Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wamiminikao Armenia kutoka Kabarakh wasimulia yaliyowasibu

Wakimbizi wakijisajili katika kituo cha Goris, Armenia.
WHO
Wakimbizi wakijisajili katika kituo cha Goris, Armenia.

Wamiminikao Armenia kutoka Kabarakh wasimulia yaliyowasibu

Wahamiaji na Wakimbizi

“Safari ilikuwa ngumu sana, tulikuwa barabarani kwa saa kati ya 26 hadi 29.” Ni simulizi ya mmoja wa wakimbizi zaidi ya 100,000 wanaomiminika Armenia wakitokea eneo la Karabakh linalozozaniwa kati ya Armenia na Azerbaijan. 


 

Tweet URL

Mkimbizi huyu mwenye asili ya Armenia akiwa Goris jimboni Syunik nchini Armenia anasema njiani msururu wa magari ulikuwa ni mrefu, “ilikuwa vigumu kufika hapa. Mama yangu ni mgonjwa, na kaka yangu ana watoto na wajukuu.” 

Nahitaji kumhudumia binti yangu 

Simulizi za aina hiyo ni nyingi hivi sasa nchini Armenia, ambako tayari shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, linahaha kusaidia wakimbizi hao wanaoendelea kumiminika nchini humo kila uchao. 

UNHCR inasema wakimbizi hao 100,000 wamewasili ndani ya kipindi kisichozidi wiki moja. 

Mkimbizi mwingine aitwaye Marine anasema, “leo tunakwenda Yerevan kusajiliwa na kupata pahala pa kuishi, tuko wanne, Nahitaji kumhudumia binti yangu mdogo.” 

Serikali ya Armenia kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na mashirika yakiraia imebeba jukumu la kuwalinda na kusaidia wakimbizi. 

Wakimbizi hawana chochote wanahitaji msaada 

Angela Moore ni Afisa ulinzi wa UNHCR anasema wakimbizi wamewasili Goris  baada ya kutumia siku kadhaa njiani. Wamewasili hapa wamechoka, wameacha kila kitu chao nyumbani.  

Bi. Moore anasema “watu wanahitaji msaada wa dharura. UNHCR imekuweko kwenye eneo hili  mapema kuwapatia wahitaji misaada ya dharura, vitanda na magodoro. Tunayo malori ambayo yatawasili na kuendelea kutoa msaada kwa wale wenye uhitaji zaidi.”