Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde pande husika sitisheni huhasama, janga kubwa zaidi la kibinadamu laja Gaza: UN

Mashambulizi ya anga dhidi ya Gaza yanaendelea.
© WHO/Ahmed Zakot
Mashambulizi ya anga dhidi ya Gaza yanaendelea.

Chonde chonde pande husika sitisheni huhasama, janga kubwa zaidi la kibinadamu laja Gaza: UN

Msaada wa Kibinadamu

Hali Mashariki ya Kati inazidi kuwa mbayá. Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo amezisihi pande zote katika mzozo kusitisha uhasama , huku mashirika ya misaada yakionya kuhusu janga kubwa zaidi la kibinadamu, wakati hapa Makao Makuu kikao cha 10 cha dharura kuhusu mzozo huo wa Mashariki ya Kati kikiendelea leo. 

 

Hali si hali kwa mujibu wa Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ambaye ameonya leo kwamba adhabu ya pamoja ni uhalifu wa vita akirejea ombi lake la pande zote katika mzozo kusikiliza wito wa amani na kusitisha mapigano hasa wakati huu idadi ya vifo ikongezeka hususan  Gaza na pia kukiwa na ripoti kwamba sasa majina ya watoto yanaandikwa kwenye mikono yako ili iwe rahisi kuwatambua endapo watauawa.

Mashambulizi ya anga yameharibu sehemu kubwa ya kaskazini mwa Gaza.
© UNRWA/Mohammed Hinnawi
Mashambulizi ya anga yameharibu sehemu kubwa ya kaskazini mwa Gaza.

Turk ameitaka Hamas kuwaachilia mara moja mateka bila masharti na kwa Israel kusitisha mara moja adhabu ya pamoja kwa Wapalestina. Pia amesisitiza kwamba kauli za kukashifu Wapalestina zinapaswa kukoma mara moja. 

Kwa mashirika ya kibinadu leo yote yanaonya kwamba mambo yanakuwa mabaya zaidi Gaza. 

Tweet URL

Mratibu wa mwasuala ya kibinada wa Umoja wa Mataifa kwenye eneo linalokaliwa la Palestina Lynn Hastings akizungumza kutoka mjini Jerusalem amesema malori 74 ya msaada yaliyoruhusiwa kuingia Gaza tangu 21 Oktoba na mengine takriban 8 yanayotarajiwa leo hayatoshelezi mahitaji ukizingatia kwamba kabla ya mzozo wa sasa kulikuwa na malozi 450 yaliyokuwa yanaingia kila siku hivyo ameomba msaada zaidi uingine Gaza.

Kwa upande wake Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA Philippe Lazzarini amezungumzia idadi ya wanaokufa na hofu ya kuongezeka idadi hiyo kila siku kutokana na mabomu na makombora na pia kwa athari za kuzingirwa Ukanda wa Gaza. 

Pia ameonya juu ya kukosekana kwa mahitaji ya msingi kama maji, dawa na chakula na amesema idadi ya wafanyakazi wa shirika hilo wanaokufa inaongezeka kufikia leo ni 53.

Na mashirika mengine lile la mpango wa chakula duniani WFP limesema limefanikiwa kufikisha asilimia 2 tu ya chakula kinachohitajika huku la afya la Umoja wa Mataifa WHO likisema lita 94,000 za mafuta zinahitajika kila siku kuweza kuendeleza huduma muhimu katika hospital kubwa 12 Gaza na hapa Makao Makuu Kikao cha 10 dharura cha Baraza kuu kinaendelea na kinatarajiwa kupigia kura mswada wa azimio uliowasilishwa na Jordan kuhusu usitishaji uhasama.