Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hongera Maria Ressa na Dmitry Muratov kwa kutwaa tuzo ya amani ya Nobel 2021:UN

Picha kutoka kwenye video wakati Maria Ressa alipokuwa akishiriki mkutano wa UNESCO kuhusu uhuru wa vyombio vya habari. (Mei 4, 2020)
UNESCO
Picha kutoka kwenye video wakati Maria Ressa alipokuwa akishiriki mkutano wa UNESCO kuhusu uhuru wa vyombio vya habari. (Mei 4, 2020)

Hongera Maria Ressa na Dmitry Muratov kwa kutwaa tuzo ya amani ya Nobel 2021:UN

Amani na Usalama

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP amewapongeza waandishi wa habari Maria Ressa kutoka Ufilipino na Dmitry Muratov kutoka Urusi kwa kutwaa ushindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huu wa 2021. 

Kwa Dimitry Mutratov imeelezwa kuwa ni mshindi wa kwanza wa tuzo hii ya amani kutoka Urusi tbaada ya kusambaratika kwa muungano wa Soviet (USSR) kwani Rais Mikhail Sergeyevich Gorbachev ndiye mrusi mwingine aliyewahi kushinda tuzo hiyo mwaka 1990 chini ya muungano wa Sovieti. 

Akitoa pongezi hizo kwa niaba ya WFP kupitia taarifa yake iliyotolewa leo David Beasley amesema “Tuzo hii ni utambuzi wa kifahari wa jukumu muhimu ambalo Bi Ressa na Bw Muratov wamelifanya katika kuchagiza amani. WFP, mshindi wa mwaka 2020, inafurahi kukabitdhi tochi, ikiamini kuwa hitaji la amani la dunia ni la haraka leo hii kama ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita.” 

Beasley ameongeza kuwa WFP inajivunia kuwa mbebaji wa maoni muhimu ya Nobel kwa mwaka mzima ikijikita na jukumu muhimu la msaada wa chakula katika kujenga njia za kuelekea amani, utulivu, na ustawi kwa wote. 

WFP ilishinda tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka 2020 na ni moja ya mashirika makubwa zaidi ya kibinadamu duniani , linalookoa maisha katika hali za dharura na kutumia msaada wa chakula kujenga njia za kuelekea amani, utulivu na ustawi kwa watu ambao wanajikwamua kutokana na vita, majanga na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Pongezi zinamiminika kutoka kila kona 

 Washindi hao wameendelea kuponkea pongezi kutoka kila kona, mjini Geneva Uswisi msemajo wa ofisi ya kamishina mkuu wa Haki za binadamu  wa Umoja wa Mataifa OHCHR, Ravina Shamdasani akizungumza na waandishi wa Habari hii leo amesema “Tuzo hii ni kutambua kazi ya waandishi wa habari inayofanyika katika mazingira magumu”. 

Ameongeza kuwa mwaka jana umeshuhudia mashambulizi dhidi ya waandishi wa Habari. 

Maria Ressa ameshiriki katika mazungumzo kadhaa na kamishina mkuu wa haki za binadamu na amekuwa akishambuliwa nchini Ufilipino kwa miaka mingi, amesema Shamdasani. 

Pia amesisitiza umuhimu wa kazi ya waandishi wa Habari na kutaka walindwe kwa manufaa ya jamii. 

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO kupitia ukurasa wake wa Twitter limewapongeza washindi hao wa mwaka 2021 Maria Ressa na Dimitry Muratov kwa juhudi zao za kulinda uhuru wa kujieleza. 

UNESCO imesisitiza kwamba “Hakuna demokrasia bila uhuru wa vyombo vya Habari, na hakuna uhuru wa vyombo vya Habari bila waandishi wa Habari ambao wanasema ukweli kwa wenye nguvu.”