Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chondechonde tuwanusuru wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuvuka Mediterrania:UNHCR 

Boto ilizama pwani ya Libya ikiripotiwa kubeba zaidi ya watu 120 na kati yao ni 47 tu walinusurika kifo.
IOM/Hussein Ben Mosa
Boto ilizama pwani ya Libya ikiripotiwa kubeba zaidi ya watu 120 na kati yao ni 47 tu walinusurika kifo.

Chondechonde tuwanusuru wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuvuka Mediterrania:UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati zahma zikiongezeka Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara na kuwalazimisha mamilioni ya watu kufungasha virago, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limetoa raia ya kuongeza juhudi za kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji hasa wanaobidi kupitia njia hatari kwenye bahari ya Mediterrania kwenda kusaka mustakbali bora.

Kwa mujibu wa UNHCR kila mara maelfu ya wakimbizi na wahamiaji hufanya maamuzi magumu ya kufunga safari za hatari kupitia bahari ya Mediterrania wakitaka kuingia Ulaya kusaka usalama na maisha bora, lakini maelfu hufia njiani kwa kukosa ulinzi, usalama na msaada. Sasa shirika hilo linaomba dola milioni 100 kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwenye nchi za Afrika watokako wakimbizi hao walio njiani kuelekea Mediterrania wakitaka kuingia Ulaya. 

Kipaumbele chao shirika hilo ni kutoa usalama na njia mbadala ya safari hizo ambazo huambatana na ukatili  wa hali ya juu  ikiwemo ubakaji, usafirishaji haramu wa binadamu , kuuawa au kutelekezwa ili wafe.Vincent Cochetel, ni mwakilishi maalum wa UNHCR kwa ajili ya hali kwenye Mediterrania ya Kati. “Fedha, kujikimu kimaisha, fursa za kupata elimu na fursa za mafunzo kwa vitendo , hivi ndio vipaumbele vyetu. Na kisha tushughulikie suala la njia halali  za kusafiri hata wakati huu wa janga la COVID-19. "

Hofu kubwa ya UNHCR ni kuongezeka kwa mizozo na kiwango cha watu kutawanywa Sahel, na Pembe ya Afrika ambapo mwaka jana 2020 pekee kulishuhudiwa vifo 1,064  bahari ya Mediterrania na wengi wakipitia Libya huku watu wengine takriban milioni 2.9 walilazimika kukimbia makwao Sahel, idadi inayotarajiwa kuongezeka endapo suluhu ya mizozo haitopatikana. Mwakilishi wa UNHCR Niger Alessandra Morelli akiwa kwenye kituo cha muda cha mapokezi anasema ,“Tuna wanawake wengi ambao wamejifungua hapa ikiwa ni matokeo ya kubakwa na hao ni idadi kubwa sana, kuna watu ambao wametuonyesha makovu ya kufanyiwa ukatili katika miili yao, hivyo kimsingi tunachokifanya sio tu zoezi la kiufundi bali ni kuwarejeshea utu wao” 

UNHCR inalenga kuimarisha vituo viwili vya mapokezi ya muda Rwanda na Niger kwa ajili ya watu wanaohamishwa kutoka Libya wakisubiri suluhu ya muda mrefu. Pia imetoa wito kwa nchi kutoa fursa ya njia salama kwa wakimbizi na wahamiaji hawa ikiwemo kwa kuwaunganisha na familia zao watokako na wanakoelekea .