Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres aunga mkono uchunguzi wa mauaji ya raia huko Bucha

Mpakani mwa Ukraine na Moldova katika eneo la Palanca wakimbizi wakiwa kwenye foleni.
© UNICEF/Vincent Tremeau
Mpakani mwa Ukraine na Moldova katika eneo la Palanca wakimbizi wakiwa kwenye foleni.

Guterres aunga mkono uchunguzi wa mauaji ya raia huko Bucha

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres  hii leo ameongeza sauti yake kwenye wito wa kimataifa unaozidi kutolewa wa kutaka uchunguzi wa madai ya uhalifu wa kivita kufuatia mauaji ya raia kwenye mji wa Bucha nchini Ukraine.
 

Maoni ya Katibu Mkuu yanafuatia picha za kutisha kutoka mji wa Bucha ulioko viunga vya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, picha zinazoonesha maiti za mamia ya watu, baadhi wakiwa wapegwa risasi na mikono  yao imefungwa nyuma  na wengine wamechomwa moto au wakiwa kwenye makaburi ya pamoja, kwenye maeneo ambayo awali yalikaliwa na majeshi ya Urusi.

Bwana Guterres ambaye alikuwa anahutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, amesema uchunguzi huru unahitaijka ili uwajibikaji uweze kuwa wa uhakika.

Ameelezea janga la Ukraine ambalo limechochwa na uvamizi uliotekelezwa na Jirani yake Urusi, kama “moja ya changamoto kubwa zaidi kuwahi kukabili mfumo wa kimataifa na muundo wa amani duniani ulioasisiwa na Chata ya Umoja wa Mataifa.”

Hadi leo hii, mashambulizi ya  Urusi yamesababisha watu zaidi ya milioni 10 kufurushwa makwao ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, amesema Katibu Mkuu.

Miongoni mwao hao, zaidi ya milioni 4.2 wamevuka mpaka wa Ukraine na kukimbilia nchi jirani, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR,. Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO linasema mashambulizi yasiyochagua maeneo yameharibu vituo vya afya 86 kati ya tarehe 24 mwezi Februari hadi tarehe 2 mwezi huu wa Aprili.

Kwa kuzingatia hali ya udharura wa sasa, Katibu Mkuu amesema amemuagiza Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya dharura, Martin Griffiths kusafiri hadi Urusi na Ukraine kushinikisha sitisho la haraka la mapigano kwa misingi ya kibinadamu.

Violeta amesafiri kutoka Odessa akiwa na Daniel mwenye umri wa miak a12 na Angelina umri wa miak a11 pamoja na paka wao wawili.
© IOM/Monica Chiriac
Violeta amesafiri kutoka Odessa akiwa na Daniel mwenye umri wa miak a12 na Angelina umri wa miak a11 pamoja na paka wao wawili.

Maiti ‘wamenajisiwa’

Huko Geneva, Uswisi nako, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu, Michelle Bachelet amelaani vikali matukio ya Bucha na kuelezea kuwepo kwa uwezekano wa  uhalifu wa kivita, ambapo ofisi yake imeelezea kuwa tukio la Bucha limeashiria hali mbaya zaidi kwenye vita hivyo kwa kuwa miili ya watu imenajisiwa.

“Kile tulichoona kinaibuka Bucha na maeneo mengine, ni dhahiri kuwa ni tukio linalochukiza… dalili zote za waathirika kuwa walilengwa moja kwa kwa moja na kuuawa,” amesema Liz Throssell, msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR.

Kabla ya matukio ya Bucha kufichuliwa, ofisi hiyo ilikuwa tayari imeelezea matukio ya mashambulizi yasiyochagua meaneo kuwa ni dalili za uhalifu wa kivita.

“Unaweza kusema kuwa kulikuwa na kifaa cha kijeshi, lakini ni vigumu sana kuona kifaa cha kijeshi kwani unaona ni mtu amelala barabarani akiwa amepigwa risasi kichwani, au mwili wake umechomwa moto,” amesema Bi. Throssell akizungumza na wanahabari Geneva, USwisi.

Ushahidi bandia

Akizungumzia suala kuwa hoja za Urusi kuhusu kilichotokea Bucha ni uzushi na hazina msingi wowote, Bi. Throssell amesema kuwa wachunguzi wa haki za binadamu walifuatilia kwa makini kanuni za uchunguzi na kuthiibtisha video au picha zinazotoka huko Bucha kuwa zinaweza kuwa uhalifu wa kivita.

“Hivi sasa inatafiti kupata jina la raia waliokufa, tarehe kama itawezekana ya lini mtu huyo alikufa na jinsi alivyokufa na hii itasaidia kubaini nani aliwaua” amesema akiongeza kuwa hadi sasa bado haijathibitishwa iwapo itakuwa uhalifu wa kivita umetekelezwa au la.

Haki huchukua muda

“Hatusemi kuwa tukio hili mahsusi ni uhalifu wa kivita, la hasha! Hatuwezi kuthibitisha hilo sasa na ndio maana tunahitaji uchunguzi wa kina… haki na uwajinikaji huchukua muda: kile muhimu ni kwamba kazi inanedelea ili kuhakikisha uwajibikaji.

Punde baada ya Urusi kuvamia Ukraine, wachunguzi wa ngazi ya juu wa haki za binadamu waliteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu la  Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi.

Jukumu la Tume hiyo Huru ya Kimataifa kuhusu Ukraine ni pamoja na kukusanya ushahiid kutoka kwa manusura wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu lakini chombo hicho si cha kimahakama kwa hiyo hakina uwezo wa kuamua kuwa matukio yatakuwa uhalifu wa kivita.

Uchunguzi mwingine ulioanzishwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC juu ya madai ya ukiukwaji wa Mkataba wa Kimatifa wa Geneva, nao unaendelea, kufuatia ombi la nchi 39 wanachama wa ICC.

Madhara mnyumbuliko

Tukirejea katika Baraza la Usalama, Katibu Mkuu Guteres ameongeza kuwa madhara ya vita vya Ukraine yamevuka mpaka na kuathiri hasa nchi zinazoendelea, imevuruga mnyororo wa usambazaji wa bidhaa duniani na kuchochea kupanda kwa bei za bidhaa kuanzia chakula, nishati, mbolea kwa kuwa ndio bidhaa zinazoongozwa kusambazwa na Ukraine na Urusi.

“Katika mwezi uliopita pekee, bei ya ngano imeongezeka kwa asilimia 22, mahindi asilimia 21 na shayiri asilimia 31,” amesema Katibu Mkuu kabla ya kueleza wasiwasi kubwa nchi 74 zinazoendelea zikiwa na idadi ya watu bilioni 1.2 ziko hatarini zaidi kutokana na kuongezeka kwa bei za mafuta, mbolea na chakula.