Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wasimulia walichokishuhudia Karabakh

Waarmenia wa kabila ya Nagorno-Karabah wanatafuta hifadhi nchini Armenia.
© WHO/Nazik Armenakyan
Waarmenia wa kabila ya Nagorno-Karabah wanatafuta hifadhi nchini Armenia.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wasimulia walichokishuhudia Karabakh

Amani na Usalama

Watu wachache wanaokisiwa kuwa kati ya 50 hadi 100 kutoka jamii ya asili raia wa Armenia wameripotiwa kusalia katika eneo la Karabakh nchini Azerbaijan baada ya msafara wa siku za hivi karibuni kushuhudia zaidi ya watu 100,000 wakilikimbia eneo hilo, umeripoti leo ujumbe wa Umoja wa Mataifa ambao umefika eneo hilo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30.

Katika taarifa iliyotolewa na Ujumbe huo kufuatia ziara yao waliyoifanya siku ya jumapili ikiongozwa na mwakilishi mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Azerbaijan Vladanka Andreeva pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu walisikia na kujionea katika jiji la Khankendi angalau, hakukuwa na dalili za uharibifu wa majengo ya umma.

“Ujumbe ulishangazwa na namna wakazi wa eneo hilo walivyoondoka ghafla makwao na mateso waliyopitia” imeeleza taarifa hiyo ya timu ya Umoja wa Mataifa.

Timu hiyo iliongeza kuwa haikusikia kutoka kwa wenyeji waliohojiwa au wengine juu ya matukio ya unyanyasaji dhidi ya raia kufuatia usitishaji wa mapigano wa hivi karibuni.

“Timu ilisikia kutoka kwa wazungumzaji kwamba kati ya Waarmenia 50 hadi 1,000 wamesalia katika mkoa wa Karabakh.”

Wakimbizi wakijisajili katika kituo cha Goris, Armenia.
WHO
Wakimbizi wakijisajili katika kituo cha Goris, Armenia.

Hawakuona uharibifu

Wakati wa ziara yao, timu ya Umoja wa Mataifa ilisafiri kutoka Aghdam hadi Khankendi, ambako kuna wanajamii ya asili Waarmenia wanaotambulika kama Stepanakert.

Katika maeneo waliyotembelea, hakukuwa na uharibifu unaoonekana kwa miundombinu ya umma, ikiwa ni pamoja na hospitali, shule, nyumba, au miundombinu ya kitamaduni na kidini. Maduka yalikuwa yamefungwa.

Timu hiyo ilibaini kuwa Serikali ya Azerbaijan ilikuwa ikifanya maandalizi ya kurejesha huduma za afya na huduma nyinginezo katika jiji hilo.

Ujumbe huo haukuweza kuyafikia maeneo ya vijijini, lakini haukuona dalili zozote za uharibifu wa miundombinu ya kilimo au mifugo.

Njia ya Lachin

Ujumbe huo ulifuata barabara ya Lachin hadi kwenye eneo la mpakani la kuvukia, njia iliyotumiwa na Waarmenia zaidi ya 100,000 katika siku za hivi karibuni. Hawakukutana na magari ya kiraia kuelekea Armenia.

Timu hiyo imesema kwamba “ni vigumu kuamua katika hatua hii iwapo wakazi wa eneo hilo wanakusudia kurejea”, kutokana na mazungumzo waliyoweza kufanya.

Kilichokuwa wazi ni kwamba kuna haja ya kujenga imani na kujiamini, na hii itahitaji muda na juhudi kutoka pande zote, iliongeza taarifa hiyo.

Pia imetaka juhudi zote zifanywe ili kuhakikisha ulinzi wa haki za wakazi wa eneo hilo, na kuongeza kuwa timu ya Umoja wa Mataifa nchini Azerbaijan iko tayari kusaidia wakazi waliosalia wa eneo hilo na wale wanaotaka kurejea, kwa kuunga mkono Serikali ya Azerbaijan. 

Hali ilivyo nchini Armenia 

Nchini Armenia, wakimbizi wengi waliofika katika mji wa Goris ulioko mpakani wametawanyishwa maeneo mengine ya nchi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM limeripoti kwamba wengi wa wale waliotafuta hifadhi nchini Armenia walifanya safari ngumu, mara nyingi wakitembea kwa siku kadhaa kutafuta hifadhi katika mapango au mahandaki, wakivumilia hali ngumu sana.

Msemaji wa IOM Joe Lowry akiwa Yerevan, aliyeko Armenia ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuwa “Kuna ripoti za utapiamlo, hasa miongoni mwa wazee na miongoni mwa watoto, na magonjwa kama vile homa kali na homa ya mapafu.”

Afya ya akili inapewa kipaumbele

Kwa ushirikiano wa karibu na serikali ya Armenia, timu za Umoja wa Mataifa nchini humo zinahakikisha msaada wa afya ya akili kuwa kipaumbele cha juu kwa wakimbizi. 

Siku ya Jumatatu, IOM ilifungua kliniki mbili tembezi, na nne zaidi zitafunguliwa katika siku zijazo.

Kliniki hizo zitakuwa na mwanasaikolojia aliyefunzwa kusaidia watu na mahitaji yao ya haraka ya afya ya akili na kisaikolojia, na kuwapa rufaa kwenda kupata huduma zaidi kama inahitajika, amesema Lowry. 

Huduma mpya

Kwa kuzingatia idadia kubwa ya watu hao takriban 100,000 katika nchi yenye wakazi karibu milioni tatu, kutakuwa na mahitaji makubwa ya upanuzi wa huduma za kitaifa. Hii ni pamoja na kuimarisha taasisi za elimu na vituo vya afya.

“Watu watahitaji shule mpya, ambazo itabidi zijengwe, haitakuwa suala la kuongeza viti vinne au vitano zaidi katika darasa , shule mpya au majengo mapya kwenye shule ambazo tayari zinatoa huduma yatalazimika kujengwa, na hospitali pia.” Msemaji huyo wa IOM ameeleza. 

Amesisitiza kuwa watu waliofika pia watahitaji usaidizi wa kujikimu kimaisha, kama vile ajira na makazi mapya. 

Wakati huo huo, jumuiya ya mwenyeji pia itahitaji msaada.