Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wakimbizi 30,000 Rwanda wapewa makazi mapya nchi nyingine:IOM

Wakimbizi kutoka kambi ya Kiziba nchini Rwanda wakijiandaa kupata makazi mapya nchini Norway.
© UNHCR/Lilly Carlisle
Wakimbizi kutoka kambi ya Kiziba nchini Rwanda wakijiandaa kupata makazi mapya nchini Norway.

Zaidi ya wakimbizi 30,000 Rwanda wapewa makazi mapya nchi nyingine:IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema wakimbizi 30,000 kutoka Rwanda wamesaidiwa kwa usalama kupata makazi mapya katia mataifa mengine tangu mwaka 2010.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo iliyotolewa mjini Geneva Uswis na Kigali Rwanda jana Jumatano kuondoka kwa kundi la wakimbizi wengine 13 kuelekea Canada ndio kumefanya idadi ya wakimbizi hao kupindukia 30,000.

Pia shirika hilo limesema safari hiyo ni ishara ya mafanikio makubwa kwa Shirika la IOM na inathibitisha dhamira yake ya kutafuta suluhu ya kudumu kwa wakimbizi na watu wanaohitaji ulinzi wa kimataifa.

Kinachofanywa na IOM wakati wa mchakato

Kwa mujibu wa IOM katika kipindi chote cha mchakato wa kupata makazi mapya, shirika huwezesha mahojiano na nchi walikopewa makazi mapya, tathmini za afya, uchunguzi na rufaa za matibabu, mwelekeo wa kitamaduni kabla ya kuondoka, kusafiri, usafiri salama na mapokezi katika nchi ya mwisho wanapowasili. 

Hii inaruhusu IOM kuhudumia wahamiaji na wakimbizi katika safari yao yote wanapoanzisha upya maisha yao katika makao yao mapya.

Mkuu wa operesheni za IOM nchini Rwanda, Ash Carl amesema "Makazi mapya yanatoa ulinzi wa kimataifa kwa watu walio hatarini zaidi katika ulimwengu wetu, pamoja na fursa kwao kujenga maisha mapya. Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali na washirika wetu nchini Rwanda, pamoja na serikali za nchi wanakoenda, ili kuhakikisha wakimbizi na wahamiaji wana njia salama na zenye heshima kuweza kujumuika katika jamii zao mpya."

Mwanamke akiondoka kwenye kambi ya wakimbizi nchini Rwanda akielekea kwenye makazi mapya nchini Norway.
© UNHCR/Lilly Carlisle
Mwanamke akiondoka kwenye kambi ya wakimbizi nchini Rwanda akielekea kwenye makazi mapya nchini Norway.

Rwanda inaifadhi wakimbizi na waomba hifadhi 135,000

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, kufikia tarehe 30 Septemba 2023  Rwanda sasa inawahifadhi zaidi ya wakimbizi na waomba hifadhi 135,000. 

Wakati suluhu zingine za wakimbizi hazipatikani, makazi mapya inaweza kuwa chaguo pekee linalowezekana kutoa ulinzi bora na kukutana na mahitaji ya wakimbizi ambao haki zao za msingi ziko katika hatari kubwa.

Ili kukidhi hitaji hili kubwa, IOM inaendelea kupanua wigo wake nchini Rwanda. Hadi sasa zaidi ya watu 6,600 wamepokea msaada wa makazi mapya mwaka huu. Miongoni mwa waliopewa makazi mapya, ni watu 1,288 ambao walihamishwa kwa mara ya kwanza kutoka Libya hadi Rwanda, kupitia Mfumo wa Usafiri wa Dharura (ETM).

Suluhu ya kudumu kama vile makazi mapya yanasaidia kuwezesha njia za uhamiaji za mara kwa mara kwa wahamiaji na wakimbizi kulingana na lengo la 10.7 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ambalo ni  "kuwezesha uhamaji na uhamiaji wa watu wenye utaratibu, usalama na uwajibikaji" na lengo la tano la Mkataba wa kimataifa wa usalama, uhamiaji wa taratibu na wa kawaida.