Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunahitaji njia kuwafikia wenye uhitaji Gaza: Wahudumu wa kibinadamu

Mashambulizi usiku mjini Gaza
© UNICEF/Eyad El Baba
Mashambulizi usiku mjini Gaza

Tunahitaji njia kuwafikia wenye uhitaji Gaza: Wahudumu wa kibinadamu

Amani na Usalama

Mwezi mmoja tangu shambulio la kigaidi la Hamasi kukatili maisha ya watu 1,400 Israel na kuteka wengine zaidi ya 240 ambao bado inawashikilia na kuendelea kwa mashambulizi ya Israel Gaza ambayo yamesababisha kupoteza maisha ya maelfu ya raia, wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa leo wametoa ombi la kupata njia ya kuwafikia wenye uhitaji mikubwa katika eneo linalokaliwa la Gaza.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO, Christian Lindmeier amesema “Kila siku unafikiri leo hali ni mbayá na kisha kesho yake inakuwa mbayá hata zaidi.”

Amesema hayo akimnukuu mmoja wa wafanyakazi wenzake aliyeko Gaza ambako kunasalia kuzingirwa hadi sasa na amesisitiza kuwa “Fursa ya ufikiaji wenye uhitaji ni lazima.”

Watoto 160 wanakufa kila siku

Kiwango cha vifo na mateso ni "vigumu kuelezeka", amesema bwana Lindmeier akiongeza kuwa kwa wastani, watoto 160 wanauawa kila siku katika eneo hilo na idadi ya vifo imepita watu 10,000, kulingana na takwimu za wizara ya afya huko Gaza.

Wakati huo huo, katika eneo linaloongozwa na Hamas, mashambulizi ya mabomu ya Israel yameongezeka na operesheni za kijeshi za ardhini zinaendelea dhidi ya wapiganaji wanaohusishwa na mashambulizi ya Oktoba 7.

Nchini Israel, watu wanaogopa, wana kiwewe na wana uchungu kwa ajili ya wapendwa wao, amesema msemaji huyo wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Bwana Lindmeier kabla ya kurejea wito kwa Hamas kuwaachilia mateka mara moja.

Ameendelea kusema kuwa wengi wa watu wanaoshikiliwa mateka wanahitaji waliofungwa wanahitaji matibabu ya haraka.

Juhudi za kidiplomasia

Akirejea maombi ya awali ya Umoja wa Mataifa  Bwana. Lindmeier amesisitiza kwamba kinachohitajika sasa ni "utashi wa kisiasa angalau kutoa usitishaji wa uhasama kwa minajili ya kibinadamu na fursa ya kupunguza mateso ya raia pamoja na mateka huko Gaza".

Amesisitiza kuwa juhudi za kidiplomasia kufikia lengo hili zimeendelea. 

Mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa Volker Türk ameanza ziara ya siku tano katika eneo hilo mjini Cairo Misri jana Jumanne ili kuzungumza na maafisa wa Serikali, mashirika ya kiraia, waathiriwa na wafanyakazi wenzake wa Umoja wa Mataifa, akisisitiza kwamba "ukiukwaji wa haki za binadamu ndio chanzo cha ongezeko hili na haki za binadamu zina jukumu kuu katika kutafuta njia ya kujikwamua na kutoka kwenye jinamizi hili lenye maumivu."

Bwana Türk anatarajiwa kuzuru Rafah kwenye mpaka wa Misri na Gaza kabla ya kusafiri hadi mji mkuu wa Jordan Amman.

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA Jens Laerke amethibitisha kwa waandishi wa habari mjini Geneva kwamba Umoja wa Mataifa umealikwa kwenye mkutano wa kimataifa wa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Gaza unaoandaliwa na serikali ya Ufaransa mjini Paris siku ya Alhamisi, na kwamba itatangazwa hivi karibuni bila shaka nani atashiriki kwa niaba ya shirika hilo.

Uharibifu mkubwa unaonekana katika ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 10 Oktoba 2023.
WHO
Uharibifu mkubwa unaonekana katika ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 10 Oktoba 2023.

Hali ya maisha isiyo ya kibinadamu

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA lilisema leo kwamba zaidi ya watu wawili kati ya watatu wa Gaza wamekimbia makazi yao ndani ya mwezi mmoja.

"Hii inakuja na hofu ya mara kwa mara na hali ya maisha isiyo ya kibinadamu kwa karibu watu milioni 1.5", limesema shirika la UNRWA, ikiwa ni pamoja na matatizo ya kila siku ya kupata mkate na maji pamoja na kukatika kwa mawasiliano ya simu mara kwa mara na kukata mawasiliano ya watu na wapendwa wao na pia kutoka duniani kote.

Zaidi ya watu 717,000 wanapata hifadhi katika vituo 149 vya UNRWA kote katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na eneo la kaskazini, ambalo limekatwa na eneo lote la Ukanda huo kutokana na operesheni za kijeshi za Israeli.

Mamia ya malori yanasubiri kuingia Gaza

Bwana Lindmeier alisisitiza kuwa "Hakuna kitu kinachohalalisha hofu inayovumiliwa na raia huko Gaza," akisisitiza haja yao kubwa ya maji, mafuta, chakula na upatikanaji salama wa huduma za afya ili kuishi.

Amerejea wito wa Umoja wa Mataifa wa "kuingia bila vikwazo, na kwa usalama kwa malori 500 ya misaada kwa siku, sio tu kuvuka mpaka lakini pia njia nzima hadi kwa wagonjwa katika hospitali, ambako upasuaji unafanyika ikiwa ni pamoja na kukatwa kwa viungo bila ganzi.”

Mamia ya malori ya mizigo ya misaada yanasubiri kuingia katika mpaka wa Misri na Gaza na wahudumu wa kibinadamu huko Gaza wako katika hali ya kusubiri ili kuwezesha usambazaji wa bidhaa za misaada.

Mashujaa wa kweli

Bwana Lindmeier pia amesema kwamba anajivunia wafanyakazi kwa kudumisha mfumo wa afya Gaza licha ya matatizo yote, ni mashujaa halisi ambao wanafanya kazi chini ya shinikizo kubwa na mara kwa mara bila kupumzika".

Amesema WHO inawaomboleza wahudumu 16 wa afya ambao wameuawa wakiwa kazini, akisisitiza kwamba mashambulizi yoyote dhidi ya huduma za afya yamekatazwa na sheria za kimataifa za kibinadamu.