Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika inaweza kuwa kiungo muhimu katika minyororo ya ugavi duniani - Ripoti ya UNCTAD

Wanawake kutoka vijijini wakijifunza jinsi ya kutengeneza vifaa vya umeme wa jua.
© UN Women/Gaganjit Singh
Wanawake kutoka vijijini wakijifunza jinsi ya kutengeneza vifaa vya umeme wa jua.

Afrika inaweza kuwa kiungo muhimu katika minyororo ya ugavi duniani - Ripoti ya UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchi za Kiafrika zinaweza kuwa washiriki wakuu katika minyororo ya ugavi duniani kwa kutumia rasilimali zao kubwa za nyenzo zinazohitajika na sekta za teknolojia ya juu na soko lao la wateja linalokua, imesema Ripoti ya Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) kuhusu Maendeleo ya Kiuchumi Barani Afrika mwaka 2023 iliyozinduliwa leo jijini Nairobi, Kenya. 

Afisa Mchumi Mkuu wa UNCTAD ambaye pia ameongoza katika kuandika ripoti hii, Habiba Ben Barka anasema, “Wakati majanga ya kimataifa kama Covid, vita ya Ukraine na athari zingine zinazohusiana na tabianchi ziliathiri biashara na mnyororo wa usambazaji ulimwenguni kote kampuni nyingi za kimataifa zilianza kutafuta njia za kujenga uwezo wa kukabiliana na mitikisiko ya siku zijazo. Kwa hivyo, Ripoti ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Afrika ya mwaka 2023 inaangalia mikakati, sera, na taratibu tofauti ambazo Nchi za Afrika zinaweza kuweka ili kuunganisha baadhi ya mnyororo huo wa ugavi.” 

Minyororo ya ugavi inajumuisha mifumo na rasilimali zinazohitajika kuendeleza, kuzalisha na kusafirisha bidhaa na huduma kutoka kwa wasambazaji hadi kwa wateja.  

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa UNCTAD Rebeca Grynspan ananukuliwa akisema, "Huu ni wakati wa Afrika kuimarisha nafasi yake katika minyororo ya ugavi duniani huku juhudi za usambazaji bidhaa zikiendelea. Pia ni fursa kwa bara la Afrika kuimarisha viwanda vinavyoibuka, kukuza uchumi na kutengeneza ajira kwa mamilioni ya watu wake."  

Rebeca Grynspan, Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, UNCTAD.
© Nicholas Hopkins-Hall

Wingi wa madini na vyuma muhimu barani Afrika, zikiwemo alumini, kobalti, shaba, lithiamu na manganisi, vipengele muhimu katika tasnia zinazotumia teknolojia kubwa, vinaliweka bara hili kama kivutio kwa viwanda, kwa sababu misukosuko ya hivi karibuni iliyosababishwa na mtikisiko wa biashara, matukio ya kijiografia na kutokuwa na uhakika wa kiuchumi zinalazimisha wazalishaji kugawanya maeneo yao ya uzalishaji. 

Afrika pia inatoa faida kama vile ufikiaji mfupi na rahisi zaidi wa pembejeo za msingi, nguvu kazi ya vijana  inayofahamu teknolojia, na inayoweza kubadilika, na tabaka la kati linalokua na linalojulikana kwa kuendelea kuhitaji bidhaa na huduma za hali ya juu zaidi. 

Kuimarisha minyororo ya ugavi barani Afrika ni muhimu kwa ukuaji wa kanda 

Ripoti hiyo inaangazia kwamba kuunda mazingira yanayofaa kwa viwanda vinavyotumia teknolojia kubwa kutasaidia kuongeza mishahara katika bara hilo, ambayo kwa sasa imewekewa kima cha chini cha dola 220 kwa mwezi, ikilinganishwa na wastani wa dola 668 katika bara la Amerika. 

Ushirikiano wa kina katika minyororo ya ugavi wa kimataifa pia utaleta mseto katika uchumi wa Kiafrika, na kuongeza mnepo wao kwa majanga yajayo. 

Aidha ripoti inaeleza kuwa kupanua minyororo ya usambazaji wa nishati barani Afrika pia ni fursa ya kuharakisha hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Uwezo mkubwa wa nishati mbadala wa bara hili, hasa katika nishati ya jua, unaweza kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati vinavyotokana na mafuta. 

Afrika inahitaji uwekezaji zaidi katika nishati mbadala ili kusaidia kuziba pengo kubwa la uwekezaji na kukabiliana na vikwazo vingine kwenye utengenezaji wa paneli za miale ya jua barani humo. Hivi sasa, ni takribani asilimia 2 tu ya uwekezaji wa kimataifa katika nishati mbadala inayoenda Afrika. Ukuaji wa uwekezaji katika nishati mbadala, kama ilivyooneshwa na UNCTAD, unaweza kukuza utengenezaji wa paneli za jua barani Afrika. 

Kwa mfano, mwaka wa 2022, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilikuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa shaba barani Afrika, ikiwa na tani milioni 1.8 za metriki na zaidi ya uchunguzi na uchimbaji, nchi hiyo inaweza kuwa mahali pazuri pa kusafisha bidhaa za chuma kwa tasnia ya magari ya umeme. 

Wekeza katika miundombinu, teknolojia na ufadhili 

Nchi 17 za Afrika, zikiwemo Angola, Botswana, Ghana na Afrika Kusini, tayari zimetekeleza kanuni za maudhui ya ndani ili kusaidia ukuaji wa minyororo ya ugavi wa ndani, kukuza uhamishaji wa teknolojia, kuunda nafasi za kazi na kuongeza thamani ndani ya mipaka yao. 

Zaidi ya hayo, nchi za Afrika zinapaswa kupata kandarasi bora za uchimbaji madini na leseni za uchunguzi wa vyuma vinavyotumika katika bidhaa za teknolojia ya juu na minyororo ya usambazaji. Hii itaimarisha viwanda vya ndani na kuwezesha makampuni ya ndani kubuni, kununua, kutengeneza na kusambaza vipengele muhimu. 

Utumiaji wa teknolojia za kibunifu za kidijitali pia ni muhimu katika kuboresha michakato ya ugavi. Nchi kama vile Kenya zimepata maendeleo makubwa katika nyanja hii, na viwango vya juu vya utumiaji wa ujuzi wa kidijitali barani Afrika. 

UNCTAD inazitaka serikali kuunda sera nzuri, kukuza mazingira wezeshi ya udhibiti na kuongeza programu ili kukuza utumiaji mkubwa wa teknolojia hizi. 

Shirika hilo la biashara na maendeleo la Umoja wa Mataifa pia linasisitiza wito wake wa suluhu bora za ufadhili ili kuzipa nchi na biashara za Kiafrika mtaji na ukwasi wa bei nafuu ili kuwekeza katika kuimarisha minyororo yao ya ugavi. 

Fedha zaidi za ugavi kwa biashara ndogo ndogo 

Ripoti hiyo inasema biashara ndogo ndogo na za kati za Kiafrika zinahitaji fedha zaidi za ugavi, ambazo zitaziba pengo la muda wa malipo kati ya wanunuzi na wauzaji, zitaboresha upatikanaji wa mitaji ya kufanya kazi na kupunguza matatizo ya kifedha. 

Kulingana na ripoti hiyo, thamani ya kifedha ya soko la ugavi barani Afrika ilipanda kwa asilimia 40 kati ya mwaka 2021 na 2022, na kufika dola bilioni 41. Lakini hii haitoshi. 

Bara hilo linaweza kukusanya fedha zaidi kwa kuondoa vizuizi vya ufadhili wa ugavi, ikiwa ni pamoja na changamoto za udhibiti, mtazamo wa hatari kubwa, na taarifa zisizotosheleza za mikopo. 

UNCTAD pia inasisitiza haja ya msamaha wa madeni ili kuzipa nchi za Afrika nafasi ya kifedha ya kuwekeza katika kuimarisha minyororo yao ya ugavi, kwani kwa wastani zinalipa mara nne zaidi kwa kukopa kuliko Marekani na mara nane zaidi ya chumi za Ulaya.