Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ni tete, mfumo wa afya Gaza umeelemewa

Mama aliyejifungua mtoto mfu akipata matunzo katika hospitali ya Al-Shifa Gaza. (maktaba)
© UNICEF/Loulou d’Aki
Mama aliyejifungua mtoto mfu akipata matunzo katika hospitali ya Al-Shifa Gaza. (maktaba)

Hali ni tete, mfumo wa afya Gaza umeelemewa

Afya

Licha ya mashambulizi dhidi ya vituo vya afya na makazi ya watu katika Ukanda wa Gaza, mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kujitahidi usiku na mchana kuhakikisha watu wanapata huduma ya afya ili kuokoa maisha yao lakini ni wazi kwamba hali inazidi kuwa mbaya kila uchao. 

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO) Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, 

"Hali haielezeki. Shoroba za hospitali zimejaa majeruhi, wagonjwa, wanaofariki dunia; vyumba vya kuhifadhia maiti vimefurika, upasuaji bila ganzi, makumi ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao wakijifadhi hospitalini.”

Hospitali ya Al-Shifa huko Gaza. WHO yaonya kuwa hospitali katika Ukanda wa Gaza ziko katika hali mbaya.
WHO/Occupied Palestinian Territory
Hospitali ya Al-Shifa huko Gaza. WHO yaonya kuwa hospitali katika Ukanda wa Gaza ziko katika hali mbaya.

Inasikitisha kusema kwamba, wiki hii mambo hajabadilika, na pale yalipobadilika, yamekuwa mabaya zaidi. Jana Jumanne, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu katika Eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, Andrea De Domenico, amewaambia waandishi wa habari kwamba, 

"Katika Gaza mapigano karibu na Hospitali ya Al Shifa yaliongezeka mwishoni mwa wiki, na miundombinu muhimu ya hospitali ya Al Shifa iliharibiwa ikiwa ni pamoja na matanki ya maji, vituo vya oksijeni, kituo cha moyo na mishipa katika wodi ya wazazi. Wauguzi watatu pia waliripotiwa kuuawa. Wengi wa watu waliokuwa katika hospitali hiyo wamekimbia au kujaribu kukimbia. Wengine wanabaki nyuma, ni ngumu sana kwetu kujua ni wangapi bado wako kwenye majengo."

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, linasema katika Ukanda wa Gaza, zaidi ya wanawake 150,000 wajawazito na wanaonyonyesha hawawezi kupata huduma muhimu. Na hali inakuwa mbaya zaidi kila saa. Kwa hiyo kuna uwezekano kwamba wakati matangazo haya yanapokufikia tayari wanaokosa huduma wameongezeka.

Mama na mtoto aliyezaliwa hivi karibuni katika hospitali ya Al Shifa katika Ukanda wa Gaza, ambapo kiwango cha vifo vya watoto wachanga kimeongezeka kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 50.
UNICEF/Loulou d’Aki
Mama na mtoto aliyezaliwa hivi karibuni katika hospitali ya Al Shifa katika Ukanda wa Gaza, ambapo kiwango cha vifo vya watoto wachanga kimeongezeka kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 50.

Wisam Al Masri amejifungua mtoto wake wa kike katikati ya mapigano yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza na kwa masikitiko makubwa anasema,

"Nililala katika usiku wa kutisha. Baada ya hapo, nilionesha dalili za uchungu. Nilijifungua kwa upasuaji na nikapata msichana. Nilipozinduka kutoka kwenye upasuaji, waliniambia ni lazima nihame hospitali mara moja. Sasa niko shuleni ambako hakuna bafu, hakuna maji na hakuna huduma inayofaa. Bado sijaangalia au kusafisha sehemu ya kidonda. Siwezi hata kumtunza binti yangu. Bado sijamuogesha, na sijui jinsi ya kumnyonyesha au hata jinsi ya kumkumbatia kawaida. Siwezi kufanya lolote.”

Zaidi ya majeraha ya moja kwa moja kwa watu, nayo hatari ya kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza inaongezeka huku vituo vya afya, maji na mifumo ya vyoo ikiwa imevurugika. Katika makazi ya shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Palestina UNRWA kwenye kambi ya Khan Younis, Gaza, msongamano wa watu ni mkubwa, kwa hivyo hali ni tete. Mwanamke huyu ambaye jina lake halikupatikana anasema, 

"Hakuna bafu sahihi. Hali ni ya kutisha. Hali ya afya ni mbaya sana, janga. Takataka na magonjwa yanawaathiri watoto.”

Itimad Al Madhoun, Afisa wa Afya ya Umma wa WHO, mwenyeji hapa Gaza anasema, “Tunahitaji dawa, tunahitaji chakula, tunahitaji chakula chenye lishe. Tunahitaji vitu vingi. Tunahitaji mahali pasafi, tunahitaji kurudi majumbani mwetu.”