Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dharura ya Karabakh inaongezeka, maelfu bado wanamiminika Armenia

Wakimbizi wakiwasili katika mji wa mpaka wa Goris nchini Armenia.
© UNHCR/Karen Minasyan
Wakimbizi wakiwasili katika mji wa mpaka wa Goris nchini Armenia.

Dharura ya Karabakh inaongezeka, maelfu bado wanamiminika Armenia

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya wakimbizi 100,000 kutoka eneo la Karabakh wamekimbilia nchini Armenia katika muda wa chini ya wiki moja na mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) hii leo.

Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi  kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X amesema "Wengi wana njaa, wamechoka na wanahitaji msaada wa haraka. UNHCR na wadau wa masuala ya kibinadamu wanaongeza msaada wao kwa mamlaka ya Armenia, lakini msaada wa kimataifa unahitajika haraka sana."

Taarifa iliyotolewa mapema hii leo na UNHCR ilieleza kuwa watu 65,000 tayari wamesajiliwa katika vituo vinavyoendeshwa na Serikali ambapo kuna misusruru mirefu.

Wasiwasi na hofu

Shirika la UNHCR linawasaidia wakimbizi kwa kuwapatia misaada muhimu, amesema mwakilishi wake nchini Armenia Kavita Belani, ambaye yupo eneo la kuwasaidia wakimbizi hao tangu siku ya kwanza ya mgogoro.

Watu wamechoka. Hii ni hali ambapo wameishi kwa chini ya miezi tisa kizuizini. Wanapoingia, wamejaa wasiwasi, wanaogopa, wanahofu na wanataka majibu ya nini kitatokea baadaye.”

Bi. Belani amesema mahitaji ya dharura zaidi ni pamoja na msaada wa kisaikolojia, dawa na makazi kwa kila mtu, kutokana na wingi wa wanaofika, pamoja na msaada unaolengwa kwa walio hatarini zaidi ambao ni wazee na watoto.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF limewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswis kwamba asilimia 30 ya wanaowasili ni watoto wadogo na wengi wametenganishwa na familia zao.

Mashirika ya UN kazini

UNICEF inashirikiana na mamlaka kuhakikisha kuwa ufuatiliaji wa familia unafanywa mara moja ili watoto waweze kuunganishwa na ndugu zao.

UNHCR inaongoza kwenye uratibu wa misaada kwa kushirikiana na mashirika ya wakimbizi ili kusaidia juhudi za Serikali ya Armenia.

Mwakilishi wa UNHCR, Bi. Belani amesema wapo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha ombi la ufadhili. Amesisitiza kuwa wakati mpango wa kukabiliana na hali hiyo ulikuwa wa muda wa miezi sita, Umoja wa Mataifa ulikuwa tayari unafikiria juu ya msaada wa muda mrefu ili kusaidia Armenia kuwasaidia wakimbizi wapya wanaowasili.

Mapema wiki hii, Alice Wairimu Nderitu, Mshauri Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kuzuia Mauaji ya Kimbari, alinukuliwa akieleza "wasiwasi wake mkubwa" juu ya hali inayoendelea na kutoa wito "juhudi zote zifanywe" kuhakikisha ulinzi na haki za binadamu za jamii ya asili ya Armenia waliobaki katika eneo hilo na wale walioondoka.

Wakimbizi wakiacha mali zao kwenye hema huko Goris, Armenia.
© UNHCR/Karen Minasyan
Wakimbizi wakiacha mali zao kwenye hema huko Goris, Armenia.

Ufuatiliaji wa familia

Wasiwasi mkubwa kwa wasaidizi wa kibinadamu ni kwamba watoto wengi wametenganishwa na familia zao, alisema Regina De Dominicis, Mkurugenzi wa Kanda wa UNICEF na Mratibu Maalum wa Majibu ya Wakimbizi na Wahamiaji barani Ulaya.

“Kwa hivyo tunafanya kazi kwanza kwa kutoa msaada wa kisaikolojia na kufanya kazi na wizara na serikali za mitaa pia kuhakikisha kuwa ufuatiliaji wa familia unafanywa mara moja na familia zinaweza kuungana,”

Tangu Jumapili, vijiji vya Armenia karibu na mpaka na eneo la Karabakh vimegeuka kuwa kambi za muda za wakimbizi.

Baadhi ya wale wanaotafuta hifadhi walikuwa na dakika chache za kufungasha virago vyao ili kuondoka na magari, mabasi na malori ya ujenzi, walisema. 

Ingawa wakimbizi wengi walionesha ahueni ya kufika Armenia kutoka Azerbaijan, bado wanasalia wakiwa na kiwewe na kuchanganyikiwa kuhusu mustakabali wao wa siku zijazo, limesema Shirikisho la Kimataifa la Mashirika ya Msalaba Mwekundu na Mwezi Nyekundu (IFRC).

“Ilikuwa dhahiri kwa kila mtu - watoto, wanaume, wanawake, wazee – muonekano wa nyuso za wale wanaoingia kwenye vituo vya usajili yanazungumza sana,” alisema Hicham Diab wa IFRC, akizungumza kutoka mji mkuu wa Armenia Yerevan.

Kila uso unasimulia hadithi

“Kila uso unasimulia hadithi ya shida, lakini pia ya matumaini, wakijua wako mahali ambapo wanaweza kupokea msaada.”

Hali hiyo ya kukata tamaa ilichangiwa na mlipuko uliotokea Jumatatu katika kituo cha mafuta katika eneo la Karabakh na kuua takriban watu 68, kulingana na taarifa zilizotolewa na mamlaka za eneo hilo.

Watu wengine 105 bado hawajulikani walipo kufuatia mlipuko huo, ambao unaripotiwa kutokea huku watu wengi wakipanga foleni kupata mafuta ya kuwasaidia kuondoka.

“Kipaumbele cha Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) katika siku za hivi karibuni kimekuwa juu ya shughuli za kuokoa maisha, ikiwa ni pamoja na uhamisho wa majeruhi katika hospitali nchini Armenia kwa matibabu na kuleta vifaa vya matibabu,” amesema Carlos Morazzani, Meneja Operesheni za ICRC.

Ameongeza kuwa katika wiki iliyopita tumefanaikiwa kuwahamisha karibu watu 130 kwa ajili ya matibabu na baada ya mlipuko huo, waliongeza ushirikiano wao na mamlaka zote za kikanda.

Upanuzi wa operesheni za Umoja wa Mataifa 

Timu ya Umoja wa Mataifa nchini Armenia, ikiongozwa na kaimu Mratibu Mkaazi Nanna Skau, inashirikiana na Serikali kusaidia ongezeko la watu wanaoongezeka kwa kasi.

Kulingana na takwimu rasmi zilizotolewa na mamlaka hivi takribani watu 100,000 wamevuka hadi Armenia.