Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 160 wanakufa kila siku Gaza na janga la magonjwa kuongeza zahma: UN

Watoto wachanga wakitibiwa katika hospitali ya Al-Shifa kaskazini mwa Gaza kabla ya kuhamishwa.
© UNICEF/Eyad El Baba
Watoto wachanga wakitibiwa katika hospitali ya Al-Shifa kaskazini mwa Gaza kabla ya kuhamishwa.

Watoto 160 wanakufa kila siku Gaza na janga la magonjwa kuongeza zahma: UN

Afya

Wahudumu wa misaada ya kibinadamu leo wameonya kwamba janga kubwa ambalo linaweza kuizuilika la vifo vya watoto linatarajiwa Gaza ambako kwa sasa watoto 160 wanakufa kila siku baada ya wiki sita za mashambulizi ya anga ya vikosi vya Israel kujibu mashambulizi ya Hamasi ya Oktoba 7 Kusini mwa Israel ambayo yalikatili maisha ya watu 1200 na takriban watu 240 kutekwa nyara.

Kwa mujibu wa msemaji wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO Christian Lindmeier akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo “Takriban watoto 160 wanauawa kila siku hiyo ni sawa na mtoto 1 kila baada ya dakika 10.”

Kauli hiyo inaunga mkono hofu ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kuhusu tishio kubwa la mlipuko wa magonjwa kwenye Ukanda wa Gaza ambalo athari zake zitakuwa ni vifo zaidi kwa watoto.

James Elder msemaji wa UNICEF amesema “Endapo watoto wataendelea kupata changamoto ya maji na usafi Gaza , tutashuhudia janga kubwa la vifo vya watoto ambalo lingeweza kuzuilika.”

Lindmeier ameeleza kwamba “ Kila dakika 10 watoto wawili wanajeruhiwa . Wakati watoto hao na familia zao wako katikakati ya mzozo , wamekuwa wakipoteza maisha katika mazingira ya kutisha.”

WHO inasema karibu watoto 180 wanazaliwa kila siku katika Ukanda wa Gaza na zaidi ya watoto 20 mioingoni mwao wanahitaji huduma maalum ya afya kama walivyo watoto wachanga katika hospital ya Al-Shifa ambako watoto wachanga njiti 31 na wale waliozaliwa na uzito mdogo waliokuwa katika chumba cha wagonjwa mahtuti wamehamishwa mwishoni mwa wiki.

Ameongeza kuwa “Jumla ya watoto hao ilikuwa 33 lakini wawili walifariki dunia kutokana na ukosefu wa huduma waliyokuwa wakiihitaji.”

Akizungumzia hali mbayá ya huduma za afya Gaza ambako chini ya nusu ya hospital zote ndizo zinazofanyakazi kwa huduma chache afisa huyo wa WHO amesema mipango inaendelea kuwahamisha wagonjwa 200 waliosalia  na wahudumu wa afya 50 kutoka hospital ya Al-Shifa hama hatua muhimu ya mwisho.

Watoto wakihahamishwa kutoka hospitali ya Al-Shifa huko Kaskazini mwa Gaza kuelekea eneo la Kusini mwa ukanda huo wa Gaza huko Mashariki ya Kati kutokana na mapigano  yanayoendelea hivi sasa kati ya Israel na wapiganaji wa kipalestina wa Hamas
© UNICEF/Eyad El Baba
Watoto wakihahamishwa kutoka hospitali ya Al-Shifa huko Kaskazini mwa Gaza kuelekea eneo la Kusini mwa ukanda huo wa Gaza huko Mashariki ya Kati kutokana na mapigano yanayoendelea hivi sasa kati ya Israel na wapiganaji wa kipalestina wa Hamas

Kukabiliwa na kifo

“Wakati watu hawa, madaktari, wauguzi, wagonjwa wakiomba kuhamishwa hilo kwa hakila ni chaguo la mwisho kabisa” amesema akiongeza kuwa hali katika eneo hilo limekuwa mbaya zaidi ambapo mbadala unaowakabili wanadhani ni kifo tu.

Hata hivyo msemaji huyo wa WHO ameeleza kwamba uhamishaji wa watu wa namna hiyo si kazi rahisi n ani hatari kubwa , pia unahitaji uratibu wa hali ya juu na vikosi vya ulinzi vya Israel na Hamas iki kuwafikisha katika eneo salama ndani ya Gaza.

Bwana Lindmeier amesema “Timu ya uhamishaji inahitaji muda, inahitaji maandalizi, inahitaji vifaa maalum na inahitaji upenyo salama wa kupita.”

WHO inasema Gaza sasa ni maskani ya maelfu ya watu waliojeruhiwa na wagonjwa mahtuti.

Limeongeza kuwa hivi sasa kuna ongezeko kubwa la magonjwa kama kuhara na magonjwa ya mfumo wa hewa , huku kukiwa na changamoto kubwa ya maji, mafuta, chakula, umeme au vifaa tiba.

Wagonjwa 72,000 wa matatizo ya maambukizi ya mfumo wa hewa wameripotiwa katika makazi ya watu waliotawanywa , pia kukiwa na wagonjwa karibu 49,000 wa kuhara na zaidi ya nusu ya wagonjwa wote hao ni watoto wadogo wa umri wa chini ya miaka 5.

Kwa mujibu wa WHO idadi hiyo ni kubwa sana ukilinganisha na idadi ya mwezi mmoja kabla ya kuzuka kwa mzozo ambapo waskati wa wagonjwa ulikuwa ni 2000 mwaka 2021 na 2022.