Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde Chonde ruhusuni raia kwenye mzozo Ukraine waondoke salama

Tarehe 5 mwezi Machi 2022 wananchi kutoka Ukraine wakiwa kwenye treni kuelekea Przemysly, Poland.
© UNICEF/Alexsey Filippov
Tarehe 5 mwezi Machi 2022 wananchi kutoka Ukraine wakiwa kwenye treni kuelekea Przemysly, Poland.

Chonde Chonde ruhusuni raia kwenye mzozo Ukraine waondoke salama

Haki za binadamu

Hii leo huko Geneva, Uswisi, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ametumia hotuba yake ya mwaka kwa Baraza la Haki za Binadamu kurejelea wito wake wa kumaliza kwa amani kwa chuki kati ya Ukraine na Urusi huku akitaka pande zote kuchukua hatua kulinda na kuruhusu raia walionasa kwenye maeneo ya mapigano ili waweze kuondoka salama. 

 

Bachelet amesema msingi wa wito wake huo ni ripoti ya kwamba nchini Ukraine katika maeneo yaliyotwaliwa na vikundi vilivyojihami mashariki mwa nchi hiyo kuna taarifa za kushikiliwa kiholela kwa wanaharakati wanaotetea Ukraine.

“Tumepokea pia taarifa za vipigo kwa watu wanaoonekana kuunga mkono Urusi kwenye maeneo ambako yako chini ya serikali ya Ukraine. Narejelea wito wangu wa haraka wa kumalizwa kwa chuki hizo kwa njia ya amani,” amesema Bachelet.

Huko Urusi nako amesema fursa za watu kujadili au kukosoa sera za umma ikiwemo Urusi kuvamia Ukraine, zinazidi kubinywa na kudhibitiwa.

Watu 12,700 wamekamatwa kiholela nchini Urusi kwa sababu ya kuandamana kwa amani, kupinga vita na wanatakiwa kutumia tu misamiati rasmi iliyopitishwa na serikali.

“Bado nina hofu kubwa juu ya matumizi ya sheria kandamizi ambazo sio tu zinazuia raia kutekeleza haki  yao ya kisiasa bali pia zinaharamisha tabia zisizo za ghasia,” amesema Bachelet.

Ofisi ya Bi. Bachelet tangu kuanza kwa vita tarehe 24 mwezi uliopita hadi leo imerekodi mauaji ya watu 406 na wengine 801 wamejeruhiwa nchini Ukraine.

Hata hivyo anaamini idadi inaweza kuwa kubwa kwa kuwa mapigano yanayoendelea yanazuia uwezo wao wa kuthibitisha taarifa za vifo maeneo mengi nchini humo.