Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tume ya UN yasikitishwa na vitendo vya kikatili vya Urusi nchini Ukraine

Mvulana wa miaka 4 wa Ukraine anacheza katika kituo cha masomo huko Bratislava, Ukrainia.
© UNICEF/Gorana Banda
Mvulana wa miaka 4 wa Ukraine anacheza katika kituo cha masomo huko Bratislava, Ukrainia.

Tume ya UN yasikitishwa na vitendo vya kikatili vya Urusi nchini Ukraine

Haki za binadamu

Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchunguzi kuhusu Ukraine imeripoti leo kwa Baraza la Haki za Kibinadamu kwamba kuna ushahidi kuwa wanajeshi wa Urusi wanaendelea kufanya uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

Katika taarifa yao waliyoiwasilisha leo katika ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi, Tume hiyo ya Huru ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kinagaubaga kwamba wanajeshi wa Urusi wanafanya mashambulizi haramu ya kutumia silaha za milipuko, mateso, unyanyasaji wa kingono na kijinsia, na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati.

Wakati wa uwasilishaji kwa Baraza la Haki za Kibinadamu, Tume imeripoti kwamba imerekodi mashambulizi ya silaha za milipuko kwenye majengo ya makazi, kituo cha matibabu kinachofanya kazi, kituo cha reli, mgahawa, maduka na maghala ya biashara. Mashambulizi haya yalisababisha vifo vya raia, uharibifu wa miundombinu muhimu, na kukatizwa kwa huduma muhimu.

Uchunguzi zaidi

Taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya Habari imeeleza kuwa Tume inachunguza sababu ya uvunjaji wa bwawa la Nova Kakhovka na athari zake kwa raia.

Wakati huo huo Tume imeeleza kuwa uchunguzi wake huko Kherson na Zaporizhzhia unaonesha matumizi makubwa na yaliyoratibiwa ya utesaji yanayotekelezwa na vikosi vya jeshi la Urusi dhidi ya watu wanaoshutumiwa kuwa watoa habari wa vikosi vya jeshi la Ukraine. Katika matukio fulani, mateso yalifanywa kwa ukatili kiasi kwamba yalisababisha kifo.

Mtu mmoja ambaye  aliteswa kwa kupigwa na mshtuko wa umeme aliiambia tume kwamba kila wakati alipojibu kwamba hajui wala hakumbuki jambo Fulani, walimpiga shoti za umeme na hajui hali hiyo ilidumu kwa muda gani kwani kwake aliona ni kama milele.  

Katika eneo la Kherson, askari wa Urusi waliwabaka na kufanya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake wa umri wa kuanzia miaka 19 hadi 83, Tume iligundua. Mara kwa mara, wanafamilia waliwekwa katika chumba cha karibu na hivyo kulazimika kusikia ukiukaji unaofanyika.

Tume imeendelea kuchunguza hali za kibinafsi za uhamisho wa madai ya kuhamishwa  watoto wa Ukraine bila usimamizi wowote na kuwapeleka Urusi. 

Mauaji ya kimbari

Tume pia ina wasiwasi kuhusu madai ya mauaji ya kimbari nchini Ukraine. Kwa mfano, baadhi ya matamshi yanayosambazwa katika Urusi na vyombo vingine vya habari yanaweza kujumuisha uchochezi wa mauaji ya kimbari. Tume inaendelea na uchunguzi wake kuhusu masuala hayo.

Tume inasisitiza wasiwasi wake mkubwa juu ya ukubwa na uzito wa ukiukaji ambao umefanywa nchini Ukraine na vikosi vya kijeshi vya Urusi na inasisitiza haja ya uwajibikaji. Pia inakumbuka hitaji la mamlaka ya Ukraine kuchunguza kwa haraka na kwa kina visa vichache vya ukiukaji wa sheria uliofanywa na vikosi vyao wenyewe. 

Taarifa hii mpya ya Tume kwa Baraza la Haki za Kibinadamu ni mwendelezo wa ripoti zake za awali, ikijumuisha Waraka wake wenye matokeo ya uchunguzi wa kina, iliyotolewa tarehe 29 Agosti 2023.

Tangu kuanzishwa kwake, Tume imesafiri zaidi ya mara kumi Kwenda Ukraine. Wakati wa uchunguzi wake, wanachama na wachunguzi wake walikutana na mamlaka za serikali, mashirika ya kimataifa, mashirika ya kiraia, na wadau wengine husika.

Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ukraine ni chombo huru kilichopewa mamlaka na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, pamoja na mambo mengine, kuchunguza ukiukwaji wote wa haki za binadamu na ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu, na uhalifu unaohusiana nao katika muktadha wa uchokozi dhidi ya Ukraine unaofanywa na Shirikisho la Urusi. Tume itawasilisha ripoti za shughuli zake kwa Baraza Kuu mwezi Oktoba mwaka huu 2023, na kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa mnamo Machi mwaka kesho 2024.