Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuzo  amani ya Nobel Kwenda kwa Narges Mohammadi inadhihirisha ujasiri na dhamira ya wanawake wa Iran: OHCHR

Narges Mohammadi mshini wa tuzo ya amani ya Nobel 2023
© VOA
Narges Mohammadi mshini wa tuzo ya amani ya Nobel 2023

Tuzo  amani ya Nobel Kwenda kwa Narges Mohammadi inadhihirisha ujasiri na dhamira ya wanawake wa Iran: OHCHR

Haki za binadamu

Kamati ya tuzo ya amani ya Nobel mwaka huu imemtunuku mfungwa mwanaharakati wa masuala ya haki za binadamu wa Iran Narges Mohammadi tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huu wa 2023, na tayari Umoja wa Mataifa umepongeza uamuzi huo. 

Baada ya kutangazwa tu leo ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR imesema “ Kumpatia tuzo Narges Mohammadi mwanaharakati shupavu wa haki za binadamu ambaye hivi sasa anatumikia kifongo cha miaka 16 kwenye gereza la Evin mjini Tehran nchini Iran  kunasisitiza ijasiri na dhamira waliyonayo wanawake wa Iran.”

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis msemaji wa ofisi hiyo ya haki za binadamu Liz Throssell amesema “ Nadhani kilicho bayana ni kwamba wanawake wa Iran wamekuwa chanzo cha hamasa ulimwenguni . Tumeshuhudia ujasiri na kujizatiti kwao katika wakati wa ukiukwaji wa haki, vitisho, machafuko na watu kuswekwa vizuizini. Na ujasiri huu na kujizatiti huku ni kwa hali ya juu, kwani wamekuwa wakibughudhwa kwa kile wanachovaa au kutovaa, wanabanwa kisheria, kijamii na kiuchumi kwa hatua zinazochukuliwa dhidi yao.”

Kauli ya Antonio Guterres

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameongeza sauti yake akisema “Narges kupewa tuzo hiyo ni umbusho muhimu kwamba haki za wanawake na wasichana zinakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo kupitia kushitakiwa kwa wanawake watetezi wa haki za binadamu nchini Iran na kwingineko.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres

Na hivyo “ Tuzo hiyo ya amani ya Nobel ni utambuzi wa wanawake wote ambao wanapambana kwa ajili ya haki za binadamu huku wakihatarisha uhuru wao, afya zao n ahata maisha yao.”

Narges amefanyakazi kwa miaka mingi kama muandishi wa habari  na pia ni mwandishi wa vitabu na pia naibu mkurugenzi wa shirika la kiraia la Defenders of Human rights Center lililoko mjini Tehran.

Mwezi mei mwaka huu alipata tuzo ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari inayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO pamoja na wanawake wengine wawili waandishi wa habari walio gerezani pia kutokana na wimbi la maandamanoi yaliyofuatia kifo cha Mahsa Amini kilichotokea mikoni mwa polisi Septemba 2022.

Kuhusu tuzo ya amani ya Nobel

Tuzo ya Amani ya Nobel ni miongoni mwa tuzo tano za Nobel zilizoanzishwa na mbunifu raia wa Sweden , mwanaviwanda, mvumbuzi na mtengenezaji wa silaha  Alfred Nobel mwaka 1895.

Tuzo zingine za Nobel ni pamoja na ya Kemia, Fizikia, Tiba na Fasihi. Makao makuu ya tuzo hiyo ya Nobel yako Oslo Norway na tuzo ya kwanza kabisa ilitolewa 10 Desemba 1901.

Miongoni mwa waliowahi kupokea tuzo hizo ni pamoja na mshindi mdogo zaidi Malala Yousafzai 2014.

Mwaka huu mshindi amepata fedha taslim Kronor za Sweeden milioni 10 sawa na dola 911,765 na pia medali ya dhahabu ya karat 18.