Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita isiyo na maana ya Urusi dhidi ya Ukraine inaendelea kusababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu - Türk

Sehemu ya muda ya kizuizini inayotumiwa na jeshi la Urusi katika mkoa wa Kharkiv wa Ukraine.
© OHCHR
Sehemu ya muda ya kizuizini inayotumiwa na jeshi la Urusi katika mkoa wa Kharkiv wa Ukraine.

Vita isiyo na maana ya Urusi dhidi ya Ukraine inaendelea kusababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu - Türk

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk leo (Julai 12) leo mjini Geneva, Uswisi ameeleza namna ambavyo Vita ya Urusi dhidi ya Ukraine inaendelea kusababisha ukikukwaji mkubwa wa haki za binadamu alipokuwa kwenye Majadiliano ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu Ukraine. 

"Ijumaa iliyopita, katika siku ya 500 ya mzozo huu, Ujumbe wetu wa Ufuatiliaji wa Haki za Kibinadamu ulielezea gharama ya kutisha ya kiraia ya vita nchini Ukraine. Zaidi ya raia 9,000, wakiwemo zaidi ya watoto 500, wameuawa tangu vita ilipoanza tarehe 24 Februari mwaka jana. Takwimu halisi zinaweza kuwa za juu zaidi," Türk ameongeza. 

Ripoti hiyo (A/HRC/53/CRP.3) iliyowasilishwa kwa Baraza la Haki za Kibinadamu, inachunguza hali ya raia ambao wamezuiliwa katika mazingira ya vita. Vyanzo vyake ni pamoja na ziara 274 za wafanyakazi wa Ofisi, ikiwa ni pamoja na kutembelea vituo 70 vya kizuizini, na mahojiano na watu 1,136.  

"Katika ripoti iliyo mbele yenu, tumeandika kuzuiliwa kiholela kwa zaidi ya raia 900, wakiwemo watoto wanane, kati ya tarehe 24 Februari 2022 na 23 Mei 2023,” Kamishna Mkuu amesema. 

"Urusi hakiruhusu ufikiaji wa maeneo ya kizuizini, hali ambayo inasababisha kupungua kwa tawimu. Hata hivyo, tuliweza kuwahoji wafungwa 178 waliokuwa wakishikiliwa na Shirikisho la Urusi, baada ya kuachiliwa. Kwa jumla, kesi 864 kati ya ambazo tuliandika zilifanywa na Shirikisho la Urusi. Wengi wao walikuwa kizuizini bila mawasiliano, sawa na kutoweshwa kwa lazima," amesema Türk. 

Ripoti hiyo pia imeandika muhtasari wa kunyongwa kwa raia 77 walipokuwa wakizuiliwa kiholela na Shirikisho la Urusi. Zaidi ya asilimia 90 ya wafungwa wanaoshikiliwa na Shirikisho la Urusi ambao ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu iliweza kuwahoji walisema walikuwa wakiteswa na kutendewa vibaya -- ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kingono, katika visa vingine -- na maafisa wa usalama wa Urusi. 

Raia waliozuiliwa na Shirikisho la Urusi ambao pia walihojiwa ni pamoja na maafisa wa serikali wa eneo hilo, wanaojitolea kusaidia binadamu wengine, wanajeshi wa zamani, wanaochukuliwa kuwa wapinzani wa kisiasa, makasisi na walimu. Katika asilimia 26 ya matukio, walihamishiwa maeneo mengine katika Ukraine iliyokaliwa au Shirikisho la Urusi, bila taarifa iliyotolewa kwa familia zao. Ripoti hiyo pia ilinakili kesi kadhaa ambazo zinaonesha kuwa raia waliowekwa kizuizini wametumiwa na vikosi vya jeshi la Urusi kama "ngao za kibinadamu" ili kuweka maeneo fulani kinga dhidi ya mashambulizi ya kijeshi. 

"Matokeo haya yanashangaza. Yanatoa kwa Shirikisho la Urusi kuchukua hatua madhubuti kufundisha na kuhakikisha wafanyakazi wao wa Urusi wanafuata sheria za kimataifa za haki za binadamu na kibinadamu," Türk amesema.