Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OHCHR yachapisha ripoti kuhusu shambulio la Hroza Ukraine

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliwasili muda mfupi baada ya shambulizi la anga lililoua raia wengi huko Groza, mashariki mwa Ukraine.
© UNOCHA/Saviano Abreu
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliwasili muda mfupi baada ya shambulizi la anga lililoua raia wengi huko Groza, mashariki mwa Ukraine.

OHCHR yachapisha ripoti kuhusu shambulio la Hroza Ukraine

Haki za binadamu

Tarehe 5 Oktoba, kombora lilipiga mgahawa katika kijiji kidogo cha Hroza Mashariki mwa Ukraine, na kuua watu 59 waliohudhuria mapokezi ya mazishi kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu OHCHR lilikuwa moja ya matukio mabaya zaidi kwa raia tangu Februari 2022.

Leo ofisi hiyo imechapisha  ripoti kuhusu tukio hilo la tarehe 5 Oktoba ambayo inahitimisha kuwa kuna sababu za kuridhisha za kuamini kwamba kombora hilo lilirushwa na vikosi vya jeshi la Urusi, na kwamba hakukuwa na dalili ya wanajeshi au shabaha zingine halali za kijeshi katika eneo hilo au karibu na mgahawa huo wakati wa shambulio hilo.

Ripoti hiyo imetokana na taarifa ziliyokusanywa na kuthibitishwa na mpango wa ufuatiliaji wa haki za binadamu nchini Ukraine HRMMU, ambao ulifanya kazi mbili za kutafuta ukweli huko Hroza tarehe 7 na 10 Oktoba. 

“Mpango huo ulikagua eneo la mlipuko huo, na kuwahoji watu 35, wakiwemo wakaazi wa eneo hilo, mashahidi, manusura wawili, wafanyikazi wa huduma za afya na wafanyikazi wa chumba cha kuhifadhi maiti.” Imeongeza ofisi ya haki za binadamu.

Raia walipoteza maisha katika kijiji kidogo cha Hroza Mashariki mwa Ukraine kufuatia shambulio
© UNOCHA/Saviano Abreu
Raia walipoteza maisha katika kijiji kidogo cha Hroza Mashariki mwa Ukraine kufuatia shambulio

Waliouawa na kuathirika na shambulio hilo

Kwa mujibi wa ripoti hiyo ya OHCHR waliouawa ni wanawake 36, wanaume 22 na mvulana wa umri wa miaka 8 wote walikuwa ni raia waliokuwa wakihudhuria hafla baada ya mazishi ya mwanamke mmoja aliyekuwa askari wa jeshi la Ukraine.

Mlipuko huo wa kombora ulisambaratisha kabisa mgahawa huo na duka lililokuwa karibu.

Ripoti hiyo inaelezea athari mbaya ya shambulio la Hroza, ambapo familia 15 zikiwapoteza wanafamilia wawili au zaidi.

Mwanaume mmoja, ajulikanaye kama Volodymyr, alisema hakuamini mkewe, mwanawe na mkwe wake walikuwa wamekwenda wameuawa akisema "Siwezi kulala, siwezi kula ninazunguka kwa matumaini ya kumuona mke wangu akitokea mahali fulani"

Mkazi mwingine alisimulia jinsi rafiki wa binti yake alivyoweza kutambuliwa tu kwa kujipamba kwenye mikono yake wakati waokoaji walipoubaini mkono wake. Kwa wengine wengi, kitambulisho kilitegemea vipimo vya vinasaba au DNA vya mabaki ya miili yao.

Heshima zimeachwa kwa watu waliofariki kufuatia shambulizi katika kijiji cha Groza.
© Yevhen Nosenko
Heshima zimeachwa kwa watu waliofariki kufuatia shambulizi katika kijiji cha Groza.

Kushindwa kwa jeshi la Urusi kulinda raia

Ripoti hiyo inasema kuwa vikosi vya jeshi la Urusi aidha vilishindwa kufanya kila liwezekanalo ili kuthibitisha kuwa lengo lilikuwa ni la kijeshi, au vilifanya makusudi kuwalenga raia au vitu vya kiraia. 

Kwa mantiki hiyo OHCHR imesema hali yoyote itakuwa inakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.

Ofisi hiyo imelihimiza Shirikisho la Urusi kufanya uchunguzi kamili na wa uwazi ili kuwawajibisha wale waliohusika na kuchukua hatua za kuzuia mashambulizi kama haya kutokea katika siku zijazo. 

Pia imetoa wito kwa Shirikisho la Urusi kutoa fursa ya ufikiaji wa suluhisho madhubuti, likijumuisha malipo ya fidia kwa waathiriwa na familia zako.