Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hongera Dkt. Mukwege na Murad mmetetea maadili yetu ya pamoja:Guterres

Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka 2018 Nadia Murad katika picha hii alipokuwa akishiriki mjadala kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani
UN /Manuel Elias
Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka 2018 Nadia Murad katika picha hii alipokuwa akishiriki mjadala kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani

Hongera Dkt. Mukwege na Murad mmetetea maadili yetu ya pamoja:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewapongeza washindi wa mwaka huu 2018 wa tuzo ya amani ya Nobel Nadia Murad na  Dkt. Denis Mukwege kwa kutetetea waathirika wa ukatili wa kingono kwenye migogoro ya vita na kusema “wametetea maadili yetu ya pamoja.”

Guterres amesema , Nadia Murad amepazia sauti ukatili usioelezeka nchini Iraq wakati kundi lenye itikadi kali la Daesh lilipowalenga kwa makusudi na kwa unyama mkubwa watu wa Yazidi , hususan wanawake na wasichana.

Kama balozi mwema wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu UNODC tangu mwaka 2016 , amekuwa akipigania msaada kwa waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu na utumwa wa ngono lakini pia haki dhidi ya waliohusika na uhalifu huo.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa harakati zake zimewagusa wengi kote duniani na kusaidia kuanzishwa kwa uchunguzi muhimu wa Umoja wa Mataifa dhidi ya uhalifu mkubwa ambao ulitekelezwa dhidi yake na watu wengine wengi.

Akimgeukia Dkt. Denis Mukwege Guterres amesema “amekuwa mtu jasirimuhimuli wa kupigania haki za wanawake walioathirika na vita vya silaha na ambao wamebakwa, kunyanyaswa na kufanyiwa ukatili mwingine“

Ameongeza kuwa licha ya kupewa vitisho dhidi ya maisha yake kila wakati “ameifanya hospitali ya Panzi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kuwa ni pepponi, mahala salama pasipo na madhila”

Dkt. Denis Mukwege, muasisi na mkurugenzi wa tiba wa hospitali ya Panzi huko DR Congo, wakati uzinduzi wa ripoti ya kamisheni ya kimataifa kuhusu afya jijini New York, Marekani 20 Septemba 2016
UN/JC Mcllwaine
Dkt. Denis Mukwege, muasisi na mkurugenzi wa tiba wa hospitali ya Panzi huko DR Congo, wakati uzinduzi wa ripoti ya kamisheni ya kimataifa kuhusu afya jijini New York, Marekani 20 Septemba 2016

 

Umoja wa Mataifa umekuwa ikiunga mkono juhudi zake , na amekuwa ni sauti muhimu ya kuitanabaisha dunia kuhusu ukatili na uhalifu wa kutisha unaowakabili wanawake wakati wa vita. “akiwa ni mtaalam na daktarin bingwa wa upasuaji mwenye utu, sio tu anarekebisha miili iliyoharibiwa vibaya , bali pia anarejesha utu na matumaini kwa wanawake hao.”

Miaka 10 iliyopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja lillilaani vikali ukatili wa kingono kutumika kama silaha ya vita.”Na leo hii kamati ya Nobel imetambua juhudi za Nadia Murad na Denis Mukwege kuwa ni nyenzo muhimu kwa ajili ya amani.”

Katibu Mkuu amesema “kwa kuwatunukia tuzo hiyo watetezi hawa wawili wa utu wa binadamu, tuzo hiyo pia imewatambua waathirika wasiohesabika duniani kote , ambao mara nyingi wamekuwa wakinyanyapaliwa, wakifichwa na kusahaulika, hii ni tuzo yao pia”.

Ametoa wito “hebu na sote tuwaenzi washindi hawa wapya wa Amani kwa kusimama kidete kuwapigania waathirika wa ukatili wa kingono kila mahali.”

Tweet URL

 

Naye mwakilishi maalimu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini DRC Leila Zerrouguiakizungumzia Ushindi wa Dkt. Mukwege amesema” Nampongeza mtu ambaye amejitolea Maisha yake sio tu kwa kuwasaidia wanawake waliopitia ukatili wa kutisha wa ukiukwaji wa haki za binadamu lakini pia kwa kuwarejeshea hadhi na uwanamke wao. Na tuzi hii sio kwa ajili ya Dkt. Mukwege peke yake bali kwa taifa zima la Congo.”