Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Haki za binadamu limesikia ukiukwaji wa haki unaoendelea Ukraine

Raia walipoteza maisha katika kijiji kidogo cha Hroza Mashariki mwa Ukraine kufuatia shambulio
© UNOCHA/Saviano Abreu
Raia walipoteza maisha katika kijiji kidogo cha Hroza Mashariki mwa Ukraine kufuatia shambulio

Baraza la Haki za binadamu limesikia ukiukwaji wa haki unaoendelea Ukraine

Haki za binadamu

Baraza la Haki za binadamu HRC leo limejadili ripoti ya hivi karibuni ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu OHCHR, kuhusu hali ya Ukraine. 

Mwanzoni mwa mkutano huo, Baraza hilo lilikaa kimya kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa shambulio la kigaidi la Hamas dhidi ya Israel.

Kuanzia mateso hadi unyanyasaji wa kijinsia

Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Nada Al-Nashif amesema kwamba mwaka mmoja na nusu baada ya shirikisho la Urusi kufanya shambulio kamili la silaha dhidi ya Ukrainie, ulimwengu unaendelea kupokea takwimu"kuhusu ukiukwaji wa wazi na unaoendelea wa haki za binadamu dhidi ya Ukraine."

Tunazungumza, amesema, kuhusu aina mbalimbali za uhalifu unaoendelea kuanzia mateso mengi na kuwekwa kizuizini kiholela hadi unyanyasaji wa kijinsia katika migogoro.

Twakimu za waliouawa hazijakamilika

Ripoti ya 36 kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Ukraine inaeleza kwamba katika kipindi cha miezi sita tu, kuanzia Februari 1 hadi Julai 31 mwaka 2023, raia 4,621 zaidi waliathiriwa na mzozo huo, huku watu 1,028 wakiuawa na wengine 3,593 kujeruhiwa na baraza hilo likisema idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi.

Pia ripoti hiyo imesema "Katika taarifa za mashahidi, waathiriwa wameelezea ukatili ambao ni mgumu kufikiria, ikiwa ni pamoja na kupigwa shoti za umeme, unyanyasaji wa kijinsia na kingono na vipigo vya kikatili ambavyo katika visa vingine vilisababisha kuvunjika kwa mifupa na kung'olewa meno. Hali kizuizini ni mbaya, ikiwa ni pamoja na uhaba wa chakula na dawa, hali mbaya ya maisha na watu kunyimwa usingizi."

Kesi za makosa ya jinai

Al-Nashif ameripoti kwamba katika eneo linalodhibitiwa na Ukraine, mamlaka ya Ukraine imefungua karibu kesi 6,000 za uhalifu kwa ushirikiano na wanaendelea kutoa idadi kubwa ya hatia katika kesi hizi.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa imeonyesha wasiwasi kwamba "wengi wa wale waliokamatwa na hata kuhukumiwa waliteseka kwa vitendo ambavyo kimsingi, wangeweza kulazimishwa kufanya na mamlaka inayokalia eneo hilo."

Katika eneo la Ukraine linalomilikiwa na Shirikisho la Urusi, ofisi hiyo imesema inazingatia kwa "wasiwasi mkubwa" sera ya utoaji wa uraia wa Kirusi kwa wakazi wa eneo hilo.

Kwa kuongeza, Umoja wa Mataifa bado una wasiwasi mkubwa juu ya ukosefu wa utaratibu wa kurudi kwa watoto wa Kiukraine  ambao walihamishwa kwenye mikoa mingine ya eneo lililochukuliwa na Urusi au ndani ya Shirikisho la Urusi.

Ukumbi wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambamo kwalo wataalamu wa haki za binadamu huchangia hoja kuhusu haki za binadamu
UN Photo/Jean-Marc Ferré
Ukumbi wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambamo kwalo wataalamu wa haki za binadamu huchangia hoja kuhusu haki za binadamu

Sheria mpya ya Urusi inaimarisha hali ya ukwepaji sheria

"Kuwajibishwa kwa ukiukaji na uhalifu ni muhimu ili kuzuia kutokea tena na kuhakikisha haki kwa waathiriwa, amesema Al-Nashif  na kuongeza kuwa Mamlaka ya Urusi haijachukua hatua zozote zinazoonekana kuwafikisha mahakamani wale waliohusika na ukiukaji unaofanywa na vikosi vyake vya usalama. Badala yake, sheria hiyo mpya inatoa msamaha kwa wanajeshi wa Urusi kwa kufanya uhalifu mwingi, ambao umeongeza hali ya ukwepaji sheria.”

Ingawa mamlaka ya Kiukreni imeanzisha uchunguzi wa uhalifu dhidi ya madai dhidi ya vikosi vyao wenyewe, jambo ambalo linakaribishwa, Ofisi bado inasubiri matokeo madhubuti ya uchunguzi huo.

Msimamo wa Ukraine

Ukraine, ikizungumza kama nchi inayohusika, imeishutumu Urusi kwa ukiukaji mkubwa wa haki za Waukraine. 

"Kuzuiliwa kiholela kwa raia, sera ya kutoa uraia wa Urusi kwa wingi, unyanyasaji na mashtaka ya makosa ya jinai, na kulazimishwa kujiunga na jeshi la Urusi bado ni sehemu muhimu ya udhibiti wa Urusi juu ya maeneo yanayokaliwa kwa muda ya Ukraine, pamoja na nchi eneo langu pendwa la Crimea," Amesema Emine Japarova, naibu wa kwanza wa waziri wa mambo ya nje wa Ukraine.

Urusi haikubaliani na hitimisho la waandishi wa ripoti hiyo

Upande wa Urusi umekanusha shutuma zilizoletwa dhidi yake na kutilia shaka uaminifu wa takwimu zilizotolewa katika ripoti hiyo. 

"Hatukubaliani kimsingi na mbinu, maudhui na hitimisho la ripoti ya hivi karibuni ya OHCHR," amesema Yaroslav Eremin, mshauri katika ujumbe wa kudumu wa Shirikisho la Urusi katika Umoja wa Mataifa huko Geneva. 

 “Badala ya kueleza kikamilifu hali duni ya haki za binadamu nchini Ukraine, kwa mujibu wa mamlaka yake, OHCHR inaendelea kuipaka chokaa Kyiv, na kuelekeza lawama kwa uhalifu wa mamlaka ya Ukraine kwa nchi yetu. Mbinu hii haikubaliki kwa Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.” ameongeza

Umoja wa Mataifa unatoa msaada Horza kufuatia shambulio la makombora (Kutoka Maktaba)
© UNOCHA/Saviano Abreu
Umoja wa Mataifa unatoa msaada Horza kufuatia shambulio la makombora (Kutoka Maktaba)

Wakati wa majadiliano, baadhi ya wazungumzaji wamesema kwamba uvamizi unaoendelea wa Urusi unakiuka sheria za kimataifa na kanuni za haki za binadamu. 

Wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua msimamo mkali dhidi ya vitendo vya Urusi ambavyo vinadhoofisha mamlaka na uadilifu wa eneo la Ukraine, na kuunga mkono Waukraine kwenye njia yao ya kupata haki na amani.

Idadi ya wasemaji walitoa maoni tofauti, wakitoa wito wa "kuepusha kuingiza siasa katika masuala ya haki za binadamu." Walisema kuwa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu "lazima ichukue msimamo usio na upendeleo na kuendeleza usitishaji wa mapema wa uhasama."

Wito kwa Shirikisho la Urusi kutoa ushirikiano

Akihitimisha mkutano huo, Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Nada al-Nashif amesema kuwa kuhusiana na kulazimishwa kuhamishwa na kufukuzwa kwa watoto wa Ukraine, pamoja na kusaidia watoto waliokimbia makazi yao na kuwezesha utafutaji wao na kuunganishwa tena na familia zao, jumuiya ya kimataifa inapaswa kulitaka Shirikisho la Urusi kutoa fursa halisi kwa mashirika ya kimataifa kwenye maeneo ya Ukraine  na amesisitiza kwamba hii ni "muhimu."

Taarifa za kina kuhusu watoto hao, amesema, zinapaswa pia kutolewa kwa mamlaka husika, kama inavyotakiwa na sheria za kimataifa za haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kwa ndugu wa karibu.

Jumuiya ya kimataifa inapaswa pia kuunga mkono uundwaji wa utaratibu madhubuti wa kuwatambua watoto hao kulingana na Al-Nashif, na hii itasaidia kazi ya mchakato huo.

Tags: Ukraine, Urusi, HRC, OHCHR, Haki za binadamu