Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhalifu wa kivita umetendwa Ukraine, uchunguzi wa tume huru ya UN wabaini 

Izyum, mji pembezoni mwa mto Donets katika eneo la Kharkiv, mashariki mwa Ukraine.
Unsplash/Oleksandr Brovko
Izyum, mji pembezoni mwa mto Donets katika eneo la Kharkiv, mashariki mwa Ukraine.

Uhalifu wa kivita umetendwa Ukraine, uchunguzi wa tume huru ya UN wabaini 

Haki za binadamu

Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa liliunda Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi kuhusu Ukraine kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu, ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu, na uhalifu mwingine ambao unaweza kuwa umefanywa katika muktadha wa uchokozi wa Shirikisho la Urusi dhidi ya Ukraine.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa Tume huru ya Umoja wa Mataifa katika matukio ya mikoa ya Kyiv, Chernihiv, Kharkiv na Sumy, ni wazi uhalifu wa kivita umetendeka nchini Ukraine baada ya Urusi kuivamia nchi hiyo, taarifa iliyotolewa Ijumaa hii jijini Geneva, Uswisi NA Ofisi ya kamishna mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) imeeleza.   

Tume imeandika ukiukaji, kama vile matumizi haramu ya silaha za milipuko, mashambulizi ya kiholela, ukiukaji wa utu kibinafsi, ikiwa ni pamoja na kunyongwa, kuteswa na kutendewa vibaya, na unyanyasaji wa kingono na kijinsia. Pia tume imegundua kuwa haki za watoto zimekiukwa. 

Uchunguzi wa unyanyasaji wa kingono na kijinsia umeonesha kuwa baadhi ya askari wa Shirikisho la Urusi walifanya uhalifu huo. Umri wa waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia na kingono ulikuwa kati ya miaka minne hadi 82. 

Katika ziara ya Ukraine mnamo Juni 2022, Tume ilishuhudia uharibifu katika majengo ya makazi na miundombinu yenye watu wengi, uharibifu uliosababishwa na silaha za milipuko zilizo na athari za eneo pana ikijumuisha shule na hospitali. Idadi ya mashambulizi ambayo Tume ilichunguza yalifanywa bila kutofautisha kati ya raia na wapiganaji. 

"Tulishangazwa na idadi kubwa ya watu waliouawa katika maeneo ambayo tulitembelea," Erik Møse, Mwenyekiti wa Tume, amesema akiongeza kwa kusema, "tuna wasiwasi juu ya mateso ambayo mzozo wa kimataifa wa kijeshi nchini Ukraine umeweka kwa raia." 

Aliongeza kuwa Tume hiyo kwa sasa inachunguza mauaji katika miji na makazi 16, na imepokea tuhuma za kuaminika kuhusu matukio mengi zaidi. Mambo ambayo yameonekana mara kwa mara katika uhalifu huu ni pamoja na kuwekwa kizuizini kwa waathiriwa na dalili zinazoonekana za kunyongwa, kama vile mikono iliyofungwa mgongoni, majeraha ya risasi kichwani, na kukatwa koo. 

Mashahidi waliipatia Tume taarifa za dhuluma na mateso yaliyofanywa wakati wa kifungo kisicho halali. Baadhi ya waathiriwa waliripoti kwamba baada ya kuzuiliwa kwa mara ya kwanza na vikosi vya Urusi huko Ukraine, walihamishiwa Urusi na kushikiliwa kwa wiki kadhaa katika vituo vya kizuizini, ambapo waliteswa na kutendewa vibaya. 

Tume pia imegundua kuwa watoto walikabiliwa na milipuko ya mara kwa mara, ukiukaji, kulazimishwa kuhama na kutenganishwa na wanafamilia, pamoja na ukiukwaji mwingine. 

Katika maeneo manne ambapo uchunguzi ulifanyika, Kyiv, Chernihiv, Kharkiv na Sumy, Tume ilishughulikia matukio mawili ya unyanyasaji dhidi ya askari wa Urusi yaliyotekelezwa na vikosi vya Ukraine ingawa matukio hayo ni machache kwa idadi, lakini matukio kama hayo yanaendelea kuangaliwa kwa ukaribu na Tume. 

Tume ilitembelea miji na makazi 27 na imewahoji waathiriwa na mashahidi zaidi ya 150. Wachunguzi wake walikagua maeneo ya uharibifu, makaburi, mahali pa vizui na mateso, pamoja na mabaki ya silaha, nakuangalia idadi kubwa ya nyaraka na ripoti. 

Katika uchunguzi wake, Tume ilikutana na mamlaka za Serikali, mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia, na wadau wengine husika.