanajikinga kupitia dawa za kuua mbu.

WHO imesema hii ni ishara ya umuhimu wa kuimarisha afya kwa wote na huduma za kiafya na uwasilishaji ili kila mtu afikie mbinu za kuzuia, kugundua na kutibu wakati na mahali anakohitaji bila kuteseka kifedha.

MBINU ZA SASA ZA KUKABILI MALARIA ZIMEPITWA NA WAKATI

 WHO imesema kuna haja ya kuwa ni mbinu mpya kwani vifaa vinavyotumika kutibu malaria sasa hivi vilitengenezwa karne moja iliyopita au hata mapema zaidi kwa 

mfano vyandarua ilizotibiwa vyenye viuatilifu, upulizaji dawa ndani ya nyumba, mifumo ya kugundua ugonjwa na dawa za kiungo cha artemisinin.

Kwa mantiki hiyo, ripoti imesema mbinu mpya za kutafiti, dawa na dawa za kuua mbu zinatengenezwa pamoja na chanjo .

Chanjo ya kwanza kabisa dhidi ya malaria ikijulikana kama RTS, S/AS01 imepelekwa Ghana na Malawi na imepangwa kutolewa Kenya.