Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana tena kuhusu mzozo wa Israel na Palestina

Wajumbe wa Baraza la Usalama wakisimama kwa ukimywa kuwakumbuka  walioathirika na mzozo wa Israel na Palestina
UN Photo/Loey Felipe
Wajumbe wa Baraza la Usalama wakisimama kwa ukimywa kuwakumbuka walioathirika na mzozo wa Israel na Palestina

Baraza la Usalama lakutana tena kuhusu mzozo wa Israel na Palestina

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekutana tena kujadili mzozo unaoendelea wa Israel na Palestina huku mazungumzo yakiendelea nyuma ya pazia kuweza kufikia baadhi ya maafikiano kuhusu vita inayoendelea Gaza, ndani ya chombo hicho chenye wajumbe 15. 

Mabalozi wamesikia ushuhuda mkali kutoka kwa mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO ambaye amesema mfumo mzima wa afya wa eneo hilo sasa umesambaratika. 

Israel: Hamas na hatia ya uhalifu wa kivita wa kiwango kikubwa 

Gilad Erdan, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Israeli kwenye Umoja wa Mataifa, amesema Waisraeli walivumilia mauaji wiki tano zilizopita, sawa na mauaji ya Kristallnacht ya Novemba 1938 chini ya Manazi.

Amesema lengo la mkutano huo lilikuwa katika hospitali za Gaza, lakini haukutaja shambulio la moja kwa moja kwenye hospitali ya Israeli siku chache zilizopita, na maroketi ya Hamas.

Amesema wapiganaji wa Hamas wamekuwa wakipiga risasi kwenye magari ya wagonjwa ili kuwazuia kusaidia majeruhi, na kwamba Israel imefichua kuwa Hamas ina makao yake makuu ndani na chini ya hospitali ya Al Shifa, na wanatumia magari ya kubeba wagonjwa kama njia ya kusafirisha silaha.

"Kila sehemu ya Gaza imegeuzwa kuwa mtego wa ugaidi", amesema. "Hakuna kitu kitakatifu kwa magaidi hawa wa Hamas. Ni uhalifu wa vita wakiwango kikubwa. Tunawezaje kufanya mkutano mfupi juu ya hali ya matibabu bila kufanya hili kuwa suala la msingi la mkutano huu?"

Ameendelea kusema kuwa Kwa wiki kadhaa Israel imewapa raia tahadhari zote zinazostahili na njia salama kuondoka katika eneo la vita linalodhibitiwa na Hamas, wakati Hamas inawazuia kufanya hivyo.

Balozi wa Kudumua wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa Gilad Erdan akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Usalama kuhusu mzozo baina ya Israel na Palestina
UN Photo/Evan Schneider
Balozi wa Kudumua wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa Gilad Erdan akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Usalama kuhusu mzozo baina ya Israel na Palestina

Tumefanya kila kinachohitajika

Amesema Israel imekwenda "imefanya kila kitu kupunguza majeruhi ya raia". Kwa Waisraeli maisha ni matakatifu, lakini kwa Hamas ni kifo.

Bwana Erdan amewashambulia maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa kwa kutoakisi ukweli wa hali hiyo mashinani. 

Amedai kuwa "Cha kusikitisha, wanasambaza uwongo ambao umejitenga kabisa na ukweli." 

Amesema tarifa ya WHO inatokana na habari kutoka kwa Hamas, sio wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa wenyewe.

Amedai kuwa mfumo wa Umoja wa Mataifa sasa unawezesha ugaidi kuhusiana na vita ya Gaza.

Balozi Erdan amesema kwa kuikaribisha Iran kuzungumza mjini New York, Umoja wa Mataifa "umepoteza dira yake ya maadili", huku Hamas wakitangaza hadharani kuwa watafanya ukatili zaidi, wakipewa nafasi hiyo.

Amesisitiza kuwa “Njia pekee ya kuzuia marudio yoyote ilikuwa kuondoa uwezo wa kikundi.”

Amehitimisha kwa kusema kuwa “Kujikita na suluhu kwa raia wa Gaza kufuatia uharibifu wa Hamas, kunapaswa kuwa kiini cha mkutano huu, na sio kitu kingine chochote”.

Palestina: Kukomesha mauaji

Riyad Mansour, Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa ,ametoa wito kwa Baraza hilo la Usalama “kukomesha mauaji hayo, na kukomesha sasa”.

Amesema “Azimio la Baraza Kuu lazima litekelezwe, Baraza la Usalama lazima liitikie wito wake. Usiruhusu siku nyingine ipite kujadili ni idadi ya malori mangapi yataingia, yanahitaji kuingia kila siku kwa mamia na maelfu”

Ameongeza kuwa "Sauti ya mashirika ya misaada ya kibinadamu inahitaji kusikika, mayowe ya watu wetu yanahitaji kusikika, na mabomu yanapaswa kunyamazishwa. Sasa na si baadaye.”

Idadi ya vifo inayoongezeka

Amesema hali hiyo ya kushangaza ni lazima ishughulikiwe, huku idadi ya vifo ikiongezeka, akikumbusha kuwa kikao cha kwanza cha Baraza kuhusu suala hilo mwezi uliopita kilitokea wakati mamia ya Wapalestina walikuwa wameuawa na leo idadi hiyo imefikia 11,000, wakiwemo watoto 4,500.

Balozi Riyad Mansour mwangalizi wa kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama kuwenye kikao kuhusu mzozo baina ya Isarel na Palestina
UN Photo/Eskinder Debebe
Balozi Riyad Mansour mwangalizi wa kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama kuwenye kikao kuhusu mzozo baina ya Isarel na Palestina

Mwangalizi huyo amesema "Tunakutana na unaweza kusikia katika kumbi hizi, ukisikiliza vizuri, kelele za watoto wetu chini ya vifusi vilivyoachwa na ubinadamu. Kwani ni malori mia chache tu yameingia Gaza kwa siku 30, na roho zaidi ya mara 10 zimeondoka kwenda mbinguni."

Ameendelea kusema kuwa mateso yale yale ambayo kizazi chake kilikabiliana nayo sasa yanawatesa Wapalestina vijana hivi leo.

“Muuaji hakuwahi kuficha nia yake, alizungumza juu ya kulipiza kisasi na unyama wa binadamu na akatangaza kwamba angeweka mzingiro wa kutisha."

Ametoa wito wa kuachiliwa kwa mateka 200 huku akichukua mateka zaidi ya milioni mbili katika mchakato huo."

Mashambulizi ya mara kwa mara

Israel inaendelea kushambulia kwa mabomu Gaza, Bwana Mansour amesema.

"Wanataka tutoke nje ya nchi yetu, nje ya ardhi yetu. Adui wao wa kimkakati ni uhuru wa serikali yetu, uhuru wa watu wetu. Chaguzi pekee ambazo wamewahi kutupa, kujisalimisha, kuondoka au kufa. Au kwa masharti ya kisheria ya kimataifa, ubaguzi wa rangi, mauaji ya kikabila au mauaji ya kimbari.

Ameongeza kuwa leo, Israel inaruhusu malori ya kutosha kujifanya kuwa hailengi kuzingirwa kwa Gaza lakini haitoshi kuokoa maisha na inatekeleza usitishaji uhasama wa kufikirika wa kibinadamu ambao lengo pekee ni kuwalazimisha watu kukimbia sio kuwapa unafuu ambayo inawahakikishia maisha yao.

“Nilikuwa nakuja hapa kutoa wito wa ulinzi wa kimataifa kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya watu wetu, sasa nakuja kushughulikia maisha ya watu wangu. Nilikuwa nakuja hapa kuzungumzia kuwalinda watu wangu dhidi ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Sasa nakuja kuomba ulinzi dhidi ya mauaji ya halaiki.”

Amesisitiza kuwa “Ikiwa kuna sheria, basi lazima zitumike kwa Israeli pia, na ikiwa kuna haki, basi watu wa Palestina wanayo haki pia, kusiwe na viwango viwili, hakuna ubaguzi na basi iwe hakuna ubaguzi".

Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina: Sekta ya afya inashambuliwa

Marwan Jilani, Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina, ametoa muhtasari wa matukio ya hivi karibuni, akibainisha kuwa amelazimika kuandika upya taarifa yake mara kadhaa kwani hali inabadilika kila dakika.

Watu wanapigwa risasi tunapozungumza, huku 20 wakijeruhiwa kutokana na mashambulizi ya moja kwa moja katika hospitali ya Al Quds katika Jiji la Gaza. Ameonya kwamba Maelfu wako chini ya tishio la kuuawa.

Marwan Jilani mkurugenzi mkuu wa jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina akitoa taarifa kwenye Baraza la Usalama kuhusu hali ya Gaza
United Nations
Marwan Jilani mkurugenzi mkuu wa jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina akitoa taarifa kwenye Baraza la Usalama kuhusu hali ya Gaza

Amesema kulikuwa na raia 14,000 waliokimbia makazi yao huko Al Quds, na jenereta kuu imefungwa kwa sababu ya ukosefu wa mafuta. 

Sasa kuna "hatari kubwa kwamba wagonjwa wote na wagonjwa mahututi na watoto kwenye incubators, wanaweza kufa.”

Amesema magonjwa yameanza kuenea. Pia ameongeza kuwa watu 36 wa familia ya daktari mkuu walikuwa wameuawa. 

Maelezo ya vifo vya watu wengi, hayawezi kutenda haki kwa hofu na kiwewe cha kulala chini ya mashambulizi ya kigaidi, amesema, akitaka mafuta yaruhusiwe haraka kuingia katika Ukanda wa Gaza.

Amesema watu wengi watakufa kwa njaa au kufa kwa magonjwa na kwa kukosa mafuta. 

Ametoa wito kwa Baraza la Usalama  kudai kusitishwa kwa mapigano kwa ufanisi na mara moja, pamoja na kuruhusu msaada wa dharura kwenda kaskazini mwa Gaza.

"Sikilizeni kilio cha watoto waliolowa damu", amesema, ambao wanashangaa kwa nini ulimwengu haujali maisha yao.

Dkt. Tedros Ghebreyesus mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani amesema baada ya kuishi katika vita akiwa mtoto na mzazi, anaelewa vyema mateso na hofu inayopatikana huko Gaza hii leo.

Akitoa maoni ya muda mrefu, amesema chombo hicho hakitumiki kwa madhumuni ambayo kilianzishwa na sio kwa karne ya 21, na kuongeza kuwa "ili kibaki kuaminika, kuwa muhimu na nguvu ya kuleta amani katika ulimwengu wetu, nchi wanachama lazima zichukulie kwa umuhimu suala la kulifanyia mageuzi Baraza la Usalama.”

Msaada wa haraka wahitajika sasa

Mkuu huyo wa WHO amesema njia bora ya kuwaunga mkono ni kuwapa kile wahudumu wa afya wanachohitaji ili kuokoa maisha. 

Takriban tani 63 za msaada huo zimetumwa, lakini fursa ya kuingiza msaada huo isiyo na kikomo inahitajika kuweza kuwafikia raia, ambao hawahusiki na mzozo huo.

Wastani wa mlori 500 kwa siku yalivuka hadi Gaza na vifaa muhimu. Tangu tarehe 21 Oktoba ni malori 650 tu ya misaada ndio yameingia katika eneo hilo, amesema.

WHO inaendelea kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano. Pia ametoa wito kwa Hamas kuwaachilia mateka hao na kuitaka Israel kurejesha usambazaji wa maji, umeme na hasa mafuta. 

Pia amezitaka pande zote mbili kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.

"Ninaelewa kile ambacho watoto wa Gaza lazima wanakipitia kwa sababu nilipokuwa mtoto, nilipitia vivyo hivyo," amesema, akikumbuka sauti za risasi za tracer, milio ya risasi na harufu na taswira ya vita. Najua nini maana ya vita.

Watoto na familia za Israel na Palestina wanataka amani na usalama.”

Hali katika eneo la Gaza ni ya kusikitisha amesema mkuu huyo wa WHO, kuanzia kwenye hospitali zinazofanya operesheni bila ya ganzi hadi ukweli kwamba mtoto huuawa kila baada ya dakika kumi.

"Hakuna mahali popote na hakuna mtu aliye salama," amesema, na kuongeza kuwa wahudumu wa afya wanajitahidi kujaribu kudhibiti mahitaji ya kiafya ya watu milioni 2.3.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akitoa taarifa kwenyenye Baraza la Usalama kuhusu hali Mashariki ya Kati
UN Photo/Eskinder Debebe
Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akitoa taarifa kwenyenye Baraza la Usalama kuhusu hali Mashariki ya Kati

Mfumo wa afya uko taabani

Tangu kuanza kwa mzozo huo, kumekuwa na zaidi ya mashambulizi 250 kwenye vituo vya afya vya Gaza na 25 nchini Israel. 

Zaidi ya wafanyakazi 100 wa Umoja wa Mataifa wameuawa. Nusu ya hospitali za Gaza hazifanyi kazi hata kidogo, na zilizobaki zinafanya kazi zaidi ya uwezo wake.

"Mfumo wa afya ukohoi “amesema.

Tedros ameongeza kuwa anaelewa kikamilifu hasira na huzuni ya watu wa Israel kufuatia mashambulizi ya kinyama ya Hamas. Mauaji ya watu 1,400 hayakubaliki ameongeza, akibainisha kuwa changamoto ya afya ya akili kwa waathirika itaendelea kwa muda mrefu.

Amesema anasikitishwa sana na mateka ambao bado wanashikiliwa na atakutana na familia zaidi wiki ijayo mjini Geneva.

Amesema pia anaelewa hasira, huzuni na woga wa watu wa Gaza, wanaoteseka "kuharibiwa kwa familia zao, nyumba zao, jamii zao na maisha wanayojua."

Israel na Palestina zote zimealikwa kushiriki katika mkutano huo, bila pingamizi.