Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Wanaoonesha mshikamano na upande wowote wasinyooshewe vidole- Wataalamu Huru wa UN

Mtaalamu Maalum UN Irene Khan ameketi kwenye kiti cha studio huku nembo ya UMOJA WA MATAIFA ikiwa imeonyeshwa kwenye skrini nyuma yake.
United Nations Irene Khan, Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.

Gaza: Wanaoonesha mshikamano na upande wowote wasinyooshewe vidole- Wataalamu Huru wa UN

Haki za binadamu
  • Waandishi wa habari, wanamichezo, wasanii wanyooshewa vidole
  • Chuki dhidi ya wayahudi yaongezeka
  • Kuonesha mshikamano na wapalestina kwahusishwa na ugaidi

Hii leo wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Bindamu wameeleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko duniani la wimbi la mashambulio, visasi, uharamishaji na vikwazo dhidi ya watu ambao wanaeleza hadharani au kwa uwazi mshikamano wao na manusura au waathiriwa wa mzozo unaoendelea kati ya Israel na Palastina. 

Kupitia taarifa yao walioyoitoa hii leo mjini Geneva, Uswisi, wataalamu hao wanne wamesema, “wito wa kukomesha ghasia na mashambulio huko Ukanda wa Gaza au wa sitisho la mapigano kwa misingi ya kiutu, au kukosoa será na vitendo vya serikali ya Israel, katika mazingira mengi kimakosa vimechukuliwa sawa na kuunga mkono ugaidi au chuki dhidi ya wayahudi.” 

Mwanamume aliyevaa fulana ya Shirika la Afya Duniani akipakia masanduku ya misaada nyuma ya gari nchini Misri.
©WHO/Misri Kampeni za kusaka misaada ya kiutu kwa ajili ya wakazi wa Gaza

Uoga kutokana na vitisho na visasi 

Wamesema kitendo hicho kinabinya uhuru wa kujieleza ikiwemo kisanii au kinaunda mazingira ya uoga katika kushiriki kwenye maisha ya kiraia. 

Halikadhalika wamesema katika muktadha mwingine “tumeshuhudia pia ongezeko la kauli za chuki dhidi ya wayahudi, pamoja na ukosefu wa stahmala kwa wale wanounga mkono Israel, au kwa wale wanoonesha huduma kwa machungu ya Israel bada ya tukio la shambulio la tarehe 7 mwezi Oktoba la mashambulizi kutoka wanamgambo wa kipalestina, Hamas. 

“Hii inaacha fursa ndogo kwa watu kutoa maoni,” wamesema wataalamu hao. 

Wanamichezo wasimamishwa kufanya kazi zao 

Wameainisha kuwa wasanii, wanazuoni, waandishi wa Habari, wanaharakati, wanamichezo wanakabiliwa na madhara makubwa na visasi kutoka kwa serikali au sekta binafsi kwa sababu tu ya dhim zao muhimu na kutambulika kwao. 

“Waandishi wa Habari na vyombo vya habari nchini Israel na nchi za magharibi wanaokosoa sera za Isareli na operesheni zao kwenye eneo la Palestina linalokaliwa wamekumbwa na vitisho,” wamefafanua wataalamu hao. 

Baadhi ya wanamichezo Ulaya wamesimamishwa kwa kuchapisha maoni yao kwenye mitandao ya kijamii, huku wengine wakitishiwa kuondolewa kwenye timu zao au mikataba kusitishwa au hata kufukuzwa kwenye nchi husika. 

Mhudumu wa dharura wa MDA aliyevaa fulana ya njano amesimama katika eneo la dharura huko Yerusalemu, huku gari lililoharibika na mkanda wa polisi ukionekana.
© Magen David Adom Israel Wafanyakazi wa dharura nchini Israel wanaitwa kumsaidia mvulana wa miaka 10 ambaye alipigwa na vipande.

Kila mtu ana haki ya kuonesha mshikamano bila kubugudhiwa

Hivyo wamesema watu wana haki ya kuelezea mshikamano wao na manusura au waathirika wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kudai hai; iwe kutoka upande mmoja au pande zote. 

“Ni wakati wa mizozo au vita ambapo tunapaswa kuzingatia haki za binadamu, na kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa bila ubaguzi, na zaidi ya yote sheria iwe msumeno na tuepuke upendeleo,” wametamatisha wataalamu hao. 

Wataalamu hao maalum ni Alexandra Xanthaki, Farida Shaheed, Clément Nyaletsossi Voule, na  Irene Khan

Kwa kina soma taarifa hiyo hapa